Magufuli na “maparoko wake” wana kesi ya kujibu

NIMEMSIKILIZA Rais John Magufuli akihutubia waamini leo katika Kanisa la Mt. Petro, Dar es Salaam, na nimebaini mambo machache ambayo ni muhimu kuyajadili kwa ufupi. Nitadokeza mambo 10 tu.

Kwanza, Magufuli ameonyesha kuwa anakerwa na matamko ya maaskofu na msimamo wa Kanisa juu ya Corona. Sababu zinaeleweka. Hakutaka waseme Corona ipo kwa kuwa yeye alishasema haipo. Na sasa tutarajie kejeli, matusi ya rojorojo, vijembe na hujuma nyingi dhidi ya maaskofu. Atatumia vyombo vyake kuwabana na kuwadhalilisha.

Pili, ingawa ametamka kuwa yeye hakatazi uvaaji wa barakoa, pale pale kanisani ameonyesha kuchukizwa na uvaaji wa barakoa. Ndiyo maana amemsifu “paroko” ambaye hakuvaa, na akajaribu kumchonganisha na askofu aliyeagiza watu wavae barakoa. Ndiyo maana alimsuta sista aliyevaa barakoa na akawasifia masista ambao hawajazivaa.

Ndiyo maana alishukuru wanakwaya kwa kutovaa barakoa; akamshutumu Jaji Mstaafu Thomas Mihayo (na mkewe) kwa kuvaa barakoa; na akasisitiza kuwa wasaidizi wake hawavai barakoa. Si kwamba hawataki, bali hawawezi kuvizaa mbele yake. Yeye hataki! Sijui anapata faida gani.

Tatu, ameendelea kutumia “Jina la Mungu” kushambulia viongozi wa dini – akitaka kuonyesha kuwa kwa vile wao wanasema kuna Corona na wamehamasisha waamini kujikinga, basi viongozi hao wana imani haba! Amekuwa anayasema haya mara kwa mara awapo kanisani au hata kwenye majukwaa ya kisiasa, labda kama njia ya kuwaaminisha wananchi kuwa yeye ni mcha Mungu kuliko viongozi wao wa kiroho.

Hata leo, ametumia njia hiyo kushutumu masista na askofu – ili ionekane kwamba wanaovaa barakoa hawamtegemei Mungu. Ametumia kauli hiyo dhidi ya padri mwongoza ibada, akitaka kuonyesha kwamba kwa vile askofu aliagiza matumizi ya barakoa, na padri hakuitumia, basi amefanya vizuri kumkaidi askofu na “kumfuata Mungu” – kana kwamba Mungu anazuia matumizi ya barakoa!

Nne, rais amejaribu kukatisha tamaa wanaovaa barakoa, akawambia kuwa hizi zitokazo nje ya nchi si salama. Anawataka ama wanunue zinazotengenezwa hapa nchini au watengeneze wao wenyewe kienyeji.

Ajabu! Serikali anayoongoza ndiyo inayodhibiti ubora wa bidhaa zote zinazoingia nchini. Anataka kusema hizo mbovu zimepita wapi kuingia nchini katika mazingira ya sasa ya kujihadhari na Corona? Na kwanini mbovu ziletwe Tanzania? Na hizi anazotaka wajitengenezee, je, hazitarajiwi kuwa na viwango maalumu vinavyohitajika? Kila mmoja ajiokotee kitambaa avae ilimradi tu zimefunika midomo na pua?

Yawezekana yeye, kwa changamoto zake binafsi, akizivaa zinamdhuru kiafya. Si awaache wasio na changamoto kama zake watumie?

Tano, wakati rais anasema hayo yote, yeye anayerubuni watu kwa jina la Mungu ameingia kanisani akiwa na vikosi vya kijeshi vinavyomlinda. Mara kadhaa, walinzi wake wamekuwa wanaingilia liturjia na kusababisha vurugu isiyo ya lazima kanisani. Waamini wanasemea chini chini tu, lakini wanakerwa.

Sasa, kama yeye anamtumaini Mungu ambaye anaona wengine hawamtumaini ipasavyo, kwanini analindwa na majeshi kila aendapo, tena wakati mwingine wakiwa na silaha za kijeshi na helikopta?

Mungu huyu anayetuelekeza ameshindwa kumlinda yeye? Kwanini rais anaona fahari kuongopea Watanzania? Kwanini hapendi wajilinde? Anapata faida au furaha gani wao wakipoteza uhai – tena kizembe? Kwanini anaumia wao wanapojilinda?

Sita, rais ameendelea kudanganya wananchi kuwa mwaka jana Corona iliondoka Tanzania. Hataki kukiri kuwa kati ya Machi na Juni 2020, Tanzania ilikuwa na maambukizi machache mno yaliyokuwa yameingia, na ilikuwa imedhibiti kuenea kwa maambukizi hayo kwa sababu wananchi waliambiwa wachukue hatua, na wageni hawakuingia nchini kiholela.

Baada ya rais kutangaza kuwa hakuna Corona, watu waliacha kuzingatia masharti, waliokuwa na maambukizo wakayaeneza kirahisi, kupitia mijumuiko mingi tu – pamoja na mikutano ya kampeni za uchaguzi – sherehe, starehe, sikukuu, sokoni, kwenye ibada, na kadhalika.

Hapo hapo, wageni (watalii) wameendelea kuingia Tanzania, na baadhi yao wameeneza virusi. Hiki tunachoona sasa ni matokeo ya uamuzi wake wa mwaka jana kusema “hakuna Corona.” Mambukizi yamekuwa yanaendelea, na kirusi kinajibadilisha, na aina nyingine zimeingizwa kwa sababu ya uzembe wetu na ubabe wa rais.

Saba, wakati Magufuli anataja nchi nyingine ambazo raia wake wamekufa kwa wingi, anatumia takwimu ambazo nchi hizo zimeweka wazi kama inavyotakiwa. Anataka kutuhadaa kuwa kwa kuwa sisi hatutangazi takwimu, basi watu wetu hawaugui wala hawafi.

Kimsingi, watu waliokufa ni wengi lakini kwa kuwa hakuna takwimu, wenye kujua misiba hiyo ni hao wanaoguza na wanaofiwa. Familia zimefiwa mno. Sasa imefika mahali wakafa watu wenye vyeo vikubwa kwenye jamii ndipo wakubwa wakaanza kushtuka. Lakini kimsingi tumepoteza wananchi wengi sana. Kuficha takwimu hakuwafufui wala hakumfanyi yeye kuwa kiongozi mungwana. Sana sana rais anaonekana ni mtu asiyejali uhai wa wenzake.

Hata wagekufa wachache, sioni kwanini Magufuli haoni kuwa hawakustahili kujengewa mazingira ya kufa. Tayari amepoteza hata washauri na wasaidizi wake waandamizi – watu wake wa karibu. Yeye bado anasema “tupo salama.” Nani afe ndipo Magufuli ashtuke?

Nane, sasa ameanza kuona ukweli kuwa tunajua kwamba Corona ipo – jambo ambalo amekuwa anaepuka kulikiri. Amekuwa anatumia mimbari za makanisani kutangazia wananchi kuwa hakuna Corona. Huku ni kutumia kanisa kueneza Corona! Wanaomruhusu kufanya hivyo walipaswa wajue kwamba nao wameshiriki kuua watu.

Baada ya hali kuwa mbaya sana na maaskofu wakamruka, wakaamua kutangaza wenyewe kwa waamini wao, sasa serikali nayo inaelekea kukiri ukweli huo huo, lakini bado inasema kwa kuzunguzunguka.

Hata hivyo, hii ni hatua. Tumemtoa kwenye hali ya kukataa katakata hadi kusema “watu wachukue tahadhari.” Si jambo jepesi, hasa kwa kiongozi anayeshupaza shingo. Tuendelee kumkumbusha na kumsukuma. Hata kama hataki, ipo siku atatuelewa.

Tisa, waamini waliokuwa wanamsikiliza leo kanisani wamemnyima makofi na vigelegele kama alivyozoea. Alikuwa anajitahidi kuzungumza kwa msisitizo na kumtaja Mungu kila baada ya maneno machache, halafu anasita kidogo kungoja magofi. Wapi! Wamegoma kuyapiga.

Maana yake ni nini? Waamini nao wamempa ujumbe moja kwa moja, pale pale, kwamba wameshajua sarakasi zake za kutumia mimbari za makanisa na jina la Mungu kufanya siasa na kujitukuza. Atambue tu kuwa hawafurahi anapowakejeli maaskofu wao na kujifanya kiranja wao.

Kumi, bado Magufuli hajatambua kuwa yeye ni muumini kama wengine. Anadhani urais wake una nguvu mbele ya madhabahu.

Anaonyesha dharau ya wazi kwa viongozi wa Kanisa, anathubutu kuwagawa kwa kuwapatia sifa na zawadi baadhi yao – hasa michango na misaada ya fedha. Na kila anapokwenda kusali anawapanga mapema viongozi wa ibada wampe nafasi ya “kusalimia” waamini baada ya misa, na yeye anaitumia kueneza propaganda zake.

Kwa viwango vyovyote, Magufuli si Mkatoliki mwanana kama alivyokuwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Wala hamkaribii Rais wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa (Mungu ampe pumziko jema).

Lakini hatukuwahi kuona marais hawa wakijitangaza na kuhutubia wananchi kila walipokwenda kanisani kusali. Walitambua nafasi yao ya uumini, si urais, mbele ya madhabahu.

Inashangaza sasa kuwa huyu ambaye amekuwa anazurura kwenye makanisa kadhaa ya kilokole kwa miaka kadhaa, aliyerejeshewa ukatoliki kwa sababu za kisiasa, kwa jitihada binafsi za Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu 2015, ndiye anataka kuwa kiranja wa maaskofu wetu.

Ndiye huyu ambaye maparoko kadhaa wanamruhusu awaswage kama punda? Ndiyo, yeye ana matatizo yake kadhaa, tunayatambua. Lakini nadhani na hawa wanaomruhusu atumie mimbari zao kueneza uwongo unaohatarisha afya za watu, wana kesi ya kujibu. Siku moja watajibu.

Like
20