BARUA YA WAZI KWA RAIS SAMIA (1)

Rais Samia Suluhu Hassan

YAHUSU BANDARI, UWEKEZAJI NA HATIMA YA UCHUMI WETU.

Mheshimiwa Rais, Amani iwe Nawe!

Ni imani yangu kuwa barua hii inakukuta ukiwa mwenye afya njema, ukiendelea na majukumu ya kulitumikia taifa letu.

Nianze kwa kwa kukupongeza kwa kazi ngumu ya kuliongoza taifa letu kwenye nyakati zenye changamoto nyingi za kiuchumi. Pamoja na hayo, kwa muda uliokaa madarakani, ni hakika umeonesha uwezo, uzalendo, maono, bidii na uvumilivu. Umeonesha kuwa kuongoza ni kumulika njia na siyo kuelekeza, kusikiliza na si kufoka, kushirikisha na si kuamrisha, kufikika na si kutisha na muhimu zaidi, kuwa mtoa matumaini badala ya kutamausha.

Mh rais, ninazo sababu kuu mbili za kuandika barua hii.

Mosi, ni kuchangia kwenye mjadala ya jinsi ya kufikiri kuhusu uchumi wetu. Nitatumia mwanya huu kujadili masuala madogo lakini ya msingi kwenye kupanga na kuendesha uchumi wetu.

Nitajadili mambo haya kwa kutumia msingi mkuu wa wachumi (ambao wewe ni mmoja wao) wa kuona yale yasiyoonekana kwa kutumia nadharia.

Pili, ni kwa sababu, tunaye rais ambaye ni mchumi na makamu wake mchumi kwa wakati mmoja. Ni maoni yangu kuwa, huu unaweza kuwa wakati maalumu zaidi kuibua mjadala wa jinsi ya kufikiri kuhusu uchumi wetu.

Mheshimiwa rais, hata hivyo, si nia yangu kujikita kwenye lawama kwani kama ujuavyo, si kazi ya wachumi kujishughulisha na lawama.

Kazi yetu kuu ni kufikiri, kubuni na kuchambua sera muafaka za jinsi ya kutumia rasilimali hafifu zilizopo kwa ufanisi na uendelevu. Lawama si moja ya rasilimali hizo. Kwa hiyo, haitakuwa kazi yangu ya msingi kujishughulisha nazo kwenye barua hii.

Mheshimiwa rais, barua yangu hii ndefu itajikita kwenye maeneo makuu sita:

  1. Uhusiano wa Sheria, Biashara na Uchumi.
  2. Safari kutoka kwenye Rasilimali za Asili kuzifanya Rasilimali za Kiuchumi.
  3. Dhana za Uchumi na Maendeleo.
  4. Uchambuzi wa Sera badala ya Miradi Kielelezo.
  5. Mawasiliano kama Zana Kuendesha Uchumi.
  6. MAPENDEKEZO

Mheshimiwa rais, nchi yetu kwa takribani  miezi miwili sasa, iko kwenye mjadala mzito juu ya mkataba 2q ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Dubai. Japo mkataba huu unahusu ushirikiano wa kiuchumi, mjadala mkuu umejikita kwenye bandari ya Dar es Salaam.

Na si kwa makosa, lakini ni kwa sababu ya hoja maridhawa za kwa nini bandari ya Dar es Salaam iboreshwe na kwa mawanda mapana, na bandari zetu kwa ujumla.

Mheshimiwa rais, pamoja na hoja kubwa na nzito kujikita kwenye bandari, ninafahamu kuwa mjadala mkubwa kupitia yanayojiri sasa, unatakiwa kuwa wa kiuchumi zaidi. Hii ni kwa sababu mjadala huu, kutokana na mkataba wenyewe, unaibua maswali ya uchumi wetu ambayo hayawezi kujibiwa na hoja za kibiashara zinazomithilika kuwa ndicho kitovu cha mkataba wenyewe.

Kisheria, kimantiki, kidiplomasia na kifalsafa, mkataba huu ni wa kiuchumi zaidi kuliko kuwa wa kibiashara kama nitakavyoeleza hapo baadaye Zaidi ni kuwa; tumekuwa na mijadala mikubwa kwa miaka 30 sasa, ya jinsi gani mikataba mithili ya huu kwenye rasilimali zetu inatusaidia kiuchumi.

Mheshimiwa rais, japo sitajikita kwenye kuchambua mkataba kwa vifungu na mantiki za kisheria kwa sababu kazi hiyo imeshafanyika sana, nitatumia mkataba huu kama nguzo ya uchambuzi.

BIASHARA KAMA MATOKEO YA UCHUMI.

Mheshimiwa rais, napenda kutumia mwanya huu kupitia hoja ya bandari, kueleza walau kidogo changamoto yetu kubwa kwenye kuendesha uchumi. Changamoto hii imejikita kwenye swali ambalo wanafunzi wa kidato cha kwanza wa somo la Biashara huwa wanaulizwa, ambalo ni; “Je, biashara ni sehemu ya uchumi au uchumi ni sehemu ya biashara?”

Nchi zinaendeshwa na fikra za kiuchumi ili kujibu swali la jinsi gani rasilimali hafifu lakini zenye mahitaji mengi zinavyoweza kutumiwa na jamii husika ili kujiletea maendeleo endelevu. Ni kwenye kujibu swali hili, nchi huzingatia nguzo kuu muhimu tatu, ambazo ni watu,uzalishaji na masoko.

Watu kama sababu kuu ya kufikiri kuhusu uchumi, uzalishaji kama nguzo kuu ya tija na uendelevu, masoko kama njia muhimu ya sababu za kuzalisha, ushindani na ubunifu. Kwa msingi huu, maswali muhimu kwenye kuendesha uchumi wa nchi ni matano kwa mfuatano maalumu.

  1. Zipi ni rasilimali zangu zinazonipa nafasi zaidi ya wengine?
  2. Nazivuna kwa maslahi ya nani?
  3. Lini nizivune?
  4. Kwa njia ipi nizivune?
  5. Ni upi mustakabali wa fursa za kiuchumi za muda mrefu kwenye dunia iliyofungamanishwa?

Ni muhimu kuwa na mfuatano huu kwa sababu dunia imekuwa kwenye jitihada za kuzifanya rasilimali ziwe za dunia kuliko kuwa za mataifa husika. Muhimu zaidi, miaka 40 iliyopita, dunia ilielezwa kuwa tukitandawazisha uchumi, kila nchi itaiona paradiso ya maendeleo ya kiuchumi.

Hata hivyo, zipo tafiti za kutosha kuonyesha kuwa wakati sehemu ya Kaskazini mwa dunia kumekuwa paradiso, sehemu ya Kusini imeendelea kujikongoja kutoka kwenye “jehanamu” ya kiuchumi pamoja na kuwa na rasilimali nyingi za asili.

Mheshimiwa rais, kwa sababu ya maswali matano hayo ya kiuchumi, nchi hubuni mikakati ya kiuchumi  ili kujibu maswali hayo barabara. Ili kutekeleza mikakati hiyo, moja ya njia zinazotumika ni mikakati ya kibiashara.

Mikakati hii ya kibiashara hutakiwa kujikita kwenye malengo makuu ya kiuchumi, hasa katika kuzalisha, kupanua fursa za kifedha kwenye shughuli za kiuzalishaji, kukidhi mahitaji ya faida na kuimarisha mitaji hiyo kwa kuvutia fursa kutoka pahala popote zinakopatikana.

Kwa hiyo, mikakati ya kibiashara huwepo kukidhi haja ya malengo mapana ya kiuchumi Ndiyo maana hata malengo mapana ya uchumi wa dunia yanatekelezwa kwa mikakati ya kibiashara. Wakati mwaka 1970 mchango wa biashara kwenye uchumi wa dunia ulikuwa asilimia ishirini na nne(24%), mchango huo umeongezeka kufikia karibu asilimia sitini(60%) mwaka 2022.

Tafiti za Oxford Economics (2016) zinaonesha kuwa; asilimia sabini na nane(78%) ya biashara ya bidhaa na huduma imefungamanishwa na rasilimali za asili za nchi za kusini kwa njia ya moja kwa moja au kwa njia ya mahusiano kati ya biashara moja na nyingine, nchi moja na nyingine au kampuni moja na nyingine. 

Nchi za Afrika kusini mwa Sahara zinachangia asilimia arobaini na saba (47%) ya hiyo asilimia sitini kwa njia ya moja kwa moja au njia ya mahusiano ya kibiashara. Pamoja na kujifungamanisha na biashara hii ya dunia kiasi hicho, bado mchango wa Afrika, kusini mwa Sahara kwenye biashara ya dunia, ni chini ya asilimia nne nukta tano (4.5) kwa mujibu wa tafiti za hivi karibuni za Chuo Kikuu cha Sussex cha nchini Uingereza.

Mheshimiwa rais, nchini Tanzania tumekuwa na changamoto kubwa kwenye eneo hili. Kwa miaka zaidi ya 30 sasa, tumekuwa tukitanguliza mikakati ya biashara na kufikiria malengo mapana ya kiuchumi baadae.

Tumekuwa tukitumia zana za kibiashara kuamua malengo makuu ya uchumi wetu na kwa kweli tumetumia zana hizo, kwa mfano sheria, wakati mwingine kujitia kwenye kitanzi. Kuna maeneo makuu matano ya kudurusu suala hili kwa kutumia mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi wa Tanzania na Dubai na kuoanisha na uamuzi wetu juu ya mambo kadhaa huko nyuma, tuliofanya kwa mtindo huo.

Itaendelea kesho na sehemu ya pili

Like
3