Membe amburuza Musiba kortini

Bernard Membe - PICHA YA MAKTABA

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mstaafu, Bernard Membe, amefungua shauri mahakama kuu dhidi ya Cyprian Musiba akimtaka alipe mabilioni ya fedha kwa kumchafua.

Shauri hili tayari limesajiliwa Mahakama Kuu ya Tanzania katikati ya wiki hii. Ni shauri namba 220 la mwaka 2018. Wanaoshitakiwa ni Musiba, mhariri wa gazeti la Tanzanite, na wachapishaji wa gazeti hilo. Membe anawataka wamlipe Sh. bilioni 10 kwa kumchafua.

Katika shauri hilo, Membe anawakilishwa na kampuni ya Millennium Law Chambers ya Dar es Salaam. Hadi tunakwenda mitamboni, mahakama ilikuwa inakamilisha utaratibu wa kisheria wa kuita washitakiwa mahakamani.

Musiba, ambaye amekuwa anajiita mwanaharakati anayejitegemea anayetetea Rais John Magufuli, anashitakiwa kwa kutoa matusi dhidi ya Membe na kumtuhumu kuwa anamhujumu Rais Magufuli, na kwamba mbinu mojawapo ya kukamilisha hujuma hizo ni maandalizi anayofanya kugombea urais mwaka 2020. Kwa mujibu wa Musiba, ambaye amekuwa anaropoka kila mara katika utetezi wake kwa rais, mipango ya Membe ni sawa na uhaini.   

Hata hivyo, wachunguzi na wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini wanasema kauli za Musiba si zake bali za kutumwa na wakubwa wanaomhofia Membe. Miongoni wa watu ambao wamebainika kumtuma Musiba ni baadhi ya maofisa waandamizi ndani ya idara ya usalama wa taifa, ambao nao wanatumiwa na Ikulu kupima joto na kutisha wanaodhaniwa kuwa “washindani watarajiwa” wa rais Magufuli.

Membe alikuwa mshindani wa Magufuli katika kinyang’anyiro cha urais ndani ya CCM mwaka 2015. Jina lake lilikwama katika ngazi ya halmashauri kuu ya CCM.

Zipo taarifa za kuaminika kwamba Magufuli haamini wanaCCM wenzake waliogombea naye mwaka 2015, na kwamba hata walio serikalini mwake, anafanya kila jitihada kuwaminya na kuwaficha wasisikike au wasionekane kwenye jamii katika matukio muhimu.

Ana hofu zaidi kwa kuwa wapo wanaCCM wengi ambao hawaridhiki na mwenendo wake wa kujimilikisha serikali na kutetea mambo ambayo yanatia doa taifa, na yanakwenda nje ya misingi ya chama chao.

Kila anachoona chema anakiita chake, lakini kila kasoro anawatupia wenzake waliomtangulia. Hata Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na Spika Mstaafu Anna Makinda, mara kadhaa wamesikika wakimshauri aseme, “serikali ya CCM,” lakini yeye na wasaidizi wake wameendelea kuiita, “serikali ya Magufuli.”

Zipo taarifa kuwa baadhi ya wanaCCM wamechoshwa na ubabe wake na wanaandaa wagombea wengine wa mwaka 2020, na wanaweza kumtaka Magufuli awe rais wa muhula mmoja. Baada ya mashushushu wake kunusa taarifa hizo, wameamua kumtoa kafara Membe, na wamemtanguliza Musiba.

Katika hali isiyotarajiwa, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ali, wiki mbili zilizopita alimshambulia Membe kwa kutumia maneno yale yale ya Musiba. Akiwa katika mikutano ya chama mikoani alimtaka waziri huyo wa zamani aende kujieleza ofisini mwake dhidiya tuhuma zinazomkabili.

Agizo la Dk. Bashiru lilishangaza wengi, kwani si utaratibu wa kawaida kuitana ofisini kwa njia hiyo. Miongoni mwa waliokosoa utaratibu huo ni Spika wa zamani wa Bunge la Jamhuri, Pius Msekwa. Wakati ule, Membe alikuwa nje ya nchi.

Watoa habari ndani ya CCM wanasema Membe aliporudi nchini alituma ujumbe kwa katibu mkuu kuitikia wito ili ampe miadi ya kujadili suala hilo, lakini katibu mkuu wake huyo amemkalia kimya hadi leo.

SAUTI KUBWA lilipowauliza wote wawili juu ya usahihi wa taarifa hizo, hawakutoa majibu. Wanaojua ukweli wa mambo wanasema Dk. Bashiru Ali amesukumwa na mambo mawili kumshambulia Membe.

Mmoja wa watendaji wa makao makuu ya CCM waliokerwa na kauli za Musiba na Dk. Bashiru Ali, huku akiomba asitajwe jina, amesema: “Kwanza, ujue kuwa ujumbe ule wa Musiba haukuwa wake, kwani Musiba ni mtu mwenye uelewa mdogo mno, na hajui lolote, bali wanaomtumia wamegundua kuwa ni mropokaji anayeweza kuvalishwa mabomu tu na kulipuka, akidhani wao watamlinda kwa kuwa wanaomtuma ni wakubwa.

“Musiba anatapika kile tu anacholishwa na kuaminishwa kuwa ndiyo msimamo wa rais. Na kiukweli, maneno yale anayosema Musiba ndiyo yanaakisi anachowaza Rais Magufuli, kwa sababu naye ana tatizo la kupenda watu wa aina ya Musiba na Makonda. Hasikilizi watu makini.

“Sasa bosi Bashiru anajua yote hayo. Aliyasema akijua kuwa bosi wake yupo nyuma yake. Akapima upepo, na baadaye akagundua upepo unamwendea vibaya. Msomi wa kiwango chake kufanya anayofanya yeye ni aibu nyingine ambayo haikutarajiwa.”

Mwanasiasa mwingine mkongwa amezungumza na SAUKI KUBWA kuhusu sakata hili, akisema: “Bashiru anajua wanaomtuma Musiba, lakini hajui nguvu ya Membe. Huyu amejichomeka katika siasa za ajabu ajabu, akafuta usomi wake wote. Lakini kwa kufanya haya, amesaidia jamii kujua kwamba Musiba hayupo peke yake, na kwamba wanaomtuma ni hao anaowatetea.”

Anaongeza: “Sasa amepotea, nadhani hatamuita tena Membe ofisini au mitaani maana sidhani kama yeye na Musiba wana ushahidi wa tuhuma zao dhidi ya Membe. Kwa hiyo, amejikausha ili wimbi hilo lipite, lakini wameshamchafua Membe mbele ya umma, naye sidhani kama atawaacha.”

Mbali ya katibu mkuu huyo kukwepa kumuita Membe kama alivyokuwa amedhamiria awali, CCM nayo imegoma kumjadili kama ilivyotarajiwa. Katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM cha Novemba 17 na 18 mwaka huu, hakukuwa na hoja ya kujadili suala la Membe.

Hali hii inaendana na taarifa za siri za wanaCCM waandamizi kuwa Musiba na Bashiru walijiingiza katika propaganda chafu dhidi ya Membe bila maandalizi ya kutosha.

Kwa shauri hili analofungua Membe dhidi ya Musiba, ni dhahiri kuwa mlalamikiwa ameingizwa katika mazingira magumu, kiasi cha “wanaomtuma” kutengeneza tangazo bandia, wakaweka tarehe ya nyuma, kuonyesha kuwa wamemsimamisha uongozi wa kampuni ambayo yeye amekuwa anadai kuwa ndiye mmiliki wake.  

Hiki nacho ni kielelezo kingine kinachochochea taarifa kuwa Musiba amekuwa anatumwa na wale wanaompatia pesa za serikali kuendeshea magazeti yake na kuyatumia dhidi ya wote wanaodhaniwa kumkosoa Rais Magufuli.

Wakati Musiba akipewa pesa za umma kwa kazi hiyo chafu, kwa njia ya matangazo, vyombo vingi binafsi vya habari vinanyimwa matangazo ili vishindwe kujiendesha. Rais Magufuli angependa vyombo vyote vifanye kazi kama anayofanya Musiba na vijigazeti vyake kumsifu na kumtukuza hata kwa habari za kutunga, huku vikizodoa na kushambulia wapinzani na wakosoaji wake.

Shauri hili la Membe linasubiriwa kwa hamu na wananchi wengi wanaofuatilia mtifuano huu unaomweka Rais Magufuli katikati ya majungu na porojo za Musiba na magazeti yake.

Katika halii inayoonyesha kuwa Musiba anatumwa na analindwa na serikali, hata pale msemaji mkuu wa serikali, Dk. Hassan Abbasi, ambaye pia ni msajili wa magazeti, alipolalamikiwa kuhusu uandishi wa hovyo wa “magazeti ya Musiba” alitamka kuwa anayeumizwa nayo ayafikishe mahakamani. Ni Abbasi huyo huyo anayeonya magazeti mengine kwa ukali kila yanapoandika habari za kweli zinazokosoa utendaji wa rais au wa serikali.

Like
10

Leave a Comment

Your email address will not be published.