Magufuli azidi kudhulumu Kanisa. Serikali yamvua uraia katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki

UTAWALA wa Rais John Magufuli umeendelea kujizolea kashfa ya kutumia “silaha ya uraia” katika kukomoa raia, kuzima sauti za wananchi na kulipiza visasi.

Zamu hii serikali imemnyang’anya uraia Padri Raymond Saba (pichani), wa Kanisa Katoliki, ambaye hadi wiki chache zilizopita alikuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC). Padri Saba ni mzaliwa wa Kigoma.

SAUTI KUBWA ina taarifa za uhakika kuwa idara ya uhamiaji ilimchukulia hatua hiyo akiwa katibu mkuu wa TEC. Hiyo ndiyo sababu iliyozingatiwa na TEC kumwondoa katika wadhifa huo na kuteua Dk. Charles Kitima.

Maaskofu walipobadili uongozi wa juu – rais na makamu wake ambao walikuwa wanamaliza muda wao – wakamwondoa na katibu mkuu. Kwa sababu kanisa halikupiga kelele, mbele ya umma suala hili lilionekana kama mabadiliko ya kawaida tu ya uongozi, lakini kulikuwa na sababu zilizotokana na msukosuko wa serikali na vyombo vyake.

Serikali, kupitia idara ya uhamiaji, imekamata pasipoti ya Padri Saba ikimtuhumu kuwa si Mtanzania, na inamtaka athibitishe uraia wake. Miongoni mwa mambo ambayo wamekuwa wanataka afanye ni kuwaonyesha makaburi ya bibi na babu zake – jambo ambalo wamekuwa wanalifanya kwa kila wanayemtuhumu kuwa si raia.

Sababu ya serikali kumtia msukosuko padre huyo ni waraka wa kichungaji wa TEC ambao ulitolewa katika kipindi cha kwaresima mwaka huu, yeye akiwa katibu mkuu. Waraka huo, miongoni mwa mambo mengine, ulizungumzia kutetereka kwa amani ya nchi na kutaka viongozi wa nchi wajitafakari.

Serikali ilichukizwa na waraka huo, na baadhi ya viongozi wa kisiasa walijiapiza kulipiza kisasi kwa kukomoa au kuumbua baadhi ya viongozi wa dini kwa namna mbalimbali. Wapo waliozushiwa kutelekeza watoto. Wapo wanaotafutiwa kesi. Wapo wanaozuiwa kusafiri nje ya nchi. Wapo wanaopigwa kwa uraia – hasa watokao katika maeneo ya mipakani. Wengi wao wanaumia kimya kimya.

Msukosuko dhidi ya Padri Saba ulifikia kilele katika kipindi ambacho Mwigulu Nchemba, aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani, alisimamisha kazi Merlin Komba, msajili wa vyama katika wizara yake ambaye alikuwa ameagizwa na Ikulu kuandika barua za maonyo kwa Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Barua ya serikali kwa TEC haikuvuja, lakini serikali ilikerwa na mawasiliano ya kanisa, na msimamo wa Padri Saba katika majibu ambayo kanisa lilitoa kwa maandishi, huku Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, aliyekuwa rais wa TEC akisumbuliwa na kuitwa ajieleze serikalini.

Baada ya maaskofu kubaini msukosuko na usumbufu uliokuwa unamkabili Padri Saba walimwondoa kwenye nafasi hiyo ili suala hilo lisiwe sababu ya nyongeza ya serikali kuendelea kuandama kanisa. Baadhi ya wapambe wa Rais Magufuli walichekelea alipoondolewa wakisema, “tumemkomoa.”

Serikali inaendelea kushikilia pasipoti yake kama inavyoshikilia pasipoti za wengine inaowachapa “kiboko cha uraia” kwa sababu za kisiasa.

Katika muda mfupi wa madaraka ya Rais Magufuli, suala la uraia limegeuzwa silaha ya kisiasa na linaendelea kuumiza wananchi kadhaa, hasa wanaokosoa serikali au wasiokubaliana na mambo kadhaa inayotenda.

Orodha ni ndefu lakini wengine wanaotajwa na vyombo vya habari, mbali na Padre Saba, ni hawa wafuatao:

Askofu Zakaria Kakobe wa Full Gospel Bible Fellowship. Alitoa mahubiri makali katika Krismasi ya 2017, akaonya serikali juu ya dhuluma, hasa mauaji ya raia. Alimtaka rais atubu. Askofu Kakobe alitiwa misukosuko na polisi na Mamlaka ya Mapato Tanzania. Walipokosa jinsi ya kumtia hatiani, idara ya uhamiaji iliibua suala la uraia wake. Sasa anachunguzwa uraia.

Aidan Eyakuze mkurugenzi mtendaji wa Twaweza, shirika lisilo la kiserikali ambalo limetangaza matokeo ya utafiti unaoonyesha kuwa umaarufu wa rais miongoni mwa wananchi umeshuka kutoka asilimia 96 (2016) hadi 54 (2018).

Wakati Twaweza walipotangaza kuwa rais alikuwa anapendwa na waanchi kwa asilimia 96 mwaka 2016, serikali haikutilia shaka uraia wa mkurugenzi wake. Ilipotangaza kushuka kwa umaarufu wake, taasisi yake ilisakamwa.

Baadhi ya vijigazeti vinavyofadhiliwa na serikali kwa ajili ya propaganda za kisiasa za CCM, vimekwenda mbali zaidi, vikamtaja kuwa ni mwanachama wa chama cha siasa (Chadema), jambo ambalo taasisi yake imekanusha. Sasa anachunguzwa uraia.

Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo Katoliki la Rulenge. Mwaka 2017 alitoa kauli kuhusu umuhimu wa kuwa na katiba mpya ili hatua nzuri zinazochukuliwa na serikali zizingatie misingi ya katiba badala ya kutegemea uamuzi wa mtu. Rais Magufuli ameshasema kuwa katiba mpya si ajenda yake.

Haikuchukua muda mrefu, idara ya uhamiaji ikaanza kuhoji uraia wa askofu huyo. Bado pasipoti yake imeshikiliwa. Anachunguzwa uraia.

Abdul Nondo, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Alitoa taarifa kupitia simu yake kuhusu watu waliomteka usiku, wakamsafirisha usiku kucha kutoka Dar es Salaam hadi Iringa.

Kwa kuwa “watu wasiojulikana” ambao wamekuwa wanateka na kupoteza watu wanahusishwa na vyombo vya dola, yalitoka maagizo mengi ya kisiasa yakitaka kijana huyo ashughulikiwe. Serikali imemfumgulia kesi mahakamani. Amesimamishwa masomo chuoni. Anachunguzwa uraia.

Padri Saba, Askofu Kakobe, Eyakuze, na Nondo ni wazaliwa wa Kigoma. Askofu Niwemugizi ni mzaliwa wa Kagera. Orodha ya wanaoshughulikiwa “kimfumo” ni ndefu.

Chanzo maalumu cha SAUTI KUBWA kinaeleza kuwa miongoni mwa waathirika wa mkakati huu ni viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya upinzani, na wafanyabiashara wasiopenda kuunga mkono Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Miezi kadhaa iliyopita, mke wa kiongozi mmoja wa dini hapa nchini alizuiwa na maafisa usalama na wa uhamiaji katika uwanja mmoja wa ndege akiwa safarini kuelekea Ulaya. Alikaguliwa kwa saa kadhaa akidaiwa kuwa yeye ni raia wa nchi moja ya ulaya. Kama hawa wengine, naye anazaliwa katika mkoa mmoja wa mpakani.

Idara ya uhamiaji katika viwanja vya ndege inathibitisha kuwa viongozi wengine wa dini wamekuwa wanatiwa msukosuko katika viwanja mbalimbali, wakiwekwa chini ya ulinzi na kuhojiwa uraia. Wapo ambao kutokana na misukosuko hiyo wameachwa na ndege. Wote waliohojiwa wanatoka mikoa ya mipakani.

Wimbi hili limechochea hisia mbaya kutoka kwa raia wanaoishi mikoa ya mpakani, wakidai kete ya uraia inatumika kuwanyima haki zao za msingi.

Habari za uhakika zinasema unyanyasaji huu umekuwa unaendeshwa chini ya usimamizi wa rais mwenyewe. Lakini baadhi ya viongozi hawa wanapomuuliza anakana kuhusika, huku kwa siri akihimiza idara ya uhamiaji “kukaza kamba” hata kuwanyang’anya pasipoti zao.

Like
26

Leave a Comment

Your email address will not be published.