WIMBI jipya la maambukizi ya ugonjwa wa Corona nchini Tanzania limeibua msimamo mpya wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), na sasa limetoa tamko rasmi kwa waamini wake.
Katika tamko hilo la leo – Januari 25, lililopewa kiremba cha mwongozo, na kusambazwa pia kwa kardinali, maaskofu wakuu, maaskofu na maaskofu wastaafu, TEC inasema kuwa Tanzania ina maambukizo mapya.
Rais wa TEC, Gervas Nyaisonga, ndiye ameandika katika mwongozo huo kwamba viongozi hao wa Kanisa wanapaswa kuwaambia waamini na Watanzania wote kuhusu umuhimu wa kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo unaoendelea kuua watu wengi duniani.
Kwa amri ya Rais John Magufuli, Tanzania ilisitisha utoaji wa takwimu za ugonjwa huo Aprili 29, mwaka jana. Rais Magufuli alidai kuwa Tanzania hakuna Corona kwa kuwa Mungu alisikiliza sala za wananchi wake. Hata Jumapili iliyopita, akiwa katika ibada ya Misa kwenye kanisa la Chato, alitangazia waamini kuwa Tanzania haina Corona.
Kumekuwepo na vitisho kutoka serikalini dhidi ya yeyote anayetangaza kuwepo kwa Corona au wagonjwa wa Corona Tanzania. Kwa sababu ya hofu, hata vyombo vya habari vimekumbwa na wimbi hili, vikaacha kuandika habari za Corona. Madaktari nao wamekuwa wanahofia kusema wazi, lakini baadhi yao wamekuwa wanaiambia SAUTI KUBWA kwa siri kuwa wagonjwa ni wengi, na hali ni mbaya.
Hadi rais anazuia kutangaza takwimu, Tanzania ilikuwa na wagonjwa waliorekodiwa na serikali kuwa wagonjwa 509 na vigo 21. Hadi leo ni nchi pekee duniani isiyo na takwimu rasmi kuhusu hali halisi ya Corona.
Baadhi ya wachambuzi wanasema amri ya rais na tangazo lake kuwa Tanzania haina Corona ni moja ya sababu zilizofanya ongezeko la wagonjwa kwa sababu wananchi waliacha kuchukua tahadhari, na qalijichanganya mno na kupokea wageni kiholela kutoka nje, huku pia wakishiriki mikutano na kampeni ya uchaguzi mkuu bila tahadhari.
Katika wiki chache mfululizo zilizopita, kumekuwepo na taarifa nyingi za wagonjwa na vifo katika mitandao ya kijamii, kiasi cha kushtua umma na watu kuanza “kuasi” dhidi ya katazo la rais.
Wiki iliyopita, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Arusha, Isack Amani, alitoa waraka akiwataka waamini wachukue hatua waachane na hadaa za kisiasa.
Katika tamko la leo kutoka TEC, wakuu hao wa Kanisa wanahimizwa kuwataka waamini na wananchi kwa jumla wafuate misingi ya kujikinga na ugonjwa huo.
Nyaisonga anasema njia za kukabili ugonjwa huo ni kuchukua tahadhari zinazoelekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), njia za kiimani. WHO inaelekeza kunawa mikono kwa maji tiririka (kwa kutumia sabuni), kujiepusha na mikusanyiko na kuvaa barakoa.
Wakati haya yakiendelea, Rais Magufuli amekimbilia Chato nyumbani kwake ambako amepageuza Ikulu isiyo rasmi kwa takribani mwezi mzima sasa. Kuna taaraifa kuwa hali ni mbaya kila mkoa ingawa Dar es Salaam na Dodoma zinaonekana kuongoza kwa wagonjwa na vifo visivyotarajiwa.
Hii ni mara ya pili kwa kanisa hili nchini kutoa tahadhari kwa waumini wake. Mapema mwaka jana, Kanisa Katoliki lilitoa maelekezo yafuatayo kwa waamini wote kuhusiana na huduma zetu za Kichungaji.
SALA: Tunawaomba waamini wote kusali sala maalumu ili kumwomba Mungu atukinge dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona, COVID-19. Tumwombe Mungu aendelee kutulinda kwa mkono wake na kuwaponya wale wote ambao wamepata maambukizi haya. Na wataalamu wetu wapate ufumbuzi wa kisayansi kuzuia kuenea kwa virusi hivi. Sala hii ni jukumu la kila mtu mmoja na jukumu la pamoja kama Kanisa kitaifa. Na Kutakuwa na sala maalumu itakayotolewa na maaskofu lakini kila mmoja wetu anaweza kusali sala inayomfaa kadri inavyoelekezwa na Askofu Jimbo. Ni wakati sasa wa kusali na kufanya toba kama taifa ili kujiunganisha na Muumba wetu.
KWENYE IBADA MBALIMBALI ZA LITURUJIA: Tunaagizwa kuzingatia taratibu za kujikinga na virusi vya Corona kadri serikali ilivyoagiza. Hakikisha kutumia maji safi kwa kuosha mikono kwa sabuni mara kwa mara unapokuwa nyumbani kwako na unapokwenda kujumuika na wengine katika shughuli za kiibada. Maji ya baraka ya kuchovya kwenye milango yatasitishwa kwa muda na tutatakiwa kutumia maji ya baraka kadri tutakavyoelekezwa kijimbo. Wakati wa kutakiana amani tusipeane mikono na waamini wafumbe mikono na kuinamiana kwa heshima. Waamini watakomunika kwenye mikono tu, mapadri wazingatie hili wanapowakomunisha watu.
Mapadri wanapoadhimisha Misa pamoja, watakomunika maumbo yote mawili kwa kuchovya Hostia Takatifu. Waamini wote wanaombwa kutoshiriki ibada na Jumuiya ndogondogo kama unajisikia kuumwa. Badala yake washiriki ibada na huduma kwa njia ya redio na njia nyingine zitakazoelekezwa. Kila mwamini ajitahidi kutumia vitabu vya ibada vya kwake. Wale wote wanaohesabu fedha za matoleo watumie sanitizers kwa ajili ya kusafisha mikono.
HUDUMA ZA MASAKRAMENTI: Wagonjwa watapakwa mafuta kwa kutumia pamba na padri aambatane na mhudumu wa afya anapokwenda kwa wagonjwa. Wakati wa kupokea Sakramenti ya Kitubio, Padri anayeungamisha na mwamini wasiangaliane uso kwa uso, na kiti cha kitubio kisitumike bali maungamo yafanyike katika sehemu ya wazi kwa kuzingatia sheria za maungamo.
MAADHIMISHO YA JUMA KUU: Ibada ya kuabudu msalaba ishara ya wokovu wetu, itafanyika kwa kuinamia msalaba bila kuugusa. Sisi Maaskofu wenu tutaendelea kutoa maelekezo kadri serikali yetu itakavyoendelea kutoa miongozo na maelekezo ya jinsi ya kudhibiti maambukizi katika nchi yetu.