Tanzania yachafuliwa Gambia kwa tuhuma za maji yenye sumu

WANANCHI wa Gambia wameingiwa na hofu juu ya usalama wa maisha yao baada ya taarifa kusambaa kwamba maji ya chupa ya kunywa yanayodaiwa kutengenezwa Tanzania, yana sumu – na kwamba maji hayo yanayozalishwa Jiji la Dar es Salaam, tayari yameua watu 180 nchini Tanzania.

Hofu juu ya maji hayo ya chupa, yanayoitwa DEW, imesambaa kupitia mitandao ya kijamii nchini humo, hasa Facebook na Instargram.

Ujumbe unaosambaa umebeba maneno haya; “Tafadhali usinunue na kunywa maji yanayoitwa DEW ambayo yameingizwa Gambia kutoka Tanzania. Maji hayo ya chupa, tayari yameua watu 180. Sambaza ujumbe huu uokoe wengine.”

Jana SAUTI KUBWA ilipokea maswali mengi kutoka kwa baadhi ya waandishi wa habari wa Gambia ambao walitaka kujua ukweli wa jambo hili.

Mmoja wa waandishi hao, Dijah Jawo, anayefanya kazi jijini Banjul, aliliza iwapo maji hayo kweli yameua watu 180 nchini Tanzania na endapo ni kweli yanatengenezwa Tanzania.

Hata hivyo, SAUTI KUBWA imegundua kwamba katika orodha ya bidhaa za maji ya chupa yanayozalishwa Tanzania, hakuna maji yenye jina hilo – DEW.

Uchunguzi wetu umebaini kuwepo kwa  maji ya chupa yanayozalishwa Dar es Salaam na Rukwa yenye jina la DEW DROP na si DEW kama inayotajwa na mitandao ya kijamii ya Gambia.

Maji ya chupa ya DEW DROP yanazalishwa Dar es Salaam na kampuni ya Dew Drop Drinks Company Limited na yamepewa nambari ya ubora “TZS 574/EAS/153” inayotolewa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Maji mengine ya DEW DROP huzalishwa  nje ya Mji wa Sumbawanga, Rukwa, na yamepewa leseni ya ubora na TBS yenye  nambari “574:2008.”

TBS pia imethibitisha kwamba haijawahi kupokea maombi ya kuchunguza ubora wa maji ya chupa ya DEW.

Pamoja na kwamba nia ya kusambaa kwa ujumbe huu bado haijulikani, jambo hili linahusishwa na ushindani wa biashara ya maji na uchunguzi zaidi uliofanywa na SAUTI KUBWA unaonyesha kwamba mtu wa kwanza kusambaza ujumbe unaohusu maji ya DEW alikuwa jijini Lagos, Nigeria mwaka 2011, na alitumia simu aina ya BlackBerry.

Mtu huyo alituma ujumbe sawa na huo unaoichafua Tanzania, akitumia maneno yaleyale, isipokuwa akabadili jina la nchi, akiandika Nigeria.

Like