KUBETI: TISHIO LA AFYA YA AKILI TANZANIA

“Wanaume ndio washiriki wakubwa wa michezo ya kamari. Inahusishwa na ukatili wa kudhuru mwili, ukatili wa kingono, hisia na ukatili wa kiuchumi, kutokana na madhara ya kiakili wanayoyapata washiriki wa michezo hiyo.”

MIAKA ya nyuma, michezo ya kubahatisha au kamari (ijulikanayo kama kubeti), ilidhaniwa kuwa ni michezo maridhawa isiyo na madhara. Ilichezewa ndani ya kumbi maalumu za burudani kama vile casino

Hata hivyo, kukua kwa teknolojia ya intaneti, upatikanaji wa simu za mkononi pamoja na kutambulika kisheria kwa kamari kama michezo halali inayochangia pato la nchi, kumechangia michezo hiyo kushamiri, hususan katika nchi zinazoendelea,Tanzania ikiwemo.

Fursa hiyo ya teknolojia imefungua milango kwa kampuni nyingi kutoka China kuvamia soko la michezo hiyo hapa nchini na kuisambaza hadi vichochoroni, sehemu za wazi, vituo vya mabasi hadi vijijini.

Mbali na kusambaa kwa michezo hiyo, wataalam wa tiba pamoja na tafiti za kisayansi zimebaini  kamari ina uraibu mkubwa kuliko dawa za kulevya kama vile cocaine, heroin na nyinginezo.

Uwekezaji mkubwa unaofanywa na kampuni kutoka China hapa Tanzania kunaweza kutajwa kuwa kunachangia tatizo la afya ya akili kwa wanaocheza michezo hiyo ya kubahatisha.

Mtaalamu wa Saikolojia Tiba, Dk. Saldeen Kimangale wa Somedics Polyclinic Heath Centre ya Upanga Dar es Salaam, amezungumza na SAUTI KUBWA na kueleza undani wa michezo ya kamarii. Anasema michezo hii ina uraibu mkali unaosababisha matatizo ya afya ya akili kwa wanaojihusisha nayo.

Dk Kimangale amesema Shirika la Afya Dunia (WHO) limeorodhesha mchezo wa kamari kuwa mojawapo ya chanzo cha magonjwa ya afya ya akili kwa binadamu.

Amesema kwa mujibu wa kitabu cha mwongozo wa utambuzi wa magonjwa ya akili ukurasa wa 358 chini ya kichwa cha habari ‘Gambling Disoder’,  kamari inaweza kusababisha ugonjwa wa kucheza kamari (uraibu).

Anasema kamari inaweza kusababisha uraibu kwa ile shauku ya kupata zaidi na kwa sababu hiyo anayejihusisha nayo anasikia raha ya kupata zaidi, na pale anapopoteza anasikia maumivu.

Dk Kimangale anasema kuwa mwenye uraibu wa kamari anapokuwa amepoteza hupenda kulipa kisasi kwa kuweka fedha zaidi na kwamba tabia hiyo ikidumu kwa muda mrefu, muhusika hupata huzuni, hasira, kukosa utulivu, kukosa umakini kwenye kazi, kukosa usingizi na hamu ya kula.

Mtaalamu wa Saikolojia, Dk Saldeen Kimangale wa Somedics Polyclinic Health Centre Upanga, Dar es Salaam.

“Wagonjwa wa aina hiyo tumekuwa tukiwatibu kwa tiba inayohusiana na mabadiliko ya tabia na hatua za mabadiliko ikiwa ni pamoja na kumuwezesha mgonjwa kujenga utayari wa kubadili tabia na wale wanaoweza kushiriki matibabu vizuri wanapona kabisa”,anasema Dk Kimangale na kuongeza

“Binafsi nimewahi kukutana na wagonjwa wa uraibu wa kamari, wapo waliofanikiwa kubadili tabia na kupona kabisa, lakini wapo walioshindwa kukamilisha matibabu” anasema Dk Kimangale

Kuhusu takwimu za uraibu wa kamari nchini, Dk Kimangale anasema ingawa Tanzania haijatoa takwimu rasmi za wenye changamoto ya afya ya akili itokanayo na uraibu wa kamari, uzoefu wa kimazingira unaonyesha tatizo ni kubwa kwa sababu wanaocheza ni wengi na vyombo vinavyoendesha michezo hii pia ni vingi na vimesambaa hadi kwenye vitongoji.

Changamoto ya afya ya akili pia imechomoza katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere kwa mwaka 2022/20203 aliyoitoa hivi karibuni.

CAG Kichere anasema kuna idadi kubwa ya watu wenye tatizo la afya ya akili na kutokana na kutokuwapo fungu la fedha pamoja na ukosefu wa wataalam wa ustawi wa jamii katika ngazi za vijiji na mitaa.

Ingawa ripoti hiyo ya CAG haikugusia chanzo cha changamoto hiyo ya afya ya akili, lakini imeweka wazi kuwa, ukosefu mkubwa wa huduma za kisaikolojia katika ngazi ya jamii kwa watu wenye mahitaji maalum haijajumuishwi katika mipango na sera ya afya za Serikali.

“Vituo vingi havipati huduma za utengamo kwa ajili ya kusaidia wagonjwa kupona, ambapo kati ya mikoa 28, ni mikoa mitano pekee ndiyo ina vituo vya utengamo vya huduma za afya ya akili.”amesema CAG Kichere.

Mhadhiri Msaidizi Kitengo cha Saikolojia cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Magolanga Shagembe, anaulinganisha uraibu wa kamari au ‘kubeti’ kama ulivyo wa pombe, sigara na dawa za kulevya na au ulevi mwingine wowote. 

Anasema mtu aliyefika kwenye ulevi huo hawezi kukaa bila kubeti, na asipobeti anajisikia vibaya kwenye akili, mwili na hisia zake; hivyo anabeti ili kuondoa maumivu anayokuwa nayo.

Anashauri watu waliofikia kwenye hatua hiyo ya uraibu wasihukumiwe, wasaidiwe kwa kuwapatia msaada wa tiba ya afya ya akili, ili warudi kwenye majukumu yao ya kila siku.

Katika ripoti ya utafiti ya Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Auckland, New Zealand iliyopewa jina la The epidemiology and Impact of gambling – harm ya Juni 2017, yaani magonjwa ya mlipuko na madhara yatokanayo na kamari, imesema kuna ongezeko kubwa la michezo ya kamari inayofanyika kibiashara na inatarajiwa kuongezeka zaidi bila kujali madhara yanayoweza kuwakabili wanaoshiriki katika michezo hiyo.

Ripoti hiyo iliyolenga kuangalia madhara yatokanayo na kamari iliwasilishwa kwenye mkutano maalumu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Juni 2017 uliangazia vileo, dawa za kulevya na tabia hatarishi.

Katika ripoti hiyo, watu waliokuwa wakikabiliwa na matatizo ya afya ya akili duniani kutokana na ushiriki wa michezo hiyo wameongezeka mara tatu zaidi kila mwaka. Hata hivyo ripoti hiyo haijasema dunia nzima ina wagonjwa wangapi wanaotokana na michezo ya kubeti.

Ripoti hiyo iliyotayarishwa na Profesa Abbott wa chuo hicho, ilieleza kuwa mwaka mmoja kabla, kesi za msongo wa mawazo na uraibu utokanao na ushiriki wa michezo ya kamari ziliripotiwa kuongezeka kutoka asilimia moja hadi asilimia sita.

Utafiti mwingine ulifanywa Juni 2021 na Aprili 2022 na kuchapishwa kwenye Jarida la Kimataifa la Afya ya Jamii (IJPH), Mei 19, 2023 na kupewa jina la Uchambuzi wa vijana wacheza kamari na unyanyasaji wa wenza jijini Mwanza.

Utafiti huo ulishirikisha wataalamu kutoka taasisi sita za Kimataifa kutoka Ujerumani na Tanzania kupitia Mwanza Intervation Trials Unit pamoja na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Kituo cha Mwanza.

Utafiti huo umeainisha namna tabia ya uchezaji  kamari na uraibu utokanao na kamari unavyochochea unyanyasaji na kuathiri familia, ambapo imebainika kuwa waathirika zaidi ni watu walio katika umri wa miaka 22- 42 ambao ni vijana.

Wataalam hao walieleza kuwa uwiano wa unyanyasaji wa wenza unaotokana na ushiriki kweye michezo ya kamari unaonesha upo katika kiwango cha juu nchini Tanzania ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Sehemu ya ripoti hiyo inasomeka hivi: “Wanaume ndio washiriki wakubwa wa michezo ya kamari huku ikihusishwa na ukatili wa kudhuru mwili, ukatili wa kingono, hisia na ukatili wa kiuchumi kutokana na madhara ya kiakili wanayoyapata washiriki wa michezo hiyo.”

Like
1