ACT-Wazalendo wahoji: Nani anaongoza nchi?

CHAMA Kikuu cha Upinzani Zanzibar, ACT Wazalendo, kimeitaka serikali ya Tanzania iseme nani anaongoza Jamhuri ya Muungano ya Tanzania katika wakati huu wa hali tete kiafya ya Rais John Magufuli.

Zitto Kabwe, Kiongozi wa chama hicho, amesema Rais Magufuli ametoweka kwa siku 16 sasa, na ameitaka serikali kutoka hadharani kueleza umma ni nani kwa sasa anaongoza nchi.

Katika taarifa yake mapema leo, Machi 16, 2021, pamoja na mambo mengine, Zitto amesema kauli zinazogongana zilizotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan zimezidisha taharuki juu ya afya ya Rais Magufuli.

Taarifa hiyo, amesema, ni tathimini ya chama chake kuhusu kutoonekana hadharani kwa Rais Magufuli. Zitto ameainisha mambo manne ambayo yanapaswa kuzingatiwa kwa sasa ikiwamo kuitaka Serikali kupitia Jeshi la Polisi kuwaachia huru watu wote iliowakamata kwa kuzungumzia afya ya rais.

Zitto pia amemtaka Katibu mkuu Kiongozi, Dk Bashiru Ally, kutamka hadharani kuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amekuwa akitekeleza majukumu yake kama Kaimu Rais kwa mujibu wa Katiba na itifaki zote, na atumie muda huo kuliambia taifa hali ya rais.

Katika tamko hilo, Zitto amezitaka taasisi za umma za kifedha ikiwamo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutoka hadharani kuzima tetesi kuhusu yanayoendelea katika taasisi hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa fedha za kigeni na akiba ya dhahabu kulindwa wakati huu wa sintofahamu.

Sambamba na hayo, kiongozi huyo wa chama amezikumbusha taasisi za kiraia ikiwa ni pamoja na Chama cha wanasheria Tanganyika (TLS) na Azaki zingine kupaza sauti zao kuhakikisha ulinzi wa Katiba, na kwamba yatakuwa ni makosa makubwa kuacha siku nyingine 16 zipite nchi ikiwa inaongozwa na watu ambao Katiba haiwapi mamlaka hayo.

Taarifa hiyo inasema: “Tunatoa wito kwa wabunge kutumia kiapo chao kulinda katiba kwa kutoa tamko la kuishinikiza serikali itoe tamko kuhusu afya ya rais.

“Katika siku za hivi karibuni suala la afya ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli limekuwa katika mijadala katika vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi, katika mitandao ya kijamii na katika medani nyinginezo.

“Kukithiri kwa mijadala hiyo kumesababisha hali ya wasiwasi na taharuki miongoni mwa wananchi. Hali hiyo inatia shaka zaidi na kutokuonekana hadharani kwa Rais mwenyewe kwa takriban siku 16 sasa. Aidha, ukimya wa hali ya juu miongoni mwa viongozi serikalini kumeongeza uzito wa suala hili.

“Afya ya Rais, kwa umuhimu wake, ni jambo lililowekewa utaratibu wa kushughulika nalo inapotetereka. Tunatambua pasi na shaka kwamba Rais anaumwa, tunashangazwa na ukimya unaoendelea kutamalaki katika suala hili. Ni kwa kiasi gani ugonjwa wa Rais unasababisha ashindwe kutekeleza majukumu yake ni suala lililo katika utaratibu wa wazi wa katiba

” Tunatoa wito kwa Serikali, kwanza iwaachie watu wote waliokamatwa na Jeshi la Polisi kwa kuhoji juu ya afya ya Rais, kisha ifanye yafuatayo ili kutuliza mshawasha wa wananchi;

“Itueleze wananchi hali halisi ya afya ya Rais, itumie pia maelezo hayo kutujibu kwa kina wananchi iwapo Rais bado anao uwezo wa kutekeleza majukumu yake au la.

” Iwapo Rais hana uwezo huo au afya yake imetetereka kiasi cha kutia mashaka, basi kifungu cha 37(2) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kitekelezwe ili jopo la matabibu litakaloteuliwa na Jaji Mkuu lifanye kazi yake na hali ya afya ya Rais ijulikane wazi kupitia kwa Spika.

“Katibu Mkuu Kiongozi atamke rasmi kuwa Makamu wa Rais amekuwa akitekeleza madaraka ya Rais Kwa mujibu wa Katiba na kwamba ni Kaimu Rais Kwa mujibu wa Itifiki zote. Hivyo basi kumtaka Makamu wa Rais atekeleze majukumu uRais Kwa mujibu wa Katiba na atumie nafasi hiyo kulieleza Taifa Hali ya Rais.

“Wakuu wa Mashirika ya Umma, na haswa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) watoke kuzima tetesi zinazoenea juu ya yanayoendelea katika taasisi hiyo nyeti kwa uchumi wa Nchi. Ni muhimu rekodi ya Fedha za Kigeni na Akiba ya Dhahabu zilindwe. Wakati huu wa sintofahamu ni vizuri Makamu wa Rais peke yake kama Kaimu Rais ndiye anapaswa kuidhinisha kwa kauli thabiti kinachoitwa ‘maagizo ya Rais’. Wananchi watahitaji Taarifa kuhusu Akiba hizi mara baada ya sintofahamu hii kuisha.

“Vile vile unatoa mwito kwa TLS (Chama cha wanasheria wa Tanganyika) na AZAKI nyingine za uwajibikaji wapaze sauti zao katika suala hili ili kulinda Katiba” amesema Zitto Kabwe na kuongeza kuwa afya ya Rais ni suala la kikatiba haipaswi kuchukuliwa kama kuna kosa kwa wanaotaka kuifuatilia.”

Like