MAKUMI ya vijana wahuni kutoka Burundi yameingizwa nchini kwa ajili ya kuongezea nguvu Chama cha Mapinduzi (CCM) katika mkakati wake wa kusaka ushindi kwa nguvu katika uchaguzi wa Jimbo la Buyungu, mkoani Kigoma.
SAUTI KUBWA imeelezwa kwamba vijana hao wa kihuni wapo nchini tangu mwanzo wa wiki hii, na wamesambazwa juzi katika kata zote kwa utaratibu maalumu. Kwenye kata hizo wamepangiwa kushirikiana na vijana wa green guard wa CCM kutengeneza mikakati ya mashambulizi dhidi ya wapinzani, hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Christopher Chiza wa CCM anachuana na Elia Michael wa Chadema, na dalili za awali zinaonyesha kuwa mgombea wa CCM anakabiliwa na hali ngumu kisiasa. CCM na jeshi la polisi wameungana kumnusuru Chiza.
Majukumu ya wahuni hao kutoka Burundi yalitajwa pia katika kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa kilichofanyika tarehe 24 Julai 2018 kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Kakonko.
Mkuu wa mkoa, ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati hiyo, hakuwepo, kwa udhuru. Badala yake kikao kiliongozwa na mkuu wa wilaya.
SAUTI KUBWA inaeleza kwa uhakika kuwa moja ya maazimio ya kikao hicho ni kusambaza wahuni hao kwa makundi katika kata za jimbo ili watoe mafunzo ya ziada kwa green guard.
Kikao kiliazimia pia kwamba lazima viongozi wa CCM katika wilaya watambue na wapeleke orodha ya wapinzani, hasa walio mstari wa mbele, ili iwe rahisi kuwadhibiti.
Walipanga kwamba operesheni ya kushambulia, kutisha na kuumiza wapinzani ianze mwanzoni mwa mwezi Agosti. Iliazimiwa pia kwamba polisi wapewe maagizo maalumu ya kusaidia na kulinda green guard watakapokuwa wameanza operesheni yao.
SAUTI KUBWA imepata taarifa kuwa hata hivyo, wapinzani nao wana taarifa za mipango hiyo na mingine, na wamejipanga kukabiliana na hujuma hizo.
“Tumejipanga. Haya yote tunayajua, na tumejipanga kwa nguvu yetu ya ziada. Tumechoka kuhujumiwa na hawa wahuni; waache waje na fujo zao, watavuna wanachopanda,” amesema John Mrema, mkurugenzi wa mambo ya nje, itifaki na uenezi wa Chadema.