Mahabusu wasimulia mateso ya kunguni, uchafu wa haja ndogo na kunyimwa dawa wakiwa vituo vya polisi Dar

MAHABUSI za vituo vya Jeshi la Polisi nchini Tanzania zimegeuzwa “jehanamu” za polisi kutesea mahabusu kinyume cha sheria, imefahamika.

Baadhi ya mahabusu walioshikiliwa katika mahabusi hizo wameeleza kuwa vituo hivyo ni vichafu mno, vina kunguni, havina sehemu za kujisaidia kwa staha, hakuna maji, na hata baadhi ya mahabusu wa kike hulazimika kujisaidia ndani ya chupa – jambo ambalo ni gumu kutokana na maumbile yao – na hivyo kusababisha haja ndogo kutapakaa vyumbani humo.

Mbali na ukosefu wa miundombinu, vyumba vyenyewe ni vidogo lakini polisi hujaza mahabusu kiasi cha kuwafanya washindwe kulala, huku wengi wao wakinyimwa dhamana na hata kukalishwa vituoni kwa zaidi ya miezi miwili bila kuonwa na ndugu zao wala mawakili.

Baadhi ya mahabusu wanasema waliingia mahabusi wakiwa wazima lakini wamepata magonjwa ya kuambukizwa kutokana na uchafu huo na msongamano huo, huku polisi wakiwakatalia matibabu. 

Haya yameibuliwa na mahabusu waliokuwa wamefungiwa katika vituo vya Chang’ombe, Buguruni, Kilwa Road, Central Police, na Mburahati.  

Wanaoeleza mateso hayo ndani ya mahabusi hizo ni wanawake na wanaume waliokamatwa na Polisi wiki iliyopita kwa tuhuma za kufanya maandamano na kukusanyika bila kuwa na vibali vya jeshi hilo, wengi wao wakiwa wafuasi, wanachama na viongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini, Chadema. 

Katika mkutano kwa njia ya mtandao ujulikanao kama MariaSpaces uliojumuisha watu zaidi ya 3,500 leo usiku – Agosti 10 – baadhi ya washiriki waliokumbwa na mateso hayo wakiwa mikononi mwa polisi, wameeleza namna walivyoteswa na askari wa jeshi hilo. 

Akizungumza kwa niaba ya mahabusu zaidi ya 40 waliokamatwa na wengine kutekwa na polisi tangu Ijumaa iliyopita – Agosti 6, 2021 – Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Catherine Ruge, ameeleza namna polisi inavyokinzana na dhima ya kuanzishwa kwake na kugeuka kuwa kundi la kutesa watuhumiwa bila hata kuwafikisha mahakamani.

Catherine alikamatwa akiwa na wanawake wengine siku hiyo, wakiwa wanaelekea mahakamani Kisutu, Dar es Salaam, kusikiliza kesi inayomkabili mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe anayetuhimiwa ugaidi. Amesema kuwa wakiwa katika Kituo Kikuu cha polisi cha Dar es Salaam, waliwekwa kwenye chumba kidogo ambamo walijazwa na “kushindiliwa kama magunia ya viazi.”

“Tuliingizwa ndani ya chumba kimoja kidogo ambacho kinatakiwa kukaliwa na watu sita, lakini  tukajazwa watu 19. Humo tulishindwa kupumua vizuri, hatukulala, na  hali zetu zilikuwa mbaya, hakika ni mateso makubwa ndani ya mahabusu,” amesema Catherine.

Kibaya zaidi, mbali na kushindwa kulala, huku wakikosa mahali pa kujisaidia kwa staha, baadhi ya wanawake ambao waliingia katika siku zao walinyimwa taulo za kike hadi siku ya pili; na kesho yake askari mmoja wa kike alipoingia katika chumba hicho aliwatolea maneno ya kejeli, akihoji: “pedi zimeingiaje humu?”

Mbali na kejeli hizo, askari mwingine aliwatisha kuwa wasingepata dhamana kamwe kwa maana walipaswa “kuozea humo.” 

Catharine amesema kuwa askari mmoja aliwambia: “Ninyi hamwezi kutoka humu, mtaozea humu, nyie kesi yenu siyo ya kawaida, bali ya kimkakati.” 

Waliokuwa na matatizo ya kiafya walikataliwa kutumia dawa. Hata baada ya siku tatu wakiwa ndani bila kuruhusiwa kuonana na ndugu zao wala mawakili, hatimaye waliporuhusiwa na kuletewa chakula na nguo za kubadilisha, walilazimishwa wazivue, wakavaa nguo zilizokuwa zimechafuka na kunuka mikojo ambazo walikuwa wameingia nazo awali. Walibaki na nguo hizo chafu hadi jana usiku walipotolewa na kurudi nyumbani kwao.

Catherine amesema kuwa ndugu zake wamemweleza kuwa walipeleka chakula kwa ajili yake polisi wakawazuia kumwona, wakapokea chakula hicho kwa maelezo kuwa wangempatia. Anasema ingawa walimpelekea chakula zaidi ya mara nane, hakuwahi kupewa chakula hicho; na haijulikani nani alikila.

Katika baadhi ya vituo, kuna watu wameshikiliwa kwa zaidi ya siku 70 wakituhumiwa kwa makosa madogo madogo kama ya ugomvi au kukutwa kwenye baa usiku wa manane, na bado hawapewi dhamana wala kufikishwa mahakamani – jambo ambalo ni kinyume cha sheria. 

Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) uliopitisha, kuridhia na kusaini matamko kadhaa ya haki za binadamu.

Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Fatma Karume, ambaye alikuwa mmoja wa waliohudhuria mkutano huo ulioitishwa na mwanaharakati Maria Sarungi, amesema ni kinyume cha sheria kukataza au kumpangia binadamu muda wa kujisaidia.

Fatma amesema pamoja na sheria kukataza kabisa polisi kushikilia watuhumiwa kwa zaidi ya saa 48, hawaruhusiwi kwa namna yoyote kuzuia mtuhumiwa kujisaidia.

Amesema mahabusu za Polisi ni eneo la kutunza watuhumiwa kwa muda, na kamwe zisigeuzwe kuwa gereza la kufunga watu ambao hawajahukumiwa na mamlaka ya mahakama.

Fatma amewashangaa wakuu wa vituo hivyo na askari wao wanaodiriki kufanya kazi katika vituo hivyo huku vikiwa vichafu vinatoa harufu mbaya ya kinyesi, huku wako wakiwa wamevalia sare nadhifu na kulia chakula maeneo hayo.

Kwa mujibu wa Fatma, suala la uchafu uliopitiliza wa mahabusi liliwahi kufikishwa kwa Inspekta Jenerali wa Polisi lakini alidai kuwa wanashindwa kuvisafisha kwa sababu ya bajeti ndogo. 

Hata hivyo, Fatma alisema kuwa kufanya usafi au kuua kunguni hakuhitaji bajeti kubwa kwani hata zikitengwa shilingi 2,000 kila siku zinaweza kutosha.

Licha ya utetezi wa polisi kuhusu bajeti ndogo, kumbukumbu za kibunge zinaonyesha kuwa Jeshi la Polisi na Ikulu ni maeneo ambayo kwa miaka sita iliyopita mfululizo yalikuwa yanachotewa pesa nyingi kinyume cha bajeti iliyopitishwa na Bunge huku wizara nyeti kama za maji na kilimo zikinyimwa mafungu yake.

Patrick Assenga, Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Segerea, Dar es Salaam, ambaye alikamatwa Ijumaa iliyopita na kulazwa mahabusi ya Buguruni na baadaye Mburahati, ameeleza mazingira ya chumba cha watuhumiwa kuwa ni mabaya na hayafai kwa binadamu kukaa hata dakika moja.

“Mahabusi ya Buguruni ni chafu sana, imejaa kunguni na inanuka kila aina ya uchafu; huku ikiwa imerundikwa watu wengi na hakuna maji ya kutumia; iwe baada ya kujisaidia au kuoga,” amesema.

Ameongeza kuwa polisi Buguruni wamegeuza mahabusu kuwa mtaji wa kuchuma pesa, kwani wanakamata watu na kuwaingiza humo kwa muda huku wakiwalazimisha kutoa rushwa ili waachiwe.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, John Heche, ambaye amekuwa akikamatwa mara kwa mara na kushikiliwa polisi kwa tuhuma mbalimbali zinazohusiana na siasa, akiwa mshiriki wa mkutano huo amesema mahabusi za Tanzania ni chafu na hazistahili kukaliwa na binadamu.

“Mahabusi za polisi ni mbaya kuliko inavyoweza kufikiriwa. Angalia kunguni anakaa kwenye sakafu – tena kuna baridi – kwa kawaida, kunguni hupenda kujificha kwenye vitu kama nguo au godoro; sasa jiulize mahali hapo ni pachafu kwa namna gani, pana vumbi kiasi gani hadi kunguni akae pale!” alihoji Heche. 

Mwanasheria Fatma alisema kila mtuhumiwa ana haki ya kuheshimiwa utu wake na kamwe hakuna ruhusa kwa askari kumdhihaki wala kumfanya dhalili kwa njia yoyote, hivyo anapaswa kuishi na kulala sehemu salama na yenye hadhi na si “jalalani.”

Mahabusu hao ambao walihifadhiwa katika vituo mbalimbali vya polisi Mkoa wa Dar es Salaam kwa zaidi ya siku nne, pia walikataliwa kuonana na ndugu zao waliofika vituoni hapo kuwadhamini au kuwaletea chakula. 

Jioni leo, wanachama na  viongozi wengi wa Chadema waliokamatwa ama wameachiwa huru au kuwekewa dhamana, isipokuwa wachache ambao mwanasheria Dickson Matata akizungumzia hatma yao, alisema huenda kesho watuhumiwa wote watakuwa huru.

Leo asubuhi, Msemaji wa Polisi, David Misime, alipohojwa na SAUTI KUBWA kuhusu tuhuma hizi alikanusha na kueleza kwamba jeshi hilo limekuwa likifuata sheria na taratibu zote katika kutekeleza majukumu yake na haliwezi kunyanyasa wala kuonea mahabusi.

Alisema jeshi hilo limekuwa mstari wa mbele kuhakikisha haki za mahabusu zinalindwa na kwamba kama wapo askari wanaokiuka sheria, huchukuliwa hatua mara moja.

“Hizi tuhuma nimezisikia, lakini hazina ukweli wowote, huenda wameamua tu kusema ili kuchafua sifa nzuri za jeshi letu, lakini hawawezi kunyanyaswa wala kunyimwa haki zao za msingi, endapo wako kwenye mikono yetu,” alisema Misime. 

Kutokana na madhila hayo ya mahabusu, wamedhamiria kushitaki jeshi la polisi, hasa wakuu wa vituo hivyo ambako wametesewa, ili kuweka msingi wa kukomesha unyanyasaji na ukatili huo. 

Like
3