Barua ya Ikulu iliyommaliza Mwigulu hii hapa

Merlin Komba, msajili wa vyama wa wizara ya mambo ya ndani, alikuwa anapigwa kama mpira huku na huku. Ikulu ilimwagiza kazi, akaifanya, ikaleta msukosuko kwa umma. Mwigulu Nchemba akiwa waziri wa mambo ya ndani alimsimamisha kazi tarehe 8 Juni 2018; Ikulu ikamrejesha kazini kwa barua ya tarehe 21 Juni 2018; Mwigulu akafukuzwa kazi baada ya siku 10.

Barua kutoka Ikulu kwenda kwa kaimu katibu mkuu wa wizara inasema: “Nakuletea maagizo ya Mamlaka kuwa Bibi Marlin Komba arejeshwe kazini…” SAUTI KUBWA imekuwekea hapa nakala ya barua hiyo ya Ikulu.

Chanzo cha habari cha kuaminika kimeiambia SAUTI KUBWA kuwa mchezo wa ujumbe kutoka Ikulu hadi wizarani hadi makanisani, hadi wizarani, hadi Ikulu tena, na wizarani tena, ulichezwa na mamlaka za Ikulu na vijana wake, wakisaidiwa na wapambe wachache kutoka nje.

Wapambe wa nje waotajwa ni  Daud Albert Bashite (Paul Makonda), Askofu Alex Malasusa ambaye alitengwa na kanisa lake, na ofisa mmoja wa Ikulu aliyetajwa kwa jina la Joachim.

Walimwendea Merlin (msajili) na kumpa ujumbe kutoka Ikulu kwamba aandike barua kwa maaskofu kuwataka wafute nyaraka zao za kichungaji, kwamba “wamejifanya miungu watu wasioguswa.” Msajili aliandika barua kali kwa mabaraza ya maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Kuvuja kwa mawasiliano kati ya msajili na KKKT kulileta mtikisiko mkubwa kwa umma. Barua ya TEC haikuvuja. Chanzo kinasema:

Baada ya mambo kuharibika, Mwigulu alimuuliza msajili, naye akamweleza kuwa ni maagizo kutoka Ikulu. Mwigulu akapiga simu Ikulu akiwa na msajili, katibu mkuu kiongozi akasema ni kweli lakini kutokana na hali ilivyo, barua hiyo ikanushwe, na mamlaka za Ikulu zisitajwe popote.

“Wakati Mwigulu anakanusha barua zile, alikuwa anafanya alichoagizwa. Tatizo ni kwamba msajili baada ya kusimamishwa kazi alilalamika kuwa ameonewa, hadi vijana wa Ikulu wakayasikia na kuyafikisha juu. Joachim ndiye alitumwa kwenda kwa msajili kumuonya aache kusema sema kwa kuwa kulikuwa na mpango wa kumrudisha kazini.

“Kwa hiyo, ni kweli kuwa Ikulu ndiyo ilianzisha mchezo huu, ikaagiza maaskofu waandikiwe barua, ikaagiza zikanushwe, na ndiyo ilimfukuza aliyesimamisha msajili, ikarejesha msajili kazini. Vita ya Ikulu na maaskofu ndiyo kwanza imeanza.

 

Like
13

Leave a Comment

Your email address will not be published.