Magufuli atumia uwanja wa ndege Chato “kupiga dili”

RAIS John Magufuli amekamatika. Sababu za yeye kutopenda kukosolewa, na bidii yake kudhibiti vyombo vya habari, wanaharakati, na wapinzani hata kwa kumwaga damu, zimeanza kujulikana. Anaogopa wapinzani na vyombo vya habari wasiibue ufisadi wake au wa rafiki zake.

Katika siku za hivi karibuni, mbali na “upotevu” wa Sh. 1.5 trilioni ambazo mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) amesema hakuona zilipo, huku serikali ikijitahidi kufunika sakata hili kwa maelezo yasiyoeleweka, na bila mafanikio, kuna wizi mwingine wa kimfumo unaohusisha Rais Magufuli na watu wake wa karibu.

Rais Magufuli anatajwa katika dili la uwanja wa ndege wa Chato, ambao ulipangiwa kujengwa kwa Sh. 39 bilioni, lakini hadi sasa umetumia Sh. 50 bilioni – kwa mujibu wa randama ya wiizara ya ujenzi kwa Bunge Machi 2018. Fedha hizo zimetumika bila idhini ya bunge. Wanaojua kinachondelea wanasema fedha hizo nazo “zimepigwa.” Wanachosikitikia ni kwamba rais anajua na anahusika, hata kama mkono wake hauonekani moja kwa moja.

Kampuni iliyopewa zabuni ya kujenga uwanja huo, Mayanga Construction Co. Ltd, inasimamiwa na Steven Makigo, mmoja wa maswahiba wakubwa wa Rais Magufuli. Urafiki wa Makigo na Magufuli ulianzia  katika Shule ya Sekondari Lake, ya Mwanza, tangu miaka ya sabini. Makigo alisomea pale 1975-1978, wakati Magufuli alisomea pale 1977-78. Makigo ni mhandisi aliyehitimu shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na Magufuli ni mwalimu wa kemia, hisabati na elimu, mhitimu wa chuo hicho.

Makigo ndiye anaonekana, katika video fupi (hapo chini) ya watu watatu iliyosambaa mitandaoni, akimshauri Magufuli agombee urais; na Magufuli akimjibu, “nikigombea, watalimia meno.” Mtu wa tatu katika video hiyo ni Charles Kitwanga, swahiba mwingine wa Magufuli ambaye ni mbunge wa Misungwi, Mwanza. Makigo ndiye alikuwa mshika fedha za kampeni za urais wa Magufuli mwaka 2015. Taarifa zinasema Makigo na Magufuli wawili hao ndio wamiliki halisi wa kampuni hiyo, ingawa mmoja amemtanguliza mwenzake kwa sababu za kisiasa.


Makigo amekuwa mkurugenzi mtendaji wa Mayanga Construction Co. Ltd, iliyosajiliwa mara ya kwanza kama kampuni ya “CIVIL” mwaka mwaka 2007, ikapewa namba ya usajili C1/0056/12/2007; halafu ikasajiliwa tena mwaka 2016 kwa namba ya usajili B1/154/04/2016 ikiwa kampuni aina ya “BUILDING.”

Mwaka 2012 Kampuni ya Mayanga iliungana na kampuni nyingine 12 za wazalendo kuunda Mbutu Bridge Joint Venture kwa ajili ya kutengeneza daraja la Mbutu, Igunga, lenye urefu wa mita 46.1. Ilizinduliwa na Rais Jakaya Kikwete, Januari 2013. Mradi huo uligharimu Sh.12.34 bilioni. Shabaha ya kuunda kampuni hiyo ilikuwa kuwezesha kampuni za wazawa kupewa zabuni za miradi minono ambayo imekuwa inachukuliwa na wageni, hasa Wachina, kwa sababu ya uwezo mdogo wa kampuni moja moja za kitanzania. Kampuni ya Makigo ndiyo ilikuwa kampuni kiongozi katika mradi huo.

Hata hivyo, kashfa za kampuni hiyo zimeibuka baada ya kampuni kupendelewa na kupewa mradi mnono wa kujenga uwanja wa ndege wa Chato, huku haina sifa wala uzoefu wowote. Katika kuonyesha kuwa serikali ililenga kuipa fedha kampuni hiyo, tangazo la zabuni namba AE-027/2016-2017/CHT/w/07 ya ujenzi wa uwanja huo lilisisitiza kuwa lazima kampuni inayoomba iwe inatoka katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara, Geita, Kagera, na Simiyu.

Wakandarasi wengine walilalamika kuwa sharti hilo lililenga kuwatenga ili kuipa zabuni “kampuni ya rais” ambayo inaendeshwa kwa mgongo wa rafiki yake. Hata hivyo, licha ya kampui hiyo kupewa zabuni hiyo, kampuni yenyewe haijawahi kujenga uwanja wa ndege popote duniani, jambo ambalo limeongeza wasiwasi juu ya vigezo vilivyotumika kuipa zabuni.

Zaidi ya hayo, inatuhumiwa kwa “upiga dili” na kushindwa kazi katika miradi mingine midogo iliyowahi kupewa. Miongoni mwa tuhuma za awali ni zile zilizotajwa na wabunge kadhaa wakiwemo Zitto Kabwe, John Heche na Marwa Chacha Marwa wa Serengeti katika mjadala makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano mwaka 2016/2017. Alisema:

“Mheshimiwa Mwenyekiti, …sasa naomba niseme kuhusu barabara ya Makutano – Nata – Mugumu – Loliondo – Mto wa Mbu. Aliyeanza kuwa na maono ya kujenga barabara hii ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wakati huo ikiitwa Makutano – Nata – Ikoma Gate. Mheshimiwa Mwenyekiti, baadaye alipokuja Mheshimiwa Benjamin William Mkapa ndipo wakaanza kuiweka kwenye Ilani ya CCM. Mkapa akaondoka, katika miaka yake kumi hakujenga barabara hii. Akaja Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ikawekwa kwenye Ilani ya CCM, wakati huo Mheshimiwa John Pombe Magufuli akiwa ndiye Waziri wa Wizara ya Ujenzi. Ikapita miaka kumi wala hakuna chochote kilichofanyika. Sasa amekuja ambaye alikuwa Waziri wa wizara hiyo, Mheshimiwa John Pombe Magufuli.

 

“Mheshimiwa Mwenyekiti, ni aibu sana, barabara hii mwaka 2013 ilitengewa fedha kwenye bajeti ili ianze kujengwa na mwezi wa tatu mwaka 2013 ujenzi wa barabara ukaanza, ambapo wakandarasi wa ndani ndio waliokuwa awarded tender ya kujenga barabara hii. Na bahati nzuri mmoja wa wakandarasi anaitwa Steven Makigo, rafiki yake sana Magufuli, akapewa kazi ya kujenga barabara hii. Yeye na wenzake contractors kumi, tangu mwaka 2013 mwezi wa tatu mpaka leo ninavyoongea wamepewa shilingi bilioni 14 hawajajenga hata mita moja ya lami. (Makofi)

 

“Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia; waliopewa kujenga barabara hii ya lami, Makutano – Nata – Mto wa Mbu ni contractors wa ndani wakiongozwa na Kampuni ya Mayanga ambayo Mkurugenzi wake ni huyu Steven Makigo, wako contractors kumi. Wakaisajili kwa jina moja wanasema Mbutu Bridge Contractors; ni wa kwetu ni wazawa. Tangu 2013 wamepewa shilingi bilioni 14 hata mita moja ya lami hakuna halafu mnasema hapa kazi tu, hapa kazi kwa issue gani? Kama mmewapa bilioni 14 wameshindwa wanyanganyeni, watumbueni majipu wale, anzeni na huyu mkandarasi, yaani hakuna chochote anachofanya lakini mnampa mahela tu.

 

“Mheshimiwa Mwenyekiti, siku moja nimeuliza swali hapa Mheshimiwa Waziri hakulijibu na hiyo wamepewa kujenga 50 kilometers kuanzia Makutano mpaka Sanzate. Sasa hivi ninavyoongea mkataba wa kujenga barabara ile uliisha mwaka 2015 mwezi wa tano, baadaye wakaomba extension wakaongezewa mpaka Machi 2016, hivi huu ni mwezi gani? Mpaka leo bado hawajajenga hata mita moja, bado tunaendelea ku-entertain watu wa namna hii, si afadhali mtuwekee pale Mchina ajenge ile barabara ikamilike haraka.

 

“Mheshimiwa Mwenyekiti, ni aibu, kama watu wamepewa shilingi bilioni 14 hata mita moja ya lami hawajajenga halafu unaniambia nisiongee, I have to talk. Nimeletwa hapa kama Mbunge wa Jimbo la Serengeti niongee kwa niaba ya wananchi wa Serengeti. Tunachokiongea hapa si mambo ya chama, hata kama ingelikuwa kwako wewe wametumia shilingi bilioni 14 hawajajenga kilometa moja ya lami utasikia vizuri, au huyo malaika akiguswa mnasikiaje? Tulia. (Makofi)

 

“Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni yenyewe sasa hivi wanajenga daraja la Mto Kiarano, hata structural engineer hawana, material engineer hayupo! Hivi hii Wizara ikoje hii? 

Na kama kweli Rais, Mheshimiwa John Pombe Magufuli anaipenda nchi hii, anawapenda wananchi wa Mkoa wa Mara, anawapenda wananchi wa Serengeti, aanze ku-deal na huyu mkandarasi. Kama mtu anaweza kutumia shilingi bilioni 14 halafu hakuna chochote alichofanya halafu watu wanaona sawa tu eti usimguse nitakugusa tu. (Makofi)”

Heche, mbunge wa Tarime Vijijini, katika ukurasa wake wa Twitter, tarehe 10 Novemba 2017, aliandika:

“Uwanja wa ndege wa Chato unajengwa kwa billion 41 haukua kwenye mpango wala bajeti ya mwaka huu!!Nini faida za kiuchumi kujenga uwanja mkubwa wenye runway ya 3km na upana 43m Chato? Je, uwanja huu ni muhimu kwa taifa kwasasa kiasi hicho? Sheria ya bajeti inavunjwa na serikali!!”

Ukubwa halisi wa uwanja huo, kwa mujibu wa zabuni hiyo, ni urefu wa mita 3000 (km3), na upana wa mita 45.

Zitto naye, tarehe 11, Novemba 2017, alijadili suala hilo katika ukurasa wake wa Twitter, akichangia hoja ya Heche, akaandika:

“Hii ni hoja ya kuundia Kamati Teule ya Bunge kwani ina viashiria vya upendeleo kinyume na Katiba na pia mkandarasi wa uwanja huu, hiki ni kiwanja chake cha kwanza kujenga na ana mahusiano ya karibu sana na Rais. John hebu lishike hili kwa kina.”.

Mbali na “kupiga bilioni 14” na kutokuwa na sifa za ujenzi wa uwanja wa ndege, huku ikipewa tenda ya kujenga uwanja wa zaidi ya Sh. 40 bilioni, kampuni hiyo imeshindwa pia kujenga barabara ya Makutano – Nata (km 50), mkoani Mara. Na taarifa ya CAG ya 2016/17 imeonyesha kuwa kampuni hiyo imelipwa na TANROADS fedha zaidi ya kiwango ilichostahili. Juu ya kile ilichostahili, imelipwa Sh. 951,815,664 zaidi.

Kifua ambacho kampuni hii imekuwa inakingiwa na upendeleo inaopewa katika mazingira haya ya kifisadi, huku Rais Magufuli akijitutumua kukema na “kutumbua” wengine anaoita mafisadi, huku akikingia kifua kampuni inayochota hela kijanja janja na kushindwa kutiiza kazi inazopewa, ni baadhi ya masuala yanayomomonyoa uadilifu wa rais katika vita dhidi ya mafisadi.

Baadhi ya watu waliofanya naye kazi kwa karibu akiwa waziri na sasa akiwa rais, wanasema kuwa hatua nyingi anazochukua rais kuadhibu watu anaowataja kama mafisadi, zinawalenga watu ambao ama aliwahi kukosana nao huko nyuma au ana maslahi ambayo anataka kulinda, na anahisi kuwa wasipoondoka katika nyadhifa zao hawatamlinda.

Katika hali isiyo ya kaiwada, hata CAG katika ripoti ya mwaka 2016/2017 hakuonyesha upungufu wa fedha za uwanja wa ndege Chato ambazo kisheria zimechotwa na kupelekwa nyumbani kwa rais bila idhini ya Bunge. Alipoulizwa kwanini hajazikagua alisukumia wabunge mzigo huo akisema ndio wanapaswa kuhoji kwanini fedha hizo zimetukika bila idhini yao.

Hata hivyo, wabunge walishtuka muda mrefu, na wamekuwa anahoji kwa nyakati mbalimbali, hata wengine kufananisha mradi huo na ufisadi wa dikteta Mobutu Seseseko wa Zaire aliyechota fedha za umma na kujenga uwanja wa ndege kijijini kwake Gbadolite. Uwanja huo ulitumika hadi alipoondolewa maradakani, akakimbilia na kufia uhamishoni Morocco mwaka 1997. Sasa hivi umegeuka pori.

Baadhi ya wachambuzi wanasema ufisadi huu wa Chato ni moja ya sababu zinazomfanya Rais Magufuli kutisha wakosoaji na wapinzani, na kufungia vyombo vya habari   vya uchunguzi.

Like
81
12 Comments
  1. Sheri banda 6 years ago
    Reply

    UJINGA WA WATANZANIA UTAMNEEMESHA,HUYU SIYO KIONGOZI NA HAJAWAHI KUWA KIONGOZI.Tumpinge,tumkosoe na tumwambie ukweli.

    8

    2
  2. Wailerz 6 years ago
    Reply

    We need to have an active national assembly.

    0

    0
  3. Makina 6 years ago
    Reply

    Mr Ngurumo, Twambie Nini shida hapa? Mm sio mwanasiasa naona shida ipo, Je wabunge wa Tanzania Vipi? Au hawasomi na kuskia haya? Hii hali inaashiria giza kubwa mbele! Ivi nini kifanyike mambo yatengemee?

    2

    0
    • Katala Mohamed 6 years ago
      Reply

      Nchi inaangamia nini kifanyike kuiokoa nchi haswa ukizingatia haturuhusiwi kuongea chochote na bwana mkubwa huyu

      2

      0
  4. kibegu 6 years ago
    Reply

    Huu upigaji dili ni mkali kuliko nchi yoyote Afrika.

    1

    0
  5. Rashidi 6 years ago
    Reply

    Add me too

    1

    0
  6. Jeff Chumi 6 years ago
    Reply

    Wewe umefanya nini kwaajili ya taifa lako…..?
    Uwezo wako wa kufikiri bila udikteta hauta pambazuma kama umeshindwa kutumia uhuru wa kidemokrasia ulionao tokea ulipozaliwa.

    2

    3
  7. Dotto 6 years ago
    Reply

    Doo mbona hatari

    1

    2
  8. Mhebho Amos 6 years ago
    Reply

    Mkikosa hoja.mnaona hoja zenu zote zimemezwa.mnatafuta hata kijinga cha moto kujishikiza.ni ukweli usio pingika kuwa magufuli kameza Sera zote za upinzani.sasa mmebaki kuwaya waya tu kama kuku aliye katwa shingo kisha akaachiwa ataruuuuuka ila atakufa tu.tumpe nafasi magufuli afanye kazi.ili Tanzania isonge mbele.muungane na msigwa.lijua likali.process jay kumtia moyo rais afanye kazi.msitafute pa kuzikiwa.nyie subilini mtazikwa 2019-2020.hapo ndo hamtaonekana kabisaaaa.kama ukawa mtarudi bungeni na wabunge 20 ntaanza kujitafakari nianze kuhamia ukawa..kazi tunaiona inafanyika..tulizeni huo mshono burudoza lifanye kazi.#zittokabwe

    5

    16
  9. Tang Zhou 6 years ago
    Reply

    Magu ni lijizi tu…
    1. Nyumba za serikali – alihonga hadi malaya wake
    2. MV Bagamoyo, ilifanya safari moja ya wiki nzima kutoka Dar hadi Bagamoyo – alipoulizwa akajidai amekigawa jeshini na watu sasa wajue vifaa vya jeshi huwa havijadiliwi
    3. Malipo hewa ya Bil.263 akiwa Waziri wa Miundombinu wakiwa na Mwakyembe
    4. Trillion 1.5

    9

    1
  10. bolamimisijasema.. 6 years ago
    Reply

    kuna siku mdomo wake utajaa michanga, msiwe na wasiwasi…

    3

    0
  11. Mtanzania 6 years ago
    Reply

    Hivi huo uwanja wa Chato upo sehem gani kule Chato? Ni kwenye ardhi ya serikali au iliyokuwa ya Magufuli? Mbona kwenye google map hauonekani? Maana nautafuta sana siuoni.

    0

    0

Leave a Comment

Your email address will not be published.