Familia yatoa kauli kuhusu uchunguzi wa mwili wa mlinzi aliyeuawa na mfanyabiashara wa madini Arusha

SAKATA la mfanyabiashara wa madini, Pendaeli Mollel, anayetuhumiwa kumuua Steven Jimmy (mlinzi) akidai kuwa alimwibia pampu ya maji, limechukua sura mpya baada ya ndugu wa marehemu kudai uchunguzi unaonyesha marehemu alichomwa kichwani kwa kisu kitu chenye ncha kali na alijeruhiwa vibaya maeneo mbalimbali ya mwili wake.

Wanadai kuwa uchunguzi huo wa kitabibu uliowashirikisha matatibu, polisi na familia, unaonyesha kuwa sababu ya kifo cha Steven ni damu kuvujia kwenye ubongo. Vile vile, alikuwa na majeraha kwenye maeneo mbalimbali ya mwili, na alivunjwa mikono, mabega na miguu.

Ernest Julius, ambaye ni binamu wa marehemu na alishuhudia mwili ukifanyiwa uchunguzi  katika Hospitali ya Terati, amewaambia waandishi wa habari kuwa  mtaalamu aliwaeleza kwamba kilichosababisha kifo cha Steven ni damu iliyomwagika kwenye ubongo kutokana na jeraha la kukatwa na kitu chenye ncha kali kichwani.

Amesema kuwa uchunguzi wa mwili wa marehemu ambao umehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhi maiti kwenye  hospitali Muriet  ulifanyika April 22, mwaka huu ambapo yeye na Mjomba wa marehemu,  John Jimmy  ni  miongoni mwa watu walioshuhudia.

“Tulikuwa na polisi na sisi kama ndugu tulishuhudia tukawa tumeona mwili wa ndugu yetu ni kama amepigwa sana mwili umeharibika huu mkono wa kushoto umevunjwa, (akionyesha kiganja) vidole vimevunjwa miguu imevunjwa sehemu ya mabega ana majeraha,” amesema Ernest na kuongeza:

“Mtaalam wa Muriet akatuambia kilichosababisha kifo chake (Steven) ni hapa kichwani kwa nyuma kumetobolewa, amepigwa na kitu chenye ncha kali kama shoka vile hivyo damu ilimwagika kwenye ubongo  na ukiingiza kidole kinaingia mpaka ndani ya ubongo . Hata  akiwa hapo Mortuary bado damu inamiminika kutoka kwenye ubongo.” 

Ernest anasema kuwa siku moja kabla ya kuchunguza mwili , Mkuu wa upepelezi, (OC  CID) wa Muriet akiwa na timu yake walimuhoji  yule mlinzi wa nyumba ya jirani na Mollel aliyesema kuwa aliona tukio la kupigwa Steven.

“Wakasema ngoja wafanye kwa vitendo usiku, usiku ulipofika majira ya kama saa mbili wakasema ngoja tuwashe gari tuangalie kama huyu mlinzi ataweza kumtambua mtu au kumuona mtu mbele ya gari wakati anamulikwa,” anasema Ernest na kuongeza:

“Yule mlinzi akaambiwa akajifiche kwenye mgomba alivyojificha siku ya tukio akaulizwa kama anamuona mtu akajibu ndiyo anamuona mtu mwenye shati nyeupe anamulikwa kwa mwanga wa gari akaulizwa unaweza kumtambua akasema ndiyo akamuelezea.”

Ernest anasema kuwa baada ya hapo yeye na baadhi ya ndugu wa marehemu  aliofuatana nao wakarudi nyumbani huku OC CID akiondoka. Siku inayofuata walienda kwa Mkuu wa upelelezi wa mkoa, (RCO) ambaye naye aliamua kufika eneo la tukio.

Mke wa Marehemu, Joyce Steven, ameiomba serikali kusaidia haki iweze kupatikana kwani mume wake hakuwahi kuwa na rekodi yoyote ya uhalifu na hajawahi kupeleka nyumbani hapo kitu chochote alichopata kwa njia isiyo halali.

Anasema kuwa yeye  na marehemu, Steven  wana watoto watano ambapo mkubwa mwenye miaka 13 akiwa anatatizo la ulemavu wa akili huku yeye akiwa ni mjamzito anatarajia kujifungua  muda wowote.

“Mume wangu aliondoka kwenye kazini tarehe 18/4 majira ya saa 11 jioni kesho yake jumanne muda anaotakiwa kuja simuoni nikipiga simu yake haipatikani nikawaambia ndugu na wao wakasaidia kumtafuta ilipofika jumatano ndiyo nikaambiwa kapatikana amekufa,” anaeleza Joyce kwa uchungu na kuongeza.

“Mimi ningeomba serikali iingilie kati ili waliohusika kumuua mume wangu wachukuliwe hatua za kisheria, (analia) Huyu baba mimi nilikuwa namtegemea kwa kila kitu na ukijaribu kuangalia tuna watoto watano na wenyewe ni wadogo , mtoto wangu wa kwanza ni mlemavu wa akili na mimi mwenyewe nategemea kujifungua muda wowote.

“Mimi kila kitu nilikuwa nategemea kupata kutoka kwa mume wangu,mume wangu hakuwa muhalifu hata  hapa ndani mnaweza kupekua hakuna kitu  hochote amewahi kuleta cha kihalifu (analia zaidi).”

Kaka wa marehemu, Joseph alisema kuwa mdogo wake hakuwa na tabia ya wizi huku akiiomba serikali iangalie haki iweze kutendeka kwani marehemu ameacha mke na watoto watano na hakuwa na nyumba ndiyo alikuwa anajipanga amalize kujenga.

“Naiomba serikali isaidie haki ipatikane, hawa  watu waliochukua jukumu la kumtoa mdogo wangu uhai wachukuliwe hatua za kisheri,” alisema Joseph.

Mjomba wa Marehemu, John Nevava, alisema kuwa siku ya jumanne jioni alipata taarifa kutoka kwa mwajiri wa Steven kuwa amekatwa na polisi na kuwa kuwa ilikuwa jioni akaona siku inayofuata atafuatilia.

Anasema kuwa alimtafuta kwenye vituo cha kati cha polisi ambapo aliwapowatajia jina la Steven Jimmy walilitafuta kwenye vitabu vya hawakuoliona wakafungua mahabusu wakaita jina la Steven ikawa hayupo akamuelekeza tuende kituo cha polisi Mbauda napo hakuwa wakatuagiza tuende kituo cha Murieti hakuwa.

Anasema baada ya kumkosa akaamua kurudi kwa mwajiri wake, Mahmoud akamweleza ambapo akamshauri aende kituo cha polisi cha Kisongo kilichopo karibu na uwanja mdogo wa ndege Arusha ambapo polisi walimweleza kuwa kuanzia April 6, mwaka huu hawajapokea mahabusu.

Mfanyabiashara maarufu wa madini jijini Arusha, Pendaeli Mollel maarufu kama Pendaa

“Tulirudi pale kwa Mahmoud lakini hatukumkuta kwa sababu ilikuwa ni muda wa swala alikuwa ameenda msikitini hivyo tukasema kwa kuwa tumeambiwa tajiri aliyedai kuibiwa pampu ya maji nyumba yake ni jirani basi acha tuende tukamuulizie hapo,” amesema Navava na kuongeza:

“Tulipofika hapo tuliwakuta mafundi tukawauliza kuna kijana wetu tunaambiwa ameketwa hapa kwamba kuna mota imeibiwa. Fundi akatwambia tusubiri ampigie tajiri yao huyo Pendael. Alipigia akamwambia Pendael sasa kuna baba yake Yule kijana amefika hapa anamuulizia Yule kijana wake mbona ameenda kule Murieti hayupo

Akamwambia waambie yuko Murieti lakini wakati fundi anatwambia yuko Murieti anatuonyeshea kidole shingoni kuonyesha ishara kuwa kafa tukawaomba namba ya tajiri yao wakasema hawawezi kutupa hivyo tukaondoka tukarudi Murieti.

“Tulipofika Murieti tukamkuta yuleyule kijana aliyetuambia Steven hayupo akatuambia nionhyi ni wanaume sasa bwana Yule Steven amefariki, akatuingiza kwa mkuu wa kituo, (OCS) tukaongea naye akatuambie nyie kamlete tajiri wa marehemu, Mahmoud.”

“Tukatoka kuelekea kwa Mahmoud lakini kabla hatujafika tukamkuta mlinzi anayelinda nyumba ya jirani na kwa Pendael tukamuuliza hivi wakati unalinda juzi usiku haukusikia kelele? Akasema kuwa alisikia kelele hapo kwa tajiri (Pendael)  na mimi baada ya kusikia kelele niliambaa ambaa nikapita kwenye mahindi nikaenda kujificha kwenye mgomba.”

Anasema akiwa pale alimtambua tajiri mwenye nyumba, Pendael Mollel na mdogo wake, na mlinzi na wawili wengine hajawatambua akaonyesha na mahali kijana alipopigiwa. Tulipofika  ni hapo kwenye geti tukakuta fimbo zenye damu nikamwambia yule fundi ni kweli kijana kapigiwa hapa angalia hizi fimbo fundi akasema mimi siji

Anasema kuwa walichukua hizo fimbo mpaka kituo cha polisi Muriet wakawakabidhi hizo fimbo hivyo polisi wakaenda eneo la tukio kwa ajili ya upelelezi.

Kamanda wa polisi mkoani Arusha, Justine Masejo, aliwathibitishia waandishi wa habari mwishoni mwa wiki kuwa wanamshikilia Mollel na watu wengine watatu kuhudiana na tukio hilo.

Alisema kuwa watu watatu waliwakamata jijini Arusha huku Mollel akikamatiwa mkoani Kilimanjaro huku akieleza kuwa upelelezi wa tukio hilo unaendelea.

Like