Dk. Kigwangalla akubali chanjo ya Corona. Apigia chapuo Sputnik V itokayo Russia

MBUNGE wa Nzega Vijijini, Dk. Hamisi Kigwangalla, ambaye ni daktari kitaaluma na waziri wa zamani wa Utalii, amesema kuna umuhimu wa Tanzania kukubali chanjo kama njia ya kupambana na ongezeko la maambukizi ya Corona nchini.

Dk. Kingwangalla anayemalizia shahada yake ya uzamivu (PhD) katika afya ya jamii, akitumia mitandao ya kijamii, ameandika kuwa pamoja na kuwepo na kuanza kutumika kwa chanjo mbalimbali za kutokomeza janga la Corona kwa nchi nyingi, anaamini chanjo ya Sputnik V kutoka Russia ni bora zaidi.

Kigwangalla, ambaye hayumo katika baraza la mawaziri kwa sasa, anaonekana kutokubaliana na msimamo wa serikali kwamba chanjo hazifai. Kigwangalla alikuwemo ndani ya baraza la Magufuli kwa miaka minne – akiongoza Utalii na Maliasili.

Tayari Rais Magufuli amezuia kuletwa kwa chanjo yeyote nchini Tanzania hadi sasa, akieleza kwamba haziaminiki na kwamba ni biahara tu ya matajiri na nchi zilizoendelea ili kujiongezea utajiri zaidi kwa kutumia janga la Corona. Hadi majuzi, Rais Magufuli amekuwa akisisitiza kuwa “Tanzania hakuna Corona.”

Akiwa na shahada ya udaktari, shahada ya uongozi katika biashara (MBA), shahada ya ubobezi katika afya ya jamii (MPH), na akiwa mwanafunzi wa PhD, Dk. Kingwangalla anasema ‘Sputnik V’ haihitaji mfumo wa mnyororo baridi kali kuihifadhi.

Mtaalamu huyo wa afya ya binadamu anasema tofauti na chanjo zingine, ‘Sputnik V’ inaweza kuhimili mazingira ya hali ya hewa kwa nchi za tropiko, hasa za Afrika, ikiwamo Tanzania na huenda ndiyo chanjo bora zaidi kwa sasa.

“Chanjo za Marekani, ikiwamo maarufu ya ‘Pfizer-BioNtech’ inahitajika kutunzwa kwenye joto la -70, ingawa watengenezaji wake tayari wameomba kurekebisha usajili ili joto la utunzaji wake liwe -20 kwa sasa, haya yote bado ni mazingira magumu kwa nchi zinazoendelea, hasa Afrika,” ameleza daktari huyo.

Daktari huyo anashauri kwamba Tanzania inaweza kuifikiria chanjo ya Sputnik V na kuanza kufanya utafiti kuhusu chanjo hiyo ili kujiridhisha kwa ubora wake kabla ya kuagiza na kuanza kuchanja wananchi wake ili kudhibiti maambukizi ya COVID-19.

Anaeleza kuwa dunia inakoelekea sasa ni kuwepo kwa makatazo kwa wasafiri wote wasiokuwa na chanjo ya COVID-19, hivyo ni vyema Tanzania kuanza kuchanja watu wake kwa kuwalinda na maambukizi na pia kuepuka mtego wa kuzuiwa kusafiri nje ya Tanzania.

Februari 2, 2021 jarida la The Lancet – jarida la afya linaloheshimika duniani lilichapisha andiko la wataalamu linalohakikiha usalama wa chanjo ya Sputnik V kutoka Urusi na kueleza kwamba inafanya kazi na kuzuia maambukizi kwa zaidi ya asilimia 91.6 bila kuleta madhara yoyote kwa binadamu.

Like