Wao walitenda, sisi tulihoji – 003

Miaka minne ya kwanza ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete, ndiyo iliweka msingi wa hoja zilizoibua uchambuzi na ukosoaji dhidi ya serikali yake kwa miaka 10 ya uongozi wake, na ndizo zilikomaza ukali wa safu ya Maswali Magumu. Naorodhesha hoja chache hapa chini:

Matukio muhimu ya awali (2005)

• Jakaya Kikwete alipojitokeza tena hadharani kuonesha rasmi nia ya kutaka urais, nilitia shaka. Sikuona kama angekuwa rais anayefaa baada ya Benjamin Mkapa. Watia nia kupitia CCM walijitokeza 11. Kikwete aliwapiku kwa sababu ya maandalizi aliyokuwa amefanya akisaidiwa na rafiki zake wa karibu, wakiongozwa na Edward Lowassa na Rostam Aziz; na mchango mkubwa wa vyombo vya habari.

• Alipoanguka jukwaani siku ya mwisho wa kampeni zake, alizua shaka juu ya afya yake. Wengine walisema ilikuwa ishara kutoka juu kwamba “Tanzania Yenye Neema,” aliyotuahidi, isingewezekana.

• Alipokwepa mdahalo wa wagombea urais, alizua shaka ya wananchi juu ya uwezo, uelewa, upeo, na utayari wake kukabiliana na majukumu ya rais.

• Kwa jinsi alivyoteka vyombo vya habari, na kuvifanya viimbe sifa zake, na kutetea makosa yake, alizua shaka juu ya uwezo na nia yake ya kuwa rais mwadilifu, muwazi, na muwajibikaji.

• Baada ya kuwa rais, akiwa jijini Mwanza, alitoa hotuba akagombeza mtengeneza wa filamu, Hubert Sauper, raia wa Ufaransa, akimlaumu na kumwita mzushi. Sauper alitumia filamu hiyo kuibua ukweli juu ya biashara ya silaha, samaki, na ukahaba – na jinsi ilivyohatarisha usalama wa wananchi. Serikali haikutaka ukweli huu ujulikane. Katika sakata hili, serikali ilimtia msukosuko mwandishi wa habari Richard Mgamba, mmoja wa watu waliomsaidia Sauper kupata watu na taarifa muhimu na kutoa tafsiri ya Kiingereza kwa ajili ya filamu hiyo. Serikali ilimsakama, hadi akalazimika kuhama Mwanza na kupata hifadhi mkoani Dar es Salaam. Nyota yake kitaaluma ikawakia Dar es Salaam. Katika hali ya kushangaza, makundi ya watu waliodaiwa kuwa wanachama wa CCM waliandaliwa wakaaandamana mjini Mwanza kumpongeza Rais Kikwete kwa hotuba yake, huku baadhi ya wananchi wakiguna chini chini.

Majaribio na mafanikio hafifu (2006)

• Rais Kikwete alipokutana na wafanyabiashara kuwashukuru, katika ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam, aliwambia wana CCM wenzake wabuni mbinu za kupata fedha safi za kufanyia kampeni. Kwa kauli hiyo tu, rais alizua shaka juu ya uchafu wa pesa iliyotumika kumwingiza madarakani. Nikakumbuka simulizi ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuhusu urais na pesa ya bangi mwaka 1995. Ajabu! Miaka 11 baadaye, tarehe 12 Machi 2017, Rais na Mwenyekiti mpya wa CCM John Magufuli, mrithi wa Kikwete, aliwambia wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM, Mjini Dodoma, kuwa licha ya utajiri wa chama hicho, bado chama hicho kimeendelea kuwa ombaomba na kupokea fedha kutoka kwa “watu wasiostahili.”

• Wimbi la ujambazi lilikuwa kubwa, huku kukiwa na tetesi kuwa baadhi ya majambazi walifadhili kampeni za urais CCM. Rais akasema anawafahamu kwa majina, ana orodha yao. Alisema pia anawajua wala rushwa, akawataka waache mara moja. Tukamtaka awataje, na awashughulikie.

• Kuna kitu kiliitwa “Mabilioni ya Kikwete.” Benki ya CRDB iliamriwa na serikali kutoa shilingi bilioni moja kwa kila mkoa ili kuwezesha wajasiriamali wazalendo. Mfumo wa kuzitoa, na shabaha yake, vilizua shaka, na vilihojiwa.

• Gado (Robert Mwampembwa) mchoraji wa katuni wa gazeti la Daily Nation la Kenya, alichora katuni ya waandishi wa habari wa Tanzania wakiwa Ikulu wanalamba miguu ya rais badala ya kumuuliza maswali. Serikali na baadhi ya waandishi walishambulia mchora katuni kwa maneno makali. Wengine walishambulia serikali ya Kenya, na Wakenya, kwa kudhalilisha rais wetu na waandishi wetu.

• Nikiwa Toronto, Canada, kwenye mkutano wa kimataifa wa masuala ya Ukimwi, niligundua jinsi ubabe wa serikali na woga wa wananchi vilivyosababisha maafa makubwa kwa raia wa China, Ukimwi ukaenea kirahisi. Nikakumbuka jinsi wananchi na vyombo vya habari vya Tanzania vilivyokuwa vinaogopa kumkosoa rais. Nikahimiza wananchi waache woga.

• Ubabe wa waziri mkuu Edward Lowassa dhidi ya gazeti la Tanzania Daima ulinipa hisia kwamba viongozi wetu hawapo tayari kukosolewa, na hawataki uhuru wa maoni, uhuru wa kujieleza; na wapo tayari kuingilia kazi za taaluma ya habari. Wanaogopa nini? Wanaficha nini?

Ubabe na ufisadi wa serikali ya Kikwete (2007)

• Serikali iliandaa “mamluki” wa kuisaidia kuandika magazetini, kushambulia baadhi ya wanasiasa, na wahariri waliokuwa wanakosoa serikali, hasa Ansbert Ngurumo, Absalom Kibanda, na Freeman Mbowe (aliyekuwa anaandika Waraka wa Mbowe kila Jumatano katika gazeti la Tanzania Daima). Siri ilivuja kabla hawajaanza. Walipoanza tu, baadhi yetu uliojua njama zao tukatungua watangulizi wao. Mkakati wao ukafa.

• Wapinzani walisema nchi inaongozwa kisanii. Baadhi ya vyombo vya habari vilianza kuwa na ujasiri wa kuandika habari hizo kwamba rais na waziri mkuu wake ni “wasanii.” Rais akadiriki kukataa kuitwa msanii. Nikamjibu kwa vielelezo.

• Kulikuwa na ugomvi wa “ukubwa” kati ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta, na Waziri Mkuu, Edward Lowassa, hasa bungeni. Mgogoro ukazaa makundi ya washindani ndani ya CCM. Lowassa akabaki na Kikwete wake, Sitta akashikamana na Dk. Harrison Mwakyembe.

• Hoja ya ufisadi: EPA, Mkataba wa Buzwagi, na orodha ya mafisadi vilitawala siasa za mwaka 2007. Wapinzani walitumia mahakama ya umma kuumbua viongozi wa serikali baada ya jitihada za kibunge kuzuiwa na spika. Vyombo vya habari viliogopa kuandika majina ya vigogo waliotajwa kwenye mkutano wa hadhara. Magazeti mawili tu – MwanaHALISI na Daily News – ndiyo yaliandika majina hayo, ingawa Daily News halikuiandika kwa undani. Gazeti la HabariLeo liliandika majina hayo katika tovuti yake, lakini yalifutwa baada ya muda mfupi.

• Akiwa safarini Ulaya, Rais Kikwete aliwambia waandishi wa habari kuwa hajui kwanini Tanzania ni maskini. Shaka ya baadhi yetu ikakua.

• Waislamu waliamka kudai Mahakama ya Kadhi Mkuu waliyoahidiwa na Kikwete wakati wa kampeni za 2005. Mchungaji Christopher Mtikila akapinga Waislamu, akidai kwamba madai yao ni kinyume cha katiba. Akatishia kufungua shauri dhidi yao mahakamani. Nao, badala ya kuendelea kumbana Rais Kikwete, wakamgeukia Mtikila. Nikawaandikia kuwataka wambane Kikwete, waachane na Mtikila. Matokeo yake, Mtikila akafungua shauri mahakamani dhidi yangu na gazeti la Tanzania Daima kwamba tulimchafua.

• Ugumu wa maisha uliongezeka. Ajenda ya ufisadi ikashika kasi. Watawala wakajikita katika kutumia propaganda kughilibu wananchi. Wananchi nao wakajenga chuki dhidi ya CCM. Wengine wakajiapiza kuiondoa madarakani, hata ikibidi kuchagua jiwe.

Lowassa nje ya serikali ya Kikwete (2008)

• Serikali iliangushwa Bungeni kwa kashfa ya Richmond. Waziri mkuu alijiuzulu; baraza la mawaziri likavunjika. Mizengo Pinda akawa waziri mkuu. Ukawa mwanzo wa mwisho wa Edward Lowassa katika siasa za CCM.

• Ufisadi ndiyo ilikuwa sifa kuu ya serikali ya awamu ya nne, chini ya Rais Kikwete.

• Baada ya kuzidiwa na mashambulizi, serikali ya Rais Kikwete iliyokuwa inajiita rafiki wa vyombo vya habari, ikaanza kutisha baadhi ya waandishi wa habari, wahariri, wamiliki, na wanaharakati.

• Ugonjwa wa ghafla na kifo cha Gavana wa Benki Kuu, Daudi Balali vilizua utata. Serikali ilidai haijui alikougulia, wala alikofia. Baadaye taarifa zilisema kuwa alifia Marekani. Hakuna anayejua alikozikwa. Hakuna ofisa wa serikali aliyeshiriki mazishi yake. Lakini huyu ndiye alikuwa na siri nzito juu ya ufisadi wa EPA. Msemaji wa Ikulu alidai serikali ina mkono mrefu, kwamba kama ingemtaka ingemrejesha akiwa hai. Tukajua kuwa “kifo cha Balali” kililenga kuua ushahidi wa EPA, lakini pia kwa kifo cha aina hiyo kwa Gavana wa Benki Kuu, hata imani ya wananchi kwa serikali ilikufa. Hadi sasa wananchi wengine hawaamini kama Balali alikufa.

• Halmashauri Kuu ya CCM ilitangaza rasmi kwamba Lowassa hakuwa fisadi. Lengo lilikuwa kumnyamazisha baada ya kutambua kwamba walimtwika mzigo usio wake, na baada ya kuona ameanza kujitetea. CCM haikutaka Lowassa aseme kuhusu wamiliki halali wa Richmond na jinsi rais alivyohusika katika mchakato wa ufisadi uliomwandama na kumchafua waziri mkuu peke yake.

• Serikali ilituma vibaka ili wadhuru waandishi na wahariri wa gazeti la MwanaHALISI lililokuwa linakosoa serikali mfululizo. Mkurugenzi wa gazeti, Saed Kubenea, na mshauri wa gazeti, Ndimara Tegambwage, walivamiwa, wakaumizwa kwa mapanga vichwani, na kumwagiwa usoni kimiminika kinachodhaniwa kuwa ni tindikali. Baada ya upelelezi, mtuhumiwa mkuu alikamatwa. Lakini alitoroka katika mazingira yenye utata, akiwa mikononi mwa polisi. Baada ya polisi kumtambua, naye alikiri na kutaja majina ya vigogo waliokuwa wamemtuma, na kwamba yeye aliagiza vibaka kutekeleza uhalifu huo. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni ACP Leonard, aliyekuwa amesimamia ukamatwaji wa mtuhumiwa huyo, naye alihamishiwa kwenye mkoa wa Geita, katika Kanda ya Ziwa Victoria. Ushahidi ukafa.

• Baadhi yetu tulianza kulaumu Kikwete, Lowassa, na Rostam kwa kuteka na kudhoofisha vyombo vya habari. Binafsi niliandika na kusisitiza pia kuwa kosa kuu la Lowassa na Rostam ni kutuwekea Kikwete Ikulu.

• Watanzania walianza kuhoji “mabilioni ya Kikwete.” Katika kipindi hiki ndipo kulizuka hoja ya “ombwe la uongozi.”

Ulaghai wa kisiasa kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi (2009)

• Ubabe wa serikali ya Kikwete ulikuwa umechomoza kwa kiasi kikubwa, uungwana wa awali alioanza nao ukapotea. Serikali ilikuwa na hofu.

• Katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa umoja wa wanawake wa CCM, Rais Kikwete alisema yupo tayari kujitoa mhanga katika vita dhidi ya ufisadi. Hatukumwamini. Aliondoka madarakani bila kujitoa mhanga.

• Wananchi walianza kuhoji: Yako wapi Maisha Bora kwa kila Mtanzania? Ipo wapi ‘Tanzania Yenye Neema’ tuliyoahidiwa mwaka 2005?

• Mjadala mpya uliibuka juu ya mitambo ya umeme, giza linalonyemelea taifa, na umuhimu wa TANESCO kununua mitambo ya Dowans. Dk. Mwakyembe na Sitta wakafanikiwa kutumia bunge kuzuia serikali kununua mitambo ya Dowans, kwa maelezo kuwa ni mitumba, na ni mali ya kifisadi.

• Ukweli kuhusu mradi wa umeme wa upepo wa Dk. Harrison Mwakyembe na wenzake, mkoani Singida, ulikuwa haujajulikana. Ulipojulikana, tukaweza kutambua sababu kuu ya ushindani wa Dk. Mwakyembe na wamiliki wa Richmond, na baadaye Dowans – kumbe ulikuwa ushindani wa kimaslahi, lakini Dk. Mwakyembe hakutangaza maslahi hayo alipokuwa anawashughulikia washindani wake kwa kutumia Kamati Teule ya Bunge. Baadhi yetu tulimwamini, akatupotosha katika sakata la Richmond.

• Waislamu walikuja juu tena, wakamkumbusha rais ahadi ya Mahakama wa Kadhi Mkuu.

• Picha ya mtandao wa Ze Utamu iliyomdhihaki Rais Kikwete ilileta mjadala mkubwa. Mtandao huo ulifungwa mara moja, wahusika wakatiwa mbaroni.

• Dk. Reginald Mengi alizungumza na vyombo vya habari, akatuhumu “mafisadi papa” watano, wafanyabiashara wenye asili ya Kiasia. Baadaye alijibiwa kwa mkutano mwingine wa vyombo vya habari, ulioitishwa na Rostam Azizi, mmoja wa waliokuwa wametajwa na Dk. Mengi. Rostam alitaja wale aliowaita “mafisadi nyangumi.” Mjadala wa ufisadi ukapata mwelekeo mpya.

• Kulikuwa na mjadala juu ya urafiki kati ya serikali na mafisadi, kiasi cha serikali kuonekana ipo mifukoni mwa mafisadi. Haya na mengine mengi ni baadhi ya matendo yao yaliyochochea uandishi wetu, na kufanya wananchi waibuke na maswali magumu kuhusu watawala wetu. Nayo yalikuwa sababu ya wananchi kutaka mabadiliko.

Like
9

Leave a Comment

Your email address will not be published.