England yatinga nusu fainali ya tatu. Brazil yashindwa robo fainali ya tatu

GARETH Southgate, kocha wa England, amejizolea sifa kemkem kwa kuwezesha timu yake kuingia nusu fainali baada ya miaka 28 ya kusuasua. England imeingia nusu fainali kwa kishindo baada ya kuichabanga Sweden magoli mawili bila, yaliyofungwa na Harry Maguire na Dele Alli.

Hii ni mara ya tatu kwa England kuingia nusu fainali ya kombe la dunia. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1966 walipobeba kombe la dunia; na mara ya pili ilikuwa mwaka 1990 walipoondolewa na Germany kwa penalti.

Akizungumzia hatua hii, Southgate amesema kuwa hata yeye haamini kilichotokea. “Nina furaha isiyo kifani, ni siamini kilichotokea. Naamini kila mmoja huko nyumbani anafurahia usiku wa leo, kwani mambo haya hutokea kwa nadra,” amesema.

Kwa matokeo haya, kikosi cha Southgate sasa kitachuana na Croatia Jumatano ijayo katika uwanja wa Luzhniki, jijini Moscow. Croatia imeiondoa Russia kwa penalti 4-3 baada ya timu hizo kufungana 2-2 hadi dakika ya 120 katika mechi iliyochezwa leo Jumamosi. Katika mechi nyingine ya nusu fainali, France itamenyana na Belgium.

Goli la Maguire lilifungwa kwa kichwa kutokana na krosi ya Ashley Young katika kipindi cha kwanza. Lilikuwa goli la 11 kwa England lililotokana na krosi ya aina hiyo katika michuano hii.

Alli naye alitumia vema kuzubaa kwa walinzi wa Sweden, akaunganisha krosi ya Jesse Lingard.

Kipa wa England Jordan Pickford aliokoa michomo mitatu golini – moja ya kichwa iliyopigwa na Marcus Berg, na mashuti ya Viktor Claesson na Berg.

Brazil yaishia robo fainali kwa mara ya tatu

Brazil, ambayo ilikuwa inapewa nafasi kubwa ya kutwaa kombe hili mwaka huu, iliondolewa Ijumaa katika hatua ya robo fainali baada ya kuchapwa na Belgium magoli mawili kwa moja. Kwa kipigo hicho, hii ni mara ya tatu kwa Brazil, ambayo imebeba kombe la dunia kuliko zote (mara tano), kuondolewa katika hatua ya robo fainali.

Timu hiyo, ambayo hujulikana kama Seleção, imecheza mechi 26 na kushinda 20, imetoka sare mara nne na kushindwa mara moja chini ya kocha wao Tite aliyeanza kuifundisha tangu tarehe 20 Juni 2016.

Imefunga magoli 55 na kufungwa manane (8). Kabla haijachapwa magoli mawili kwa moja na Belgium katika robo fainali iliyochezwa Ijumaa, Brazil ilikuwa imecheza mechi 15 bila kushindwa, na ilikuwa haijafungwa zaidi ya goli moja katika mechi moja.

Kipigo cha ghafla kutoka kwa Belgium ndicho kiliyeyusha matumaini ya Selecao kubeba kombe kwa mara ya sita.  Kuna matumaini kwamba licha ya kipigo hicho, kocha wao ataendelea kunoa timu hiyo kwa ajili ya michuano ijayo ya mwaka 2022.

Imepita miaka 40 tangu kocha aliyeshindwa aliporuhusiwa kubaki katika nafasi ya kuandaa timu ya taifa kwa ajili ya kombe la dunia linalofuata. Ilitokea kwa Mario Zagallo ambaye aliandaa timu kwa ajili ya kombe la dunia la mwaka 1974 nchini Germany baada ya ubingwa wa timu yake nchini Mexico mwaka 1970.

Akizungumzia mechi hiyo aliyoshindwa, Tite amesema: “Licha ya maumivu niliyonayo kwa kushindwa, bado naweza kufanya tathmini na kusema kile mpenda kabumbu safi aliyetazama pambano letu na Belgium atakuwa ameburudika.”

Like

Leave a Comment

Your email address will not be published.