Kidata yupo wapi? Amejificha, amefichwa, au amepotea?

Kidata - FILE PHOTO

ALIYEKUWA Balozi wa Tanzania nchini Canada, Alphayo Kidata, hajulikani aliko. Rais John Magufuli alitengua ubalozi wake, akamrejesha nyumbani, na akamvua hadhi ya ubalozi.

Kidata alirejea Tanzania tarehe 1 Novemba 2018. Aliitwa Ikulu tarehe 5 Novemba 2018. Hiyo ndiyo ilikuwa mara yake ya mwisho kuonekana hadharani, kwa mujibu wa kumbukumbu rasmi.

SAUTI KUBWA limekuwa linamtafuta kumhoji kuhusu masuala kadhaa yanayomhusu lakini halikufanikiwa kumpata. Baadhi ya maofisa wa serikali wanadai “amepotea,” wengine wanadai amejificha, wengine wanadai amefichwa, huku familia ikidai haijui aliko. Baadhi ya watendaji wa serikali wanasema, “tunaogopa kuulizia mustakabali wake.”

Kabla ya kuteuliwa kuwa balozi, Kidata alifanya kazi Ikulu kwa miezi saba akiwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais tangu Machi 2017, baada ya kuwa Kaimu Kamishana Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) tangu Desemba 2015.

Hakuna taarifa za rasmi kuhusu sababu zilizosababisha ubalozi wake usitishwe na kutenguliwa, lakini SAUTI KUBWA linatambua kuwa serikali ilikuwa inafanya maandalizi ya kumfikisha mahakamani kwa agizo la Rais Magufuli.

Hata hivyo, baadhi ya maswahiba wa Rais Magufuli, wanaotoka maeneo yale yale na Kidata na Magufuli mwenyewe, wamemshauri rais aachane na mpango wa kumshitaki KIdata, kwa maelezo kuwa tuhuma zinazomkabili si zake peke yake; na kwamba iwapo atashitakiwa kuna wakubwa wengine walio karibu na rais nao watajikuta matatani.

Taarifa zisizo rasmi zinasema Rais Magufuli amewakubalia. Miongoni mwa maswahiba hao wa rais ni Charles Kitwanga, rafiki yake wa muda mrefu, ambaye alimfukuza kazi ya waziri wa mambo ya ndani katika mazingira yenye utata ambayo ingawa serikali ilitaka kuyahusisha na “ulevi wa waziri,” yalilenga kumnusuru Kitwanga katika sakata la ufisadi wa Lugumi. Kitwanga ni mmoja wa watu wanaoaminika kwa Rais Magufuli hata sasa. Na sakata la Lugumi limemalizwa kinyemela.

Kuna taarifa kuwa Kidata, alipokuwa bosi wa TRA, alifumbia macho mzigo wa kigogo mmoja ambaye haivi na rais. Kitwanga na wenzake wamemlaumu rais kwa kumvua Kidata ubalozi wakisema tuhuma zinazomkabili hazihusiani kabisa na uamuzi wa rais kumvua cheo hicho.

Bado kuna utata kuhusu Kidata, kama ni kweli kuwa serikali na familia hawajui alipo. Mmoja wa ndugu wa Kidata ameliambia SAUTI KUBWA: “Hatujui alipo ndugu yetu. Tutafurahi iwapo atajitokeza yeye mwenyewe au mtu yeyote anayejua akatujulisha aliko. Mazingira ya sasa yanatia hofu na wasiwasi…”

Like
6

Leave a Comment

Your email address will not be published.