Kamati ya Bunge yabaini kashfa katika stempu za kieletroniki

Kamati ya Bajeti imesema Stempu za Kielectroniki (Electronic Tax Stamp-ETS) NI KASHFA KUBWA: Kampuni iliyopatikana kinyemela kulipwa TZS67 bilioni kwa mwaka. Hii hapa kauli ya kamati kama ilivyowasilishwa na Hawa Ghasia.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/19 Serikali imedhamiria kuanzisha Mfumo wa Stempu za Kodi za Kieletroniki ili kudhibiti udanganyifu wa wazalishaji wa bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa. Kampuni ya SCIPA kutoka Uswiss ndiyo iliyoshinda zabuni hiyo hapa nchini na ina mkataba wa miaka mitano na Serikali kwa mfumo wa Self Financing. Mfumo huo unamtaka mwekezaji kurudisha gharama zake za uwekezaji kwa kutoza stampu ya kieletroniki kwa kila bidhaa itakayozalishwa. Kiasi cha fedha kinachotarajiwa kuwekezwa na SCIPA ni Dola za Marekeni 21,533,827 sawa na Shilingi 48,472,644,577.

Mheshimiwa Spika, Kamati haina pingamizi na uanzishwaji wa mfumo huu, jambo la msingi ambalo linahitaji lifanyike kwa umakini ni kujiridhisha na gharama za mfumo huo ambazo zitabebwa na watumiaji wa bidhaa pamoja na mapato atakayoyapata mwekezaji kutokana na stempu.

Mheshimiwa Spika, Kamati ina maoni kuwa hatua ya Serikali kutoongeza ushuru wa bidhaa zisizo za petroli itakuwa haina maana kama gharama ya stempu itabaki kama ilivyopangwa na Serikali. Hatua hii itasababisha kuongezeka kwa bei kwenye vinywaji kama maji, soda, bia na juisi ambazo sasa hazitozwi stempu. Aidha, tathmini ya Kamati inaonesha kuwa pale Serikali itakapokuwa inaongeza ushuru wa bidhaa kwa asilimia ya mfumuko wa bei kama Sheria ya Ushuru wa Bidhaa inavyotaka, kiwango cha stempu kitakuwa kinaongezwa juu yake kulingana na Mkataba kwa miaka mitano (Rejea Jedwali Na. 5 na 6) linaonesha jinsi bei itakavyoongezeka kwa vinywaji baridi.

Mheshimiwa Spika, Kamati imefanya uchambuzi ili kubaini kiwango cha fedha ambacho kampuni ya SCIPA itakipata katika Mkataba huo kwa Mwaka mmoja. Uchambuzi huo umehusisha takwimu za bidhaa tatu za maji, soda na sigara bila spiriti kwa kuangalia viwango vya uzalishaji wa bidhaa hizo kwa mwaka. Uzalishaji huo unaonesha Kama ifuatavyo:- kiwango kinachozalishwa nchini kwa mwaka; Maji ni lita za ujazo 268,702,209 Soda ni lita za Ujazo 732,315,008 Bia ni lita za ujazo 409,274,746 na Sigara ni Pakti 429,310,400.

Mheshimiwa Spika, ukikadiria kwamba stempu itatozwa kwa idadi (unit) na sio kwa ujazo (lita), hivyo chupa moja ya bia ml 500 itatozwa Shilingi 22.73; Soda 500 mls itatozwa Shilingi 13.5, Spirit 1000 mls itatozwa Shilingi 29.57. Hivyo, ukijumlisha na ushuru wa bidhaa kwa kila bidhaa iliyoainishwa hapo juu inaonekana kuwa gharama itakwenda kwa mlaji wa mwisho. Kwa mantiki hii, ukokotoaji unaonesha kwa mwaka mmoja SCIPA atakusanya jumla ya Shilingi 66,690,313,798.84 bila ya kuhusisha takwimu za bidhaa ya spiriti. Aidha, Kiasi hiki ni kikubwa kuliko alichowekeza katika kipindi cha mwaka mmoja tu wa mkataba.

Mheshimiwa Spika, Kamati imekuwa ikifuatilia hatua mbalimbali za Serikali zenye lengo la kukusanya mapato yake yenyewe na sio kutumia mawakala kukusanya mapato. Mfano; kuhamisha fedha zake kutoka Benki Binafsi kupeleka Benki kuu, mfumo wa manunuzi ya Luku kutoka Kampuni ya Max Malipo na Mitandao ya simu kwenda GePGS (Government Eletronic Payment Gateway Systerm), ukusanyaji wa mapato katika mabasi ya mwendo kasi na matumizi ya mashine za EFD.

Mheshimiwa Spika, Kamati inaona kuwa Serikali kuamua kumpa SCIPA Mkataba wa miaka mitano wa kuhakiki uzalishaji kupitia stempu za kielektroniki ilhali uhakiki huu ungeweza kufanywa na Serikali yenyewe. Hata hivyo, Kamati imeona kuwa kiwango cha mapato kinachotarajiwa kukusanywa katika kipindi cha mwaka mmoja (Shilingi 66,690,313,798.84) kwa bidhaa nne zilizo ainishwa hapo juu ni kikubwa kuliko kiwango cha uwekezaji cha Shilingi 48,472,644,577 ambacho kimewekezwa na Kampuni ya SCIPA. Baada ya Kamati kufanya uchambuzi huo inaishauri Serikali yafuatayo:-

i. Serikali iwekeze yenyewe mfumo huu wenye mtaji wa kiasi cha Shilingi 48,472,644,577 ili kiasi cha fedha kitakachopatikana iwe ni sehemu ya mapato ya Serikali badala ya mapato yatokanayo na stempu kuchukuliwa na Kampuni binafsi kama ilivyofanya kwenye Mfumo wa TANCIS;

ii. Serikali ianze kutumia mfumo huu kwenye vinywaji vikali ambavyo mara kwa mara mbele ya Kamati Serikali imekuwa ikithibitisha kuna udanganyifu mkubwa; na

iii. Ni bora Serikali kuongeza ushuru wa bidhaa kwa asilimia 5 ya mfumuko wa bei kama ilivyokuwa ikifanya hapo awali kuliko inavyopendekeza sasa kutumia mfumo wa stempu kwa bidhaa hizo kwa kuwa gharama za stempu ni kubwa kuliko ushuru wa bidhaa wa asilimia 5. Mathalani ukichukua bidhaa ya soda (250 ml) inatozwa ushuru wa bidhaa kiasi cha shilingi 15 na wa stempu utatozwa kiasi cha shilingi 13.5. Hivyo, gharama ya jumla (gharama ya ushuru wa bidhaa na wa stempu) itakuwa kiasi cha 28.5 na hivyo itaongeza gharama kwa uzalishaji na kwa mlaji.

Like
3

Leave a Comment

Your email address will not be published.