Kenya yaamuru watumishi wa umma wachajwe kwa lazima

SERIKALI ya Kenya imeamuru watumishi wote wa umma nchini humo kuchanjwa kwa lazima dhidi ya COVID-19.

Taarifa iliyosainiwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma, Joseph Kinyua, iliyotolewa leo kwa umma, inaeleza kwamba wafanyakazi wote wa serikali sasa watalazimika kuwa wamechanjwa ifikapo Agosti 23.

Wale ambao hawatachanjwa hadi tarehe iliyopangwa wataainishwa kuwa ni watovu wa nidhamu na watachukuliwa hatua za kisheria, ikiwamo kufukuzwa kazi.

Kinyua amewataka makatibu wakuu na maafisa watendaji wa taasisi na mashirika yote ya umma kuhakikisha kuwa uamuzi huo unatekelezwa kikamilifu.

Hatua hii imechukuliwa na serikali ikiwa ni njia ya kuendelea kudhibiti maambukizi mapya ya janga la Corona linaloendelea kusumbua dunia.

Like