Rais Magufuli amejipa likizo ya siku 150 kijijini kwake Chato? Kwa sheria ipi?

President Magufuli - File photo

NAOMBA kuchangia mjadala kuhusu hatua ya Rais John Magufuli kuhamishia Ikulu nyumbani kwake Chato- kinyemela.

Ni makosa makubwa. Ni matumizi mabaya ya madaraka kwa kiongozi wa nchi kuhamishia Ikulu (iwe Ikulu kubwa yenyewe au Ikulu ndogo) nyumbani kwake. Kwanini?

Kwanza, in it’s very nature,  Ikulu ni jengo la serikali ambalo ni makazi ya rais wa nchi. Na makazi hayo yapo kwenye makao makuu ya serikali. Kwetu sisi, makao makuu hayo ni Dodoma na Dar es Salaam.

Pili, nyumba hiyo (Ikulu) si tu kwamba inakuwa na ofisi ya rais, lakini pia ndiyo inashughulika na majukumu yote rasmi ya rais – ikiwa ni pamoja na kuapisha viongozi wa juu wa serikali, kukaribisha viongozi kutoka nchi za nje, dhifa za kitaifa, vikao vya Baraza la Mawaziri – na kiusalama ni mahali penye ulinzi mkubwa, na ni “mahali patakatifu.” 

Tatu, kwenye mji ambao kuna Ikulu, mara nyingi utakuta kuna Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani, na Bunge. Kuwepo kwa majengo hayo matatu ndiyo kunathibitisha uwepo wa serikali kuu mahali hapo.

Nne, majengo mengine yanayoitwa Ikulu ndogo, kwa kweli ni nyumba za mapumziko tu ambazo kiongozi wa nchi anapokuwa ziarani hufikia. Gharama zote za uendeshaji wa Ikulu, iwe ndogo au kubwa, hugharamiwa na serikali.

Rais Magufuli anakosea. Chato si Ikulu. Msasani, Butiama, Msoga na Masasi nyumbani kwa marais wastaafu, hakujawahi kuwa Ikulu wala Ikulu ndogo za marais hao. 

Chato haipaswi kupewa umaalumu wa kipekee. Hata suala la likizo nalo ni la maudhi. Rais ana haki ya kuchukua likizo kwa kumwandikia Katibu Mkuu Kiongozi na kuliarifu Baraza la Mawaziri.

Huu ni mwezi wa tano tangu Rais akae Chato. Mwaka jana mwanzoni alikaa siku 56 Chato na Rubondo. Sasa yupo huko kwa zaidi ya siku 150. Hiyo haiwezi kuwa likizo. Huyu ama amehamia, au ameikimbia Ikulu. Amekwenda nyumbani kwao.

Likizo ya rais ni ya siku 28 kama watumishi wengine. Na kwa uzoefu wetu, tangu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hadi Kikwete, hakuna rais aliyekwenda likizo ya siku 28.

Na kama yupo likizo, hana uhalali wowote kisheria wa kutawala nchi akiwa likizo ambayo haipo kisheria wala kikatiba. Ni mtoro! 

Kulingana na mipango inayoendelea, Chato sasa inaandaliwa kuwa makao makuu ya mkoa mpya wa Rubondo. Kamwe, Chato si makao makuu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano. 

Ajabu ni kwamba majengo yanayojengwa Chato wala hayafanani na majengo ya makao makuu ya mikoa. Yanafanana na ya makao makuu ya Serikali. 

Nia yake kwa kweli ni kuifanya Chato kuwa Ikulu kisirisiri kutokana na aina ya miundombinu na majengo makubwa anayojenga – mahakama, mamlaka ya mapato, benki, uwanja wa mpira, uwanja wa ndege, madaraja, na kadhalika.

Kwanini Magufuli anafanya yote haya?

Kimsingi, hajui atendalo. Kama anajua, basi anajua kuwa anaogopwa.  Bunge halifanyi kitu, vyombo vya habari havina sauti. Kwa hiyo, anajifanyia atakavyo.

Anapata fedha nyingi za bure. Kila kitu kinagharamiwa na serikali. Wageni wote wanalipia kila kitu wanapoenda kule.

Ipo sababu nyingine. Anaogopa kukaa Ikulu ya Dar es Salaam. Anaogopa pia kulala Ikulu ya Dodoma. Tunaambiwa ameambiwa kuwa Ikulu hizo zina majini.  Hizi ni sababu za kishirikina.

Ipo sababu nyingine maalumu ya kumkimbiza Dar es Salaam. Baadhi ya wasaidizi wake wanadai kuwa kila awapo Dar es Salaam husumbuliwa na “mzimu” wa Ben Saanane, mwanaharakati aliyepotezwa na “watu wasiojulikana” tangu Novemba 2016.

Wanadai kuwa baada ya kuwagomea madai yao, Saanane aliamriwa afikishwe Ikulu Dar es Salaam; na katika kumhoji kwa hamaki, huku akiwa ameshikiwa bastola usoni, ilimfyatukia akapoteza maisha. Mwili wake ulibebwa na kutupwa katika Mto Ruvu ili aliwe na mamba na kupoteza ushahidi.

Miongoni mwa watu wanaodaiwa kumpeleka Ikulu na hatimaye kutupa mwili wake majini, wawili walishapatwa na masahibu makubwa. Mmoja alikufa baada ya kuumwa kichwa mfululizo na mwingine alikatika miguu yote baada ya kupata ajali ya gari maeneo ya Bagamoyo mwaka juzi, akapoteza na ajira. Mwingine aliyekuwa na cheo jeshini alikumbwa na mkasa, akashushwa cheo.

Lakini kuna haja ya kukumbuka kuwa Chato ni mfano wa Gbadolite. kijiji cha nyumbani kwa Rais Mobutu Seseseko wa Zaire – enzi zile.

Wanaoikumbuka (hata wasioijua wanaweza kufanya utafiti) watakubaliana nami kuwa kile kijiji cha nyumbani kwao Rais Mobutu ambacho alikipendelea na kukigeuza paradiso kwa miundombinu na miradi mikubwa kama tunavyoona Chato, kilichakaa mara baada ya yeye kuondolewa madarakani.

Rais kutumia raslimali za taifa kujenga nyumbani kwake ni wizi. Ni ufisadi ambao unapaswa ukemewe na kila mmoja anayejiita mzalendo, anayelitakia mema taifa la Tanzania.

Niamini, Rais Magufuli, kwa kufanya yale yale ya Mobutu, anajipa raha ya muda mfupi sana kwa miradi ya aina hii. Ni wachache wa aina yake walioishi kwa amani baada ya muda wao kuisha. Na waliogoma kuondoka waliondolewa kwa aibu.

Like