KLABU ya soka ya Arsenal, wakati ikiendelea kusaka mtu wa kuziba nafasi ya kocha anayeondoka, Arsene Wenger, inafikiria kufanya mazungumzo na mfungaji bora wa zamani wa timu hiyo, Thiery Henry.
Kwa mujibu wa mtandao wa Sky Sports News, mazungumzo hayo yamepangwa kufanyika wiki ijayo.
Tayari klabu hiyo imeshazungumza na Mikel Arteta, aliyekuwa mchezaji kiungo wa timu hiyo ambaye sasa ni kocha msaidizi wa Manchester City (bingwa wa EPL 2017/18) inayonolewa na Pep Guadiola.
Taarifa zinasema Arsenal na Arteta waliteta Alhamisi wiki hii, na kuna tetesi kuwa ndiye chaguo namba moja miongoni mwa wanaofikiriwa hadi sasa, lakini mchujo na uamuzi wa mwisho utafanyika baada ya klabu kukamilisha mazungumzo na wengine.
Kwa mujibu wa mipango ya klabu, wangependa kuwa wamepata kocha mpya kabla ya kuanza michuano ya Kombe la Dunia inayotarajiwa kuanza mwezi ujao nchini Urusi.