Mochuari zaanza kuzidiwa Muhimbili, Ilala, Mwananyamala

VYUMBA vya kuhifadhia maiti katika hospitali za Muhimbili, Ilala na Mwananyamala jijini Dar es Salaam vimefurika. Taarifa hizo zinahusu pia Hospitali ya Mount Meru jijini Arusha.

Uchunguzi wa siku tano uliofanywa na SAUTI KUBWA ndani ya hospitali hizo za rufaa, umethibitika pasipo shaka kuwa idadi ya watu wanaofariki kwa kipindi cha mwezi mmoja sasa, imeongezeka.

“Hakika tunapitia changamoto kubwa sana, pamoja na kwamba ni kazi yetu kuhifadhi na kuhudumia maiti, lakini tumekumbwa na janga, sijui tutakwepea wapi,” amehoji kwa masikitiko mhudumu wa chumba cha kuhifadhi maiti Muhimbili aliyeomba kutotajwa jina.

Hali ya kujaa kwa vyumba huvyo imoenekana Ilala na Mwananyamala, zikiwa ni hospitali za rufaa  baada ya kupandishwa hadhi. Muhimbili ni hospitali kuu ya taifa.

Pamoja na kwamba wahudumu wote waliozungumza na SAUTI KUBWA wakiomba kutotajwa majina yao, lakini wanakiri kuwa “hali ni mbaya,” na wanahemewa na maiti kila siku.

Uchunguzi umeonyesha kuwa ndugu na jamaa wa marehemu katika hospitali hizo wameombwa kuhakikisha maiti za ndugu zao hazikai zaidi ya siku mbili ili kutoa nafasi kwa maiti wengine.

Katika Hospitali ya Muhimbili, majokofu ya kuhifadhi maiti yamejaa na wengine wamekuwa wakilazimika kuwekwa sakafuni, hali ambayo inaelezwa na wataalamu wa vyumba hivyo kuwa ni “hatari sana.”

SAUTI KUBWA ikiwa katika Hospitali ya Muhimbili Jumamosi – Februari 20, usiku saa 5:12, ilifika gari iliyobeba maiti na ndugu walianza taratibu za kuomba kumhifadhi ndugu yao pale, lakini walielezwa kwamba vyumba vya kumhifadhi ndugu yao vimejaa, hivyo waende Hospitali ya Ilala.

Waandishi walifuatana na wafiwa hadi Hospiali ya Ilala, ambako walikutana na maelezo kama ya Muhimbili kwamba vyumba vimejaa na kushauriwa kwenda Hospitali ya Mwananyamala, ambako walifika saa 6.34 usiku na kuambiwa “vyumba vimejaa.”

Hata hivyo, baada ya mazungumzo ya muda mrefu, uongozi wa hospitali hiyo uliruhusu kuhifadhiwa kwa ndugu yao kwa masharti ya kumuondoa siku inayofuata kwani mazingira hayaruhusu – “kumejaa.”

Kutoka Arusha, chanzo chetu cha habari kilisema: “Jirani yangu amefariki, kapelekwa mortuary ya Mount Meru na ndiyo pekee tuliyonayo Arusha, kumejaaaa top.” Picha zilionyesha baadhi maiti zikiwa zimewekwa zimelaliana. Kwa sababu za kimaadili hatuwezi kuchapisha picha hizo.

Pamoja na kwamba wataalamu wa afya wameogopa kuzungumza waziwazi sababu za ongezeko hilo la vifo katika kipindi cha mwezi mmoja, inaaminika kuwa maambukizi ya Corona ndiyo chanzo.

Mwongozo wa serikali kwa hospitali zote ulitolewa hivi karibuni unadaiwa kuwazuia madaktari kutaja chanzo cha kifo kuwa ni Corona, badala yake waeleze na kuandika katika hati za vifo kuwa ni “changamoto ya kupumua” au “nyumonia kali.”

Like
3