Kesi ya Mbowe: Luteni Urio ahitimisha ushahidi baada ya kibano cha Kibatala kwa siku nne

Kama ilivyowasilishwa na ripota raia, BJ, leo Februari 1, 2022

Jumla ya maswali yaliyoulizwa leo na Wakili Kibatala leo ni 161. Yaliyojibiwa na shahidi ni 157. Miongoni mwa hayo majibu (idadi ikiwa katika mabano) ya ‘SIFAHAMU’ (29) ‘NAFAHAMU’ (9), ‘HAPANA’ (5), ‘SIJUI’ (4), ‘NAKUMBUKA’ (2) na ‘NAMFAHAMU’ (2). Maswali yaliyoulizwa na Mawakili wa Serikali ni 15.

Jaji ameingia Mahakamani 3:44 leo Jumanne, Februari 1, 2022.

Kesi namba 16 ya mwaka 2021 ya Jamuhuri dhidi ya Khalfani Bwire, Adam Kasekwa, Mohammed Ling’wenya na Freeman Mbowe imeshatajwa.

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Ikupendeza Mheshimiwa Jaji mimi naitwa Robert Kidando, nipo pamoja na wakili:

  1. Pius Hilla
  2. Abdallah Chavula
  3. Jenitreza Kitali
  4. Nassoro Katuga
  5. Esther Martin
  6. Ignasi Mwinuka

Peter Kibatala Mheshimiwa Jaji ikupendeza naitwa Peter Kibatala na nipo pamoja

  1. Hadija Aron
  2. Michael Mwangasa
  3. Maria Mushi
  4. Dickson Matata
  5. Alex Massaba
  6. Seleman Matauka
  7. Michael Mwangasa
  8. Nashon Nkungu
  9. Lusako Mwaiseke anayeshika mikoba ya Wakili John Malya kwa leo.

(Jaji anawaita washitakiwa wote wanne na wote wanaitika kuwa wapo Mahakamani).

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji na sisi tupo tayari kuendelea.

KIBATALA: Shahidi habari za toka jana?

SHAHIDI: Nzuri.

KIBATALA: Uliwahi kufahamishwa katika kesi hii jabla ya kuendelea kuliwahi kufanyika kesi ndogo mbili?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Kwa hiyo hufahamu kwamba mshitakiwa Adam Kasekwa na mshitakiwa Mohammed Ling’wenya walisema katika ushahidi wao kuwa wewe ulikuwa mmojawapo wa watu waliokamatwa?

SHAHIDI: Ndiyo nasikia kutoka kwako.

KIBATALA: Naomba unikumbushe tena nani aliyekupa taarifa ya wewe kuja kutoa ushahidi.

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji, jana ulisema kuwa maswali yasirudiwe.

KIBATALA: Wacha niulize kwa namna nyingine. Shahidi ulishawahi kukutana na Wakili wa Serikali Robert Kidando kabla ya kutoa ushahidi wako hapa?

SHAHIDI: Nilienda kuripoti Ofisi ya DCI. Baada ya hapo Jumatano nikaripoti hapa na kukutana na mawakili wa Serikali.

KIBATALA: Kwa maana hiyo shahidi hujawahi kuzungumzia lolote kuwa wewe hujawahi kukamatwa na maafisa wa Polisi akiwamo Jumanne Malangahe pamoja na Goodluck?

SHAHIDI: Nasemaje wakati bado sijakamatwa. Siwezi kutoa taarifa ambazo hazijanitokea.

KIBATALA: Katika ushahidi wako hujawahi kupinga kuwa hujawahi kufikishiwa katika Kituo cha Polisi Tazara?

SHAHIDI: Yangekuwa yamenitokea ningemwambia Jaji.

KIBATALA: Kwa maana hiyo pia hujawahi kusema kuwa hujawahi kufikishiwa katika Kituo cha Polisi Mbweni siku ya tarehe 9?

SHAHIDI: Sijawahi kufikishiwa popote kituo cha Polisi wala kuhojiwa.

KIBATALA: Wewe una ugomvi wowote na Adamoo au Ling’wenya?

SHAHIDI: Sijawahi kugombana nao.

KIBATALA: Unaweza kutusaidia kwanini watu hawa wawili watunge uongo wa namna hiyo wenye detail?

SHAHIDI: Mimi sifahamu.

KIBATALA: Na nilikuuliza kwamba detail ya kwamba wewe uliwekwa katika cell ya Polisi Mbweni ambayo ilikuwa kabla ya cell ya Mohammed Ling’wenya?

SHAHIDI: Kwanini unaniwekea maneno?

KIBATALA: Jibu swali. Usikasirike.

KIBATALA: Unafahamu kwanini nilikiwa nakuuliza kuhusu sehemu unayosali na Paroko wako?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Baada ya wao kuhojiwa kwamba nani aliwaunganisha wao na kiongozi wa upinzani Freeman Mbowe, wao baada ya mateso walikutaja wao, na baada ya hapo ukakamatwa?

SHAHIDI: Jana nilishajibu kuwa nilikuwa kamanda wa QRF wakati huo.

KIBATALA: Katika ushahidi wako ulimtaja ex commando anaitwa Khalid?

SHAHIDI: Simfahamu.

KIBATALA: Katika ushahidi wako ulimtaja ex commando anaitwa Gabriel Mhina?

SHAHIDI: Simfahamu.

KIBATALA: Una ugomvi na hawa niliowataja?

SHAHIDI: Sina.

KIBATALA: Unafahamu maana ya ‘mdepo’?

SHAHIDI: Intake mates.

KIBATALA: Khalid anasema wewe ni ‘mdepo’ mwezake.

SHAHIDI: Simfahamu mtu huyo.

KIBATALA: Khalid ana sababu ya kutunga uongo juu yako?

SHAHIDI: Sijui.

KIBATALA: Kwa kuwa wewe ulikuwa unazungumza na Kingai, je, alishawahi kukuambia kuwa kuna washitakiwa wengine makomandoo wawili?

SHAHIDI: Hajawahi kuniambia.

KIBATALA: Kwa hiyo ulikuwa pia hufahamu kuwa katika hii kesi palikuwa na makomandoo wawili ambao walikuwa washtakiwa?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Khalid nasema kuwa baada ya kumwona Bwire anamlinda Freeman Mbowe, anamuuliza kuhusu kazi akasema akuulize wewe. Akakutafuta kwa mtandao wa Facebook.

SHAHIDI: Sasa nawasiliana na Khalid wangapi?

KIBATALA: Mwanzo umesema h7akuna Khalid unayemfahamu ambaye ni ex commando wa 92 KJ.

SHAHIDI: Simfahamu ndiyo. Khalid yeyote.

KIBATALA: Khalid anasema baada ya kuKutafuta wewe, ulimwambia utamtafutia kuhusu kazi ya mgodini.

SHAHIDI: Huyo Khalid simfahamu.

KIBATALA: Na baada ya akina Adamoo na Ling’wenya kukamatwa ukasema kwamba ile kazi imebumburuka kwa hiyo huwezi tena?

SHAHIDI: Simfahamu Khalid. Nihoji watu ambao nimetolea ushahidi.

KIBATALA: Unafahamu kwamba kuna Afisa wa Polisi ambaye anaitwa Jumanne alikuja hapa mahakamani na kukiri kuwakamata Gabriel na Khalid?

SHAHIDI: Sifahamu kuhusu Jumanne, na simfahamu Jumanne.

KIBATALA: Unafahamu kwamba siyo kawaida kwa mtu kusikilizwa vifaa vyake kwa zaidi ya mwaka mmoja?

SHAHIDI: Inategemea sasa na suala lenyewe.

KIBATALA: Kwa vifaa vyako ni mazingira gani?

SHAHIDI: Nilienda kuuliza mwaka mmoja uliopita wakasema bado uchunguzi unaendelea.

KIBATALA: Unamfahamu mtu anaitwa John Urio?

SHAHIDI: Ambaye ni nani?

KIBATALA: Ambaye ni baba yako mdogo.

SHAHIDI: Simfahamu.

KIBATALA: Unakumbuka nilikuuliza kuhusu gari yako ya silver?

SHAHIDI: Nakumbuka.

KIBATALA: Nikakuuliza kuhusu hotel uliyofikia?

SHAHIDI: Nakumbuka.

KIBATALA: Nikisema kwamba wewe upo chini ya ulinzi na haupo huru?

SHAHIDI: Nashangaa sana kufikiria hivyo.

KIBATALA: Unafahamu kwamba gari yako ni mke wako ndiye aliyefuatilia na kuitoa kwa muda mrefu kwa viongozi wa Jeshi?

SHAHIDI: Ni uongo.

KIBATALA: Gari yako imeenda Kihonda lini?

SHAHIDI: Haijawahi kufika Kihonda.

KIBATALA: Una- confirm hapa kwamba gari hiyo imepakiwa kambini Kizuka?

SHAHIDI: Na- confirm na siku ya kwanza ndivyo nilivyo jibu.

KIBATALA: Tukitaka kujua kuwa wewe upo katika Active Duty kwamba hujafukuzwa kazi kwa kosa la kuwasiliana na kiongozi wa upinzani?

SHAHIDI: Unaangalia kitambulisho na kumuuliza mwajiri wake.

KIBATALA: Hakuna Duty Roaster?

SHAHIDI: Ipo. Wewe unauliza Duty Roaster ya kazini kwangu kwanini?

KIBATALA: Wewe jibu swali kwamba moja ya uthibitisho wako kuwa upo active, ni Duty Roaster.

SHAHIDI: Ni kweli.

KIBATALA: Ni nyaraka ipi unathibitisha kwamba wewe ulipewa hiyo QRF Kamanda.

SHAHIDI: Nilisema kwamba kuanzia tarehe 3 nilikuwa QRF kamanda.

KIBATALA: Kwa hiyo nikukuombea ahirisho uende ukalete karatasi linalosema wewe upo katika Active Duty?

SHAHIDI: Wewe si unajua taratibu za ofisi? Naenda kuomba nyaraka kama nani?

KIBATALA: Nasema tena mahakama ikikupa ahirisho kwamba ukalete karatasi ambalo litathibitisha kuwa upo katika Active Duty utaenda kuleta?

SHAHIDI: Andikeni barua ndiyo watanipa. Mimi sina mamlaka.

KIBATALA: Kwa hiyo nikiomba kwa Mahakama na Mahakama ikatafakari ukalete unaweza kuleta hilo karatasi?

SHAHIDI: Ndiyo. Kwa barua naweza kwenda.

KIBATALA: Na huo mchakato unaweza kuchukua siku ngapi kwa makadirio?

SHAHIDI: Siwezi kujua kwa sababu ofisi inaweza kutafakari na kujibu.

KIBATALA: Shahidi ni kweli au si kweli mtoto wako Jackson alipozaliwa, uliletewa huko ulipokuwa huko mafichoni umuone?

WAKILI WA SERIKALI: (Pius Hilla) Mheshimiwa Jaji swali limeshaulizwa.

JAJI: Kuhusu kupelekewa mtoto kumuona halijaulizwa.

KIBATALA: Shahidi ni kweli au si kweli kwamba mtoto wako alipozaliwa uliletewa mtoto ulipokuwa mafichoni umuone?

SHAHIDI: yaani mtoto azaliwe halafu niletewe kizuizini? Jaribu ku- think kidogo wakili msomi. Who are you by the way?

KIBATALA: Shahidi jibu swali. Usikasirike.

KIBATALA: Ni kweli hata mama yako alikuja kukuona ulipokuwa kizuizini huko mafichoni?

SHAHIDI: Sijawahi kuwa kizuizini.

KIBATALA: Ni kweli au si kweli hata unapokuja hapa Mahakamani unasindikzwa na maafisa wa Jeshi wenye silaha?

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji, shahidi kila saa anasema hayupo kizuizini. Wakili aulize maswali yenye mantik. Sioni kwanini atoe allegations.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji sijatoa allegations. Sisi tunauliza maswali (ili) tukileta mashahidi mbao watayathibitisha kuwa shahidi alikuwa kizuizini, isionekane (kwamba) hatukuuliza. Kama Wakili wa Serikali anachagua swali la kuuliza na namna ya kujitetea, basi wasiwe wanaleta kesi Mahakamani.

JAJI: Swali linahusu knowledge, sioni kama kuna tatizo shahidi kujibu.

KIBATALA: Ni kweli au si kweli kwamba shahidi unapokuja Mahakamani upo kizuizini na unasindikzwa na maafisa wa Usalama wenye silaha?

KIBATALA: Sipo kizuizini. Mawakili wananipitia kila siku hotelini.

KIBATALA: Magari yanayokupitia huko hotelini ni magari yao binafsi au ya Serikali? Hao mawakili unasema ni wa kwako?

SHAHIDI: Sijui kama ni magari yao au ya serikali. Labda niende kuyakagua.

KIBATALA: Je, jibu lako kwamba mawakili wako (Mawakili wa Serikali) inaoanisha vipi na jibu la kwamba unakutana nao asubuhi Mahakamani? Je, hizo dhana mbili zinaoana?

SHAHIDI: Nahisi hujaeleza narudia tena. Siku ya kwanza nimekuja kukutana na mawakili hapa Mahakamani. Baada ya hapo kila siku nakuja nao na kuondoka nao.

KIBATALA: Shahidi sawa. Kazi yangu ni kuuliza maswali.

KIBATALA: Unaweza kufahamu shahidi mwingine yeyote ambaye anapitiwa hotelini na mawakili wa Serikali kuletwa Mahakamani?

SHAHIDI: Mie sijihusishi na shahidi mwingine.

KIBATALA: Ni sahihi kwamba ni utaratibu wa kupitiwa hotelini na kurudishwa Hotelini?

SHAHIDI: Siyo kila siku. Kuna siku napewa mtu wa kukupeleka.

KIBATALA: Kama lini vile?

SHAHIDI: Hata Ijumaa.

KIBATALA: Uliondoka na gari gani?

SHAHIDI: Gari ndogo.

KIBATALA: Ni mtu binafsi au mtu wa Usalama?

SHAHIDI: Ni mtu binafsi.

KIBATALA: Lakini hujamwambia Mheshimiwa Jaji kuwa gari hilo ni teksi au mali ya mtu binafsi.

SHAHIDI: Nitamwambiaje Jaji kuhusu masuala yangu binafsi?

KIBATALA: Kwani hujaambiwa kuwa hapa kwenye ushahidi kila kitu ni hadharani? Labda iwe Jaji kaona linavunja haki zako.

SHAHIDI: Nafahamu.

KIBATALA: Shahidi unafahamu kwamba viongozi wote wa Serikali wamehamia Dodoma kutoka angalau mwaka 2018?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Unafahamu kwamba ofisi za DCI, IGP, CDF wote wamehamia Dodoma?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Je, ulimwambia Mheshimiwa Jaji kwamba DCI alikuambia yupo Dar es Salaam kikazi mnaweza kuonana?

SHAHIDI: Sijazungumzia.

KIBATALA: Unafahamu kwamba DCI kahamia Dodoma na shughuli zote za Ofisi ya DCI zinafanyika Dodoma?

SHAHIDI: Siwezi kuzungumzia kuhusu Ofisi ya DCI.

KIBATALA: Aliyeleta masuala ya kufika Ofisi ya DCI?

SHAHIDI: Ni mimi.

KIBATALA: Shahidi unafahamu kuhusu neno “CIMIC”?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Unajua kirefu chake?

SHAHIDI: Sijui. Ila najua maana yake ni nini.

KIBATALA: Nikisema Kwamba ni Civic and Military Coordination utakubali au utakataa?

SHAHIDI: Siwezi kukubali au kukataa.

KIBATALA: Nikisema maana yake ni taratibu za Jeshi Kuratibu Mahusiano na Raia au taasisi zingine za kijeshi?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Kwa Tanzania ipo hiyo CIMIC?

SHAHIDI: Haipo. Ipo katika Active Operation kama nchi zenye vita.

KIBATALA: Kwa maana yake Tanzania hakuna utaratibu wa Jeshi kushea taarifa na Jeshi kama la Polisi?

SHAHIDI: Utaratibu huo upo.

KIBATALA: Kwa maana hiyo CIMIC ipo?

SHAHIDI: Ndiyo ipo.

KIBATALA: Kwa maana hiyo Jeshi wanaweza kumkamata mtu na bangi kisha Jeshi likaona ni suala la Polisi, wakampeleka Polisi?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Hata kama si kazi ya Jeshi kuchunguza ugaidi, chini ya mwamvuli wa CIMIC Jeshi si wanaweza kumkamata na kumpeleka Polisi?

SHAHIDI: Hapo unampeleka Polisi.

KIBATALA: Na kinyume chake taasisi za kiraia zinaweza kuona mtu kwa taarifa zake wanaweza kumkabidhi kwa Jeshi kwa tuhuma zake?

SHAHIDI: Hakuna kitu kama hicho.

KIBATALA: Kwani coordination maana yake nini under CIMIC?

SHAHIDI: Mahusiano lwa ajili ya kubadilishana taarifa.

KIBATALA: Unafahamu kuhusu Presence Patrols?

SHAHIDI: Ndiyo. Nafahamu.

SHAHIDI: Lakini haifanyiki mara kwa mara.

KIBATALA: Hata kama mara tatu au mbili, Jeshi linafanya au halifanyi?

SHAHIDI: Linafanya.

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji, majuzi ulitoa uamuzi mdogo kuhusu taarifa za kijeshi. Naomba Wakili Peter Kibatala azuiwe asijadili taarifa za Operation za Kijeshi, maana anakoenda si pazuri.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji, wakati uamuzi unatolewa nilikuwapo na nilisikia. Sijauliza kuhusu vifaru vingapi wala silaha ni ngapi.

KIBATALA: Labda hajui kuhusu Presence Control. Presence Control maana yake ni kwamba Jeshi linachukua askari wake wanapita mtaani. Iwe kwa sababu za kiusalama kwa sababu ya taharuki. Labda hata wanasiasa wakitoa matamko Jeshi wakati fulani hata Tanzania lilipitisha wanajeshi na magari mtaani baada ya tamko la maandamano. Lakini Mheshimiwa Jaji ukisema niache nitaacha.

JAJI: Basi kuhusu frequently msifike, kama idadi ya mara ngapi.

KIBATALA: Sawa Mheshimiwa Jaji.

KIBATALA: Shahidi, ni sahihi Presence Patrols inafanyila kuonyesha maadui kuwa Jeshi lipo?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Ni sahihi katika Tanzania kumefanyika Presence Patrols?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Je, kunapotokea tishio la ugaidi, Jeshi linahusika au halihusiki?

SHAHIDI: Kuna level of protocols. Mpaka wanaohusika wa- declare kuwa Jeshi lije kuongeza nguvu.

KIBATALA: Shahidi unafahamu Jeshini kuna kitu kinaitwa kwa jina la utani ‘Office Number 10’?

SHAHIDI: Nafahamu.

KIBATALA: Na kila kikosi au kambi ya Jeshi ina intelligence office?

SHAHIDI: Nafahamu.

KIBATALA: Na kazi yake ku- deal na masuala mtambuka?

SHAHIDI: Ipo specific siyo masuala yote mtambuka.

KIBATALA: Shahidi, kuna sehemu umetaja spray ya sumu au powder ya sumu.

SHAHIDI: Sikusema.

KIBATALA: Hukusema kwa sababu Bwire hakukuambia kuhusu spray ya sumu au powder ya sumu?

SHAHIDI: Mheshimiwa Jaji mbona ananiwekea majibu mdomoni?

KIBATALA: Jibu swali langu.

SHAHIDI: Sijazungumzia kuhusu spray ya sumu au powder ya sumu.

KIBATALA: Unamfahamu Tundu Lissu?

SHAHIDI: Ndiyo. Namfahamu.

KIBATALA: Je, unafahamu kwamba Khalfani Bwire na wenzake walihusika kumlinda Tundu Lissu wakati anawasili Tanzania?

SHAHIDI: Rais mwenyewe halindwi na komando.

KIBATALA: wewe jibu swali langu.

SHAHIDI: Sifahamu kama walimlimda.

KIBATALA: Shahidi unafahamu kwamba moja ya jukumu ulilowaitia lilikuwa kumlinda Tundu Lissu?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Unafahamu kwamba Tundu Lissu kwa madhila aliyopata alikuwa anataka ulinzi wa hali ya juu?

SHAHIDI: Najua kazi ya ulinzi kwa mgombea ni kazi ya Polisi.

KIBATALA: Kwani wewe unajua kuwa mgombea analindwa na polisi wangapi?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Wewe uliongea na Polisi kuhusu walinzi wa wagombea?

SHAHIDI: Sijawahi.

KIBATALA: Ulishawahi kumlinda mgombea wa urais?

SHAHIDI: Sijawahi.

KIBATALA: Ulishawahi kumlinda hata katibu kata?

SHAHIDI: Sijawahi.

KIBATALA: Je, unafahamu kwamba Jeshi la Polisi pamoja na kulinda raia, lakini Lissu alipigwa risasi zaidi ya 30?

SHAHIDI: Nafahamu.

KIBATALA: Unafahamu kwamba mpaka leo Jeshi la Polisi hawajamkamata mtu hata mmoja mpaka leo?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Unafahamu kwamba Freeman Mbowe alikuwa na mlinzi wake anaitwa Allan Bujo na hapa Mahakamani yupo?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Unafahamu mtu anaitwa Ben Saa Nane?

SHAHIDI: Simfahamu.

KIBATALA: Unafahamu kwamba Mbowe, homeboy wako, msaidizi wake Ben Saa Nane kapotea mpaka leo hajulikani alipo?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Je, mpaka hapo huoni kwamba mtu alikuwa anahitaji walinzi?

SHAHIDI: Suala la walinzi ni suala la mtu binafsi.

KIBATALA: Je, kwa wewe kuwasiliana na Freeman Mbowe, jeshi lingefahamu au wakubwa zako au Office Number 10. Je, wangejua unawasiliana na Freeman Mbowe kiongozi wa upinzani limekuwa kosa au si kosa?

SHAHIDI: Siyo kosa.

KIBATALA: Je, kwa ufahamu wako wewe mwanajeshi na afisa wa Jeshi, kanuni, miongozo na sera, je, afisa wa Jeshi anaruhusiwa kuwa na mahusiano ya moja kwa moja na kiongozi wa kisiasa?

SHAHIDI: Personal anaruhusiwa.

KIBATALA: Kisiasa je?

SHAHIDI: Harusiwi.

KIBATALA: Je, kwa afisa wa Jeshi kama wewe kwenda kumtafutia kiongozi wa upinzani walinzi, inaruhusiwa kijeshi?

SHAHIDI: Haikuwa kwa bahati mbaya ndiyo maana mpaka leo sijashitakiwa.

KIBATALA: Nani anaamua kuwa hili ni kosa la kinidhamu au si kosa la kinidhamu?

SHAHIDI: Ni mimi mwenyewe.

KIBATALA: Unafahamu au hukufamu kwamba hawa walinzi, mojawapo ya majukumu waliokuwa wanayafanya kama walinzi wa Mbowe na Chadema ikiwamo katika vikao vya ndani vya Chadema?

SHAHIDI: Sifahamu. Mie najua Mbowe aliwashawishi kwenda kumdhuru Sabaya Moshi baada ya hapo waje kulipua vituo vya mafuta Dar es Salaam.

KIBATALA: Unafahamu au hufahamu kwamba Adamoo na Ling’wenya walipoenda Moshi walipokelewa na gari yenye charter na bendera ya Chadema?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Je. unafahamu kwamba Siku wanakuja kumpokea Lissu walikuja kutoka Moshi kwa kusafiri na gari ya Chadema?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Je, uliwauliza?

SHAHIDI: Siwezi kuwauliza kila saa watashtuka.

KIBATALA: Nimekuuliza kuhusu tarehe 26, kabla hamjakata mawasiliano, je, ulikuwa unawa- monitor kwa details kama hizo?

SHAHIDI: Ndiyo maana Khalfani Bwire ali- confess kwangu kuwa wamekengeuka.

KIBATALA: Adamoo ali- confess kwako?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: Ling’wenya ali- confess kwako?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: Shahidi unafahamu maana ya Dimina?

SHAHIDI: Nafahamu.

KIBATALA: Unajua kuwa moja yake ni kama hiyo ya kuulizwa kingine na kujifanya hujaelewa?

SHAHIDI: Nimesema kwamba niliwauliza.

KIBATALA: Walikuambia nini?

SHAHIDI: Waliniambia kuwa walikuwa wanasubiri kuajiriwa.

KIBATALA: Siku wanakuambia wanasubiri kuajiriwa ilikuwa tarehe ngapi?

SHAHIDI: Siwezi kukumbuka.

KIBATALA: Nilisikia kwamba Mbowe alikuambia atashiriki uchaguzi.

SHAHIDI: Hakuniambia kuhusu uchaguzi. Aliniambia kuwa wamepanga kuchukua dola kwa namna yoyote.

KIBATALA: Kwa hiyo hapa Mahakamani hakuna maneno kwamba katika uchunguzi huu, chama chake kimejipanga kuchukua dola kwa namna yoyote?

SHAHIDI: Yapo.

KIBATALA: Sasa mbona unakataa.

KIBATALA: Je, unafahamu kwamba yeye mwenyewe Freeman Mbowe alishiriki uchaguzi jimboni kwake?

SHAHIDI: Nafahamu.

KIBATALA: Na Freeman Mbowe alisema kwamba “Chama changu kimepanga kuchukua dola” siyo “Mimi Freeman Mbowe nimepanga kuchukua dola”?

SHAHIDI: Alisema chama changu kimepanga kuchukua dola.

KIBATALA: Unafahamu kwamba Chadema ilikuwa na wagombea ubunge nchi nzima?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Unafahamu kwamba Chadema ilikuwa na mgombea urais?

SHAHIDI: Nafahamu.

KIBATALA: Je, kwamba mgombea urais kuzunguka nchi nzima kufanya kampeni?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Kwa kuwa wewe ulikuwa na mawasiliano nao kama sehemu ya kuwa- monitor, je, unafahamu kwamba moja ya majukumu yao ilikuwa kulinda makao makuu ya Chadema, Mtaa wa Ufipa?

SHAHIDI: Sikuwahi kufahamu.

KIBATALA: Freeman Mbowe katika ushahidi wako aliwahi kukuambia katika mpango huo kuna kiongozi yeyote wa Chadema ambaye anahusika au kushiriki?

SHAHIDI: Hakuwahi kuniambia.

KIBATALA: Je, unafahamu kuwa zile pesa zilikuwa ni za Freeman Mbowe binafsi au za chama ambazo zilitoka kwa kufuata utaratibu wote?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Unafahamu kwamba suala la kutafuta walinzi lilikuwa maamuzi ya Chama?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Unafahamu kwamba Freeman Mbowe hawezi kuleta walinzi mpaka Makao Makuu waje kulinda bila idhini ya Chama?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Shahidi unafahamu kwamba hawa walinzi waliajiriwa Katokana na mapendekezo ya Kurugenzi ya Ulinzi na Usalama ya Chadema?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Unafahamu kwamba hata wanamuziki kama Diamond au wacheza mpira wana ma- body guards?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Hivi mtu akiwa discharged Jeshini kuna zuio la kufanya kazi nyingine?

SHAHIDI: Hakuna. La msingi afuate sheria.

KIBATALA: Hata kunywa bia lazima ufuate sheria, ndiyo maana inatakiwa uwe above 18.

KIBATALA: Je, kiongozi wako wa kambi ulimwambia kwamba wewe uliwa- recruit hawa walinzi?

SHAHIDI: Ndiyo nilimwambia.

KIBATALA: Kwa hiyo ofisi inafahamu wewe uliwa- recruit hawa?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Ilikuwa ofisini au nyumbani?

SHAHIDI: Ilikuwa ofisini.

KIBATALA: Kwa hiyo tukiomba taarifa hiyo katika ofisi tutapata?

SHAHIDI: Siwezi kujua.

KIBATALA: Katika Hati ya Mashitaka, hapa kwanini uliamua kuwa mkutane Morogoro?

SHAHIDI: Kwa sababu ndiyo centre.

KIBATALA: Je, ulisema lolote kuhusu kufanya kikao Mwanza?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: Kuhusu Mwanza?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: Kuhusu Arusha?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: Wakati unatoa taarifa ulimwambia kuwa matukio yalitokea tarehe ngapi kati ya wewe na Mbowe?

SHAHIDI: Kati ya tarehe 1 Julai mpaka tarehe 10.

KIBATALA: Sasa kwenye Hati ya Mashitaka wenzetu wameandika tarehe 1 Mei. Hujamwambia wewe?

SHAHIDI: Sijasema hivyo mimi.

KIBATALA: Unafahamu kwamba Aishi Protea Machame Hotel wakati huo ilikuwa tayari imeshakodishwa?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Uliwahi kufahamu kama Mbowe aliwahi kusafiri nje ya nchi baada ya kukuambia taarifa hizo?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Unamfahamu Godbless Lema?

SHAHIDI: Ndiyo. Namfahamu.

KIBATALA: Unafahamu kwamba yupo uhamishoni?

SHAHIDI: Sina taarifa.

KIBATALA: Unafahamu Lissu anaishi uhamishoni?

SHAHIDI: Sijui kama uhamishoni au kaenda kutalii.

KIBATALA: Unafahamu kwamba kama hawa vijana watatu wasingekamatwa, Lissu angebakia nchini? Kanyang’anywa walinzi wake, na wapo mahakamani wanashitakiwa?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Unafahamu kwamba hata Godbless Lema kukimbilia uhamishoni ni kwa sababu kijana mmoja hapa alikuwa amepangiwa kumlinda Godbless Lema?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji naomba kuishia hapa kwa shahidi huyu. Asante sana.

Shahidi anahema sana. Ameshusha pumzi.

WAKILI WA SERIKALI: (Abdallah Chavula) Mheshimiwa Jaji nina maswali machache sana.

WAKILI WA SERIKALI: Shahidi umeulizwa hapa kuhusu mtu kuwa na ambao ni specialized walinzi ukasema ni suala lake binafsi. Ulikuwa unamaanisha nini?

SHAHIDI: Kuna makampuni mengi binafsi yanatoa huduma, ila kimsingi suala la ulinzi wa Watanzania lipo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani.

WAKILI WA SERIKALI: Uliulizwa swali kuhusiana kama Jeshi lingejua kuwa una mahusiano na Freeman Mbowe, ukasema hakuna tatizo.

SHAHIDI: Ndiyo. Kwa sababu hakuna mtu anazuiwa kuwa na mahusiano na mtu mwingine, kama ni personal.

WAKILI WA SERIKALI: Eleza taratibu.

SHAHIDI: Kufahamiana na mtu si kosa kama tu mwanasiasa akijiingiza katika siasa zake ndiyo kosa.

WAKILI WA SERIKALI: Umeulizwa hapa kama wewe ni mtu muhimu au siyo mtu muhimu.

KIBATALA: Objection. Hakuna mtu aliulizwa swali hilo. Shahidi ali- volunteer mwenyewe.

WAKILI WA SERIKALI: Sawa shahidi. Kwanini unasema wewe si mtu muhimu?

SHAHIDI: Hakuna Mtanzania muhimu kuliko mwingine.

WAKILI WA SERIKALI: Vile Vile jana ulipewa kisa kimoja cha kwenye Biblia kuhusu Daniel, halafu mwisho wa siku ukaambiwa kisa cha Daniel na akina Ling’wenya ukasema ni tofauti. Fafanua.

SHAHIDI: Kwa Daniel zilitungwa sheria kwa sababu alikuwa anaabudu mara tatu. Wakili anataka kufananiisha na suala la akina Bwire. Hawa ni watu wazima, ndiyo maana wali- confess kwa kutaka kumdhuru Sabaya na kuja kulipua kituo cha mafuta.

WAKILI WA SERIKALI: Na uliulizwa masuala kuhusiana na mzazi wake Ling’wenya, baada ya kukupigia wewe, wewe ukasema mpigie bosi wake. Fafanua.

SHAHIDI: Ni kweli mzazi wake alinipigia. Ni kweli nilimwambia kwamba mpigie bosi wao kama akimkosa Bwire.

KIBATALA: Objection! Suala la kupigiwa Bwire ni jipya.

WAKILI WA SERIKALI: Shahidi suala la kumpigia bosi wake ulikuwa unamaanisha nini?

SHAHIDI: Ampigie Freeman Mbowe ndiyo bosi wake kama kuna jambo limempata yeye ndiyo anajua.

WAKILI WA SERIKALI: Suala la kwamba simu siyo salama, niwezeshe nikutane nao. Fafanua.

SHAHIDI: Kukutana pamoja na kuongea pamoja ni sahihi zaidi. Simu si salama ndiyo maana nikaomba aniwezeshe.

WAKILI WA SERIKALI: Kingine ni suala la meseji saa 2:24 siku ya tarehe 22 Julai 2020, kwamba atumie namba za wasaidizi wake au wakala,

SHAHIDI: Nilikuwa nakwepa kuonekana namtega, nikataka kujenga uaminifu. Mbowe aliniambia simu siyo sahihi.

Wakili Dickson Matata: Objection! Hakuna maeneo ambayo Mbowe alisema kuwa simu siyo sahihi. Atoe hayo maneno.

JAJI: Wakili Peter Kibatala tusaidie hilo. Nakumbuka aliulizwa swali kuhusu hilo.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji naomba shahidi ajibu swali kwanza.

JAJI: ameshajibu.

KIBATALA: Kwa ruhusa yako…

JAJI: Amejibu kuwa alikuambia kuwa atumie simu ya wasaidizi wake au wakala kwa lengo la ku- win trust.

KIBATALA: Sawa. Tumuache aendelee.

WAKILI WA SERIKALI: Kuna lingine kwenye SMS hapa ya tarehe 22 Julai 2020, seseji ya saa 12 :27 ulinukuliwa hapa ukisema kwamba ikiwezekana uwe unanitumia fedha ya kuwa- mobilise. Ulimaanisha nini?

SHAHIDI: Nilikuwa namaanisha kwamba anitumie pesa ya kuwa- mobilise huko walipo, niwafanyie vetting kwa ajili ya kuja kufanya jukumu lao.

WAKILI WA SERIKALI: Kuna suala umeulizwa hapo kuhusiana na fedha, kama ulitumiwa kuwa siyo za kigaidi au ugaidi na wewe ukaafiki siyo kwa ajili ya ugaidi.

SHAHIDI: Nilikuwa namaanisha kwamba pesa zilitumwa kwa malengo ya ugaidi, ila wapokeaji walikuwa hawajui kuwa walikuwa wanapokea kwa ajili ya matukio ya ugaidi.

WAKILI WA SERIKALI: Uliulizwa hapa, ukasema hukushangaa kusikia Khalfani Bwire amekamatwa. Ulikuwa unamaanisha nini?

SHAHIDI: Kwa sababu niliwaambia kuwa mnaenda kufanya kazi ila matukio ya uhalifu mniambie, Wao wakanyamaza kimya. Baada ya hapo Khalfani Bwire akaniambia “Bro, nimekengeuka kwamba wale madogo wapo ground. Ndiyo maana sikushangaa kwa sababu taarifa alinipa too late ikiwa wameshaingia kwenye uhalifu.

WAKILI WA SERIKALI: Kuna swali moja umeulizwa kuhusu kujitambulisha kwako ukamwambia huna cheo, lakini ukasema kwamba ulikuwa sahihi japo ulisema uongo.

SHAHIDI: Nisingeweza kukutana na mtu siku ya kwanza halafu nimpe details zangu zote.

SHAHIDI: Ni suala la kiusalama.

WAKILI WA SERIKALI: Umeulizwa tena suala lingine hapa kwamba wale watu (washtakiwa) waende wakafanye kazi ya ulinzi waambatane naye kuchukua dola. Ulikuwa unamaanisha nini?

SHAHIDI: Nilikuwa namaanisha kwamba Freeman Mbowe alikuwa anatafuta watu kwa ajili ya kuuchua dola. Katika kuchukua dola huko alikuwa anataka experts katika kuchukua dola huko kwa ajili ya kukata miti na kulipua vituo vya mafuta.

WAKILI WA SERIKALI: Ulionyeshwa hapa maelezo ambayo uliyaandika ukiwa Polisi. Kuna maeneo ambayo katika maelezo umezungumza kifupi ila hapa umezungumza kirefu. Kwanini imetokea hivyo?

SHAHIDI: Kwa sababu aliyekuwa anaandika siyo maneno yote alikuwa anaandika. Hapa naongea kwa sababu nipo free. Kwa hiyo siyo maneno yote kaandika mle.

(Maswali yamesimama. Mawakili wa Serikali wanateta chini chini. Wanamwomba jana “samahani kidogo” wakimwomba asubiri. Jaji anawatazama).

WAKILI WA SERIKALI: (Abdallah Chavula) Mheshimiwa Jaji, sisi hatuna maswali sana. Nafikiri yanatosha.

JAJI: Shahidi tunakushukuru kwa ushahidi wako.

(Shahidi anatoka kwenda kukaa kwenye benchi walilokaa mawakili wa Serikali).

JAJI: Jamhuri?

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji, huyo ndiye shahidi tuliyekuwa naye kwa leo na hatuna shahidi mwingine. Hivyo tunaomba ahirisho la siku mbili (2) kwa maana ya tarehe 2 na tarehe 3 ili tuweze kuendelea Ijumaa tarehe 4.

WAKILI WA SERIKALI: (Ijumaa tarehe 4) ndipo tutakuwa tume- procure shahidi mwingine, kwa sababu shahidi ambaye tulipanga baada ya shahidi huyu hakuwezi kufika Kwa sababu zilizo nje ya uwezo wetu. Hivyo katika mazingira hayo na ili kupata uhakika wa kuendelea Ijumaa, tunaomba ahirisho ili hata kama tukishindwa tuweze kupata shahidi mwingine. Ni hayo tu Mheshimiwa Jaji.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji, sisi kwa kweli bila kuwakosea wenzetu hatuoni sababu ya ahirisho.

KIBATALA: Kwenye Committal Bundle wameorodhesha mashahidi wengi sana. Inawezekana vipi kukosa mashahidi? Kama nilivyosema mwanzo, kwamba wateja wetu wana haki ya kkujua hatima yao. Tunatamani kesi iendelea. Tunapinga kuahirisha kesi. Tunaomba Mahakama iwaelekeze walete mashahidi ukizingatia wengine adress zao ni Dar es Salaam.

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji, tumesikia hoja ya kupinga ahirisho kutoka kwa wenzetu, ila tunaona kwamba wamekuwa too emotional kuliko kuleta hoja za kisheria. Kuita mashahidi kuna masuala mengi sana. Si jambo rahisi na mengine hatuwezi kuyasema hapa. Ukiangalia shahidi huyu ameanza kuwa cross examined kuanzia Alhamisi.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji, hii ni rejoinder au hoja mpya. Ajibu hoja zetu.

JAJI: Nisaidie kujibu hoja ya siku mbili. Wao wanasema kwamba waje kesho. Je tu- assume mpaka kesho kutwa huwezi kupata shahidi?

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji, naweza kusema Alhamisi tukaja kupoteza resources hapa. Mheshimiwa Jaji naomba hata kama kuna alternative iwe Ijumaa basi.

(Jaji anaandika anaandika na mahakama iko kimya).

(Bado kimya kimetawala mahakamani).

JAJI: Katika kutolea uamuzi wa hoja ya ahirisho, kuhusu kuhairisha mpaka tarehe 4, nafahamu kwamba ipo sheria inayowabana upande wa mashitaka katika kuleta mashahidi. Lakini upande wa mashitaka wametoa hoja ambayo inawalazimu kuleta mashahidi tarehe 4. Upande wa utetezi hoja yao ni kuwa shauri lipo katika Mode ya Speed Trial, na kwamba ni shauri ambalo linatakiwa kuisha haraka. Lakini Mahakama inaona ni busara hata kama ikilizamisha mama mashahidi hawapo Mahakama haitaweza kuendelea. Kwa sababu hiyo naahirisha Mahakama mpaka Ijumaa tarehe 4 Februari 2022. Washitakiwa wataendelea kuwa rumande chini ya Magereza mpaka hiyo Ijumaa.

Jaji anaondoka katika chumba cha mahakama.

Like
2