Kutoka mahabusu Dar: Waraka wa Mbowe kwa Watanzania

WARAKA huu umeandikwa kutoka mahabusu. Aliyeuandika na Freeman Mbowe, mwenyekiti wa Chadema, ambaye dola imemkamata akiwa Mwanza kuandaa kongamano la katiba, ikamtungia mashitaka ya ugaidi na mauaji ili akose dhamana. Katika siku ya pili akiwa korokoroni, leo Mbowe ameandika waraka wa kuwatia matumaini Watanzania kwa maneno yafuatayo:

SALAMU ZANGU KWENU WATANZANIA!

Wakati fulani ukatili wa utawala wa Magufuli ulipofikia kilele kisichoweza kufikiriwa na binadamu yoyote dhidi ya siasa zetu hapa nchini usalama wetu uliteteleka; huku maisha na biashara zetu zikitetea na mitaji yetu kuporwa kwa nguvu na mamlaka za dola kwa maagizo mahususi.

Mwishowe nilifikia uamuzi wa kuangalia mahala pengine nje ya nchi ambapo ningeweza kufanya uwekezaji wangu kibiashara. Hata hivyo, bado sikuweza kuwa na utulivu wa moyo kila nilipowaza juu ya nchi yangu na hali yake ya kidemokrasia, masuala ya haki na maendeleo.

Kiuhalisia, niliiona nafasi na wajibu wangu uliokuwa dhahiri ambao kamwe sitaweza kuusaliti kwa nchi yangu – ni kuendesha mapambano ya kutetea haki, demokrasia na maendeleo.

Ningeweza kujaribu kulikimbia jukumu hili na kuungana na wengine katika kuyafaidi maisha mahala pengine duniani lakini kamwe nisingeweza hata kwa nukta moja kuiona furaha ya moyoni.

Ni kwa sababu hii leo nipo nyuma ya kuta nene za Mahabusu hapa Dar es Salaam nikihesabiwa uzalendo nilionao kwa nchi yangu kuwa ni ugaidi dhidi ya miungu ya kiafrika yenye tamaa ya madaraka, miungu ambayo ipo tayari kuilinda mamlaka yao kwa gharama ya uhai wa yeyote anayesimama kinyume chao.

Huenda nikakaa mahabusu muda mrefu kuliko hata wale mashehe wa uamsho kutoka kule Zanzibar, au hata ikibidi kukikabili kifo changu nikiwa ndani ya kuta hizi, lakini sizihesabu hatia hizi za uongo zinazonena kinyume na ukweli unaojulikana na watu wote (ikiwa ni pamoja na watesi wenyewe) kuwa kitu cha kunikatisha tamaa.

Nitaendelea kusimama kama shujaa nikiuishi wito wangu katika zamu yangu, nikijua kuwa hiki ni kitabu changu cha historia ya maisha yangu ambacho hakina budi kusomwa na watoto, wajukuu na vitukuu wangu ambao bila shaka watakuwa na neno la kusema juu yangu.

Popote mlipo napenda kuwajuza kuwa mashtaka haya hayajanikatisha tamaa kwa hali iwayo yoyote ile, nipo imara kama jana na juzi, naam najiona kuzidi kuwa kijana zaidi katika mapambano haya ya siasa za hapa nyumbani Afrika licha umri wangu kuanza kuchwea.

Natarajia mfano huu tunaouacha sisi wazee wenu utawafaidia sana ninyi vijana wetu. Ni historia njema kwenu kulala mahabusu kwa ajili ya mapambano ya haki kuliko kwenda huko kwa ujambazi na ufisadi dhidi ya nchi yenu.

Pindi mnapokamatwa na kutupwa mahabusu jihesabieni ni fahari kuu kwenu kwa kuwa mimi mmoja wa baba zenu nipo huku kwa furaha wala sihisi majonzi yoyote.

Kamwe siitazami hii hali ya kunitweza, kunidhalilisha na kunishtaki kwa kesi za uongo kama jambo nitakalolipa fursa moyoni mwangu kunikatisha tamaa, la hasha! Uso wangu nimeukaza mbele nikizitazama siku za furaha za wajukuu na vitukuu wangu katika Tanzania iliyo huru na mahala salama kwa kila mtanzania.

Napenda moyo wa namna hii uote katika vifua vya ninyi nyote, ishindeni hofu na kifo mbele ya hao wategemeao kuteka, kutesa na kuua, lakini katika hayo yote wayafanyayo kamwe hawawezi kuzibadili dhamiri zetu safi zisizo na mawaa tulizo nazo juu ya Tanzania yetu.

Wanaweza kudumu kwa kitambo katika madaraka hayo na kiburi cha uharibifu waufanyao lakini kwa hakika watajimaliza wenyewe kwa mbegu za uharibifu wazipandazo kwa mikono yao wenyewe.

Msije kamwe mkausahau Ukuu wa Mungu uliomwondoa “mwendazake” aliyetarajiwa kuonekana kanisani siku ya jumapili iliyokuwa inafuata, lakini alitoweka jumla asionekane hadharani hadi leo.

Hakuna kati yetu aliyetumia rungu wala manati kupambana na vifaru vyao lakini Mungu alitushindia nasi tukamtukuza. Vivyo hivyo, endeleeni kuwa na moyo mkuu katika mapambano haya.

Tunakata nchi iandike katiba mpya, huu ndio wimbo wetu kwa sasa. Ukiwa ndani ya magereza au uraiani, hebu iambie akili yako hivyo.

Kila mmojawetu anaweza kufanya jambo fulani katika mapambano haya, basi na afanye lile lililo katika uwezo wake mpaka pale tutakaposimama kama nchi moja yenye watu wanaoheshimiana.

NIWATAKIE USIKU MWEMA NA TAFAKURI NJEMA KATIKA WARAKA WANGU HUU KWENU USIKU WA LEO.

22/07/2021.

Like
1