CCM wataka kukamua mzungu milioni 30 za uchaguzi wa kata

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) tayari kimeingia katika kashfa iliyoleta mgawanyiko baada ya viongozi kutofautiana juu ya nguvu na jeuri inayotumika kukamua wafanyabiashara na wawekezaji wa kigeni kwa kisingizio cha kuchangia uchaguzi unaoendelea katika kata mbalimbali nchini.

Baadhi ya viongozi waliokerwa na wizi huo, wameiambia SAUTI KBWA kwamba wanaamini kuwa jukumu la gharama za uchaguzi huo “si la wahindi au wazungu, bali ni chama, kupitia ofisi ya katibu mkuu, na chama kina pesa za uchaguzi.” Mmoja anasema viongozi wake wameomba kiasi cha milioni 30 kutoka kwa mzungu mmoja.

Wanasema wametofautiana na wenzao wanaodai kuwa uchaguzi huu ni wakati mwafaka wa “kupiga dili kama hizi, na kwamba lazima chama tawala kionyeshe nguvu, hata ikibidi kulazimisha wafanyabiashara, hasa wenye asili ya Asia na Ulaya wanaoishi katika maeneo husika, wagharamie uchaguzi, kwa kuwapelekea “barua za kuwaomba michango.” Mmoja wao anasema, “barua zimeandikwa maombi ya mchango, lakini kusema kweli wenzetu wanalazimisha. Huu ni wizi.”

SAUTI KUBWA limefanikiwa kupata nakala ya bajeti ya uchaguzi katika kata ya Namwawala, Wilaya ya Kilombero. Jumla ya shilingi milioni 28 zimepangwa kutumika. Lakini viongozi wanatumia bajeti hiyo kuomba na kutisha wahusika.

Vile vile, SAUTI KUBWA imepata baadhi ya nakala za barua iliyoandikwa na Petronila Kichele, Katibu wa CCM wa wilaya hiyo kwenda kwa mashirika na makampuni mbalimbali yanayoombwa kuchangia uchaguzi, yakiwemo mashirika ya dini na taasisi zinazotoa huduma za kijamii.

Moja ya barua hizo, yenye kumbukumbu namba CCM/WK/U.40/1/VOL.3451 imepelekwa kwa meneja wa SolidarMed, shirika la kigeni lisilo la kiserikali linalojishughulisha na utoaji wa huduma ya afya katika nchi tano za Afrika – Tanzania, Lesotho, Msumbiji, Zambia na Zimbabwe. Barua hiyo ya tarehe 17 Julai 2018, imenakiliwa kwa katibu wa mkoa.

Kilichokera baadhi ya viongozi ni vitisho ambavyo wenzao wanatumia kusaka pesa hizo kutoka kwa watu ambao kwa kazi yao, kwanza hawapaswi kujihusisha na siasa, lakini pia wanatoa mchango mkubwa kwa nchi kupitia huduma za afya.  SAUTI KUBWA imeambatanisha barua mojawapo.

Like
10

Leave a Comment

Your email address will not be published.