Mbowe amjibu Samia kuhusu uchaguzi

MUDA mfupi baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumwapisha Mohamed Mchengerwa kuwa waziri anayeshugulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), na kumpa ujumbe maalumu kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa 2014, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)  Freeman Mbowe, amejibu mapigo.

“Nimemsikia Rais Samia akiapisha mawaziri. Amesema wazi kabisa kwamba amemteua Mchengerwa kuongoza TAMISEMI kwa sababu mwakani kuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji.

“Samia amesema amemteua Mchengerwa kwasababu mwakani kuna kivumbi…na amesema kivumbi kwasababu anaijua shughuli yetu CHADEMA. Anasema eti amemteua kwasababu anamjua sana na anataka akaweke mambo sawasawa.

“Ni hivi…wasifikiri tupo kwenye enzi za Magufuli. Chadema tuko imara na tutashinda kwa sababu Watanzania wote wameichoka CCM. Na aweke ndugu zake zote, bado tutawatandika,” alisema Mbowe na kushangiliwa na wananchi.

Mbowe alisema hayo leo wakati akihutubia maelfu ya wananchi wa Nyashimo, Jimbo la Busega, mkoani Simiyu.

Alisema Mchengerwa hataweza kuokoa Chama cha Mapinduzi (CCM) kisianguke katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, kwani tayari Watanzania wamechoka Chama cha Mapinduzi (CCM).

Uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, umepangwa kufanyika mwakani.

Kwa mujibu wa sheria, uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji. umekuwa ukisimamiwa na Waziri wa TAMISEMI, ambaye, pamoja na mambo mengine, amepewa dhamana ya kuandaa kanuni na maadili ya uchaguzi, kufanya maandalizi na kuendesha uchaguzi.

Katika Mkutano wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), uliofanyika hivi karibuni jijini Dar-es-Salaam, na kupokea maoni ya wadau kuhusu maboresho ya sheria na mifumo ya uchaguzi, wadau mbalimbali wa demokrasia, ikiwemo CHADEMA, pamoja na mambo mengine, walipinga vikali, uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji kusimamiwa na TAMISEMI, kwani Waziri mwenye dhamana na wizara hiyo pamoja na chama chake (CCM) ni sehemu ya washindani katika uchaguzi huo, hali inayofanya kuwe na mgongano mkubwa wa kimaslahi na kuufanya uchaguzi huo kukosa taswira ya uchaguzi huru na haki.

CHADEMA imependekeza ama kuandikwe katiba mpya kabla ya uchaguzi au kufanyike marekebisho muhimu katika katiba ya sasa na sheria za uchaguzi, ili kuruhusu kuanzishwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi, ambayo, ipatiwe pia jukumu la kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, mbali na uchaguzi mkuu.

Like