Zanzibar yaanza kutoa chanjo ya Corona

ZANZIBAR imeanza kutoa chanjo dhidi ya COVID-19 kwa wananchi wake na jana watumishi wenye hatari zaidi ya kuambukizwa walidungwa kinga hiyo.

Zanzibar ilipokea shehena ya kwanza ya chanjo hiyo mwishoni mwa mwezi uliopita – Juni.

Watumishi wa awali waliodungwa chanjo hiyo ni wahudumu na maofisa tabibu katika hospitali za serikali, watumishi wa Uwanja wa Ndege wa Abeid Karume na wenzao wa Bandari ya Malindi.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Zanzibar Ahmed Mazrui amesema wameanza kutoa chanjo dhidi ya virusi vya Corona jana kwa baadhi ya watumishi ambao wako kwenye mazingira hatarishi zaidi ya kupata maambukizi.

Mazrui akizungumza na SAUTI KUBWA leo asubuhi amesema kuwa serikali iliamua kufanya jitihada za kupata chanjo mapema kwa kuwa visiwa vya Zanzibar viko katika hatari kubwa ya kuwa na wagonjwa wengi kwa kuwa ina muingiliano mkubwa wa wau kutoka mataifa mbaimbali wanaowasili visiwani humo kutalii.

“Sisi ni kisiwa kinachopokea idadi kubwa ya wageni, hivyo tuna muingiliano mkubwa na wanaokuja, hata kama kuna tahadhari, ni vyema kujikinga zaidi ili kupunguza athari za janga la Corona,” amesema Mazrui.

Waziri huyo ametanabaisha kwamba mbali na watumishi hao, baadhi ya hoteli zimeanza kutoa chanjo kwa wahudumu wake na kwamba serikali inafuatilia kwa karibu kuona mwenendo wa waliopata kinga hiyo.

Akizungumzia takwimu za maambukizi na wagonjwa wa COVID-19, Mazrui amesema kwamba hadi leo asubhi Zanzibar hakuna ripoti ya kuwepo kwa mgonjwa hata mmoja katika hospitali zote; serikali na binafsi na kwamba hakuna vifo.

Juni Mosi, mwaka huu, SAUTI KUBWA iliripoti kuwepo kwa mpango wa serikali kuagiza chanjo haraka iwezekanavyo kwa Wazanzibari ili kujihami na janga la ugonjwa huo unaoendelea kusumbua dunia.

Haijafahamika endapo Serikali ya Zanzibar imepokea shehena ya chanjo kupitia utaratibu gani; kununua kutoka kampuni zinazozalisha chanjo hizo nje ya nchi au kupitia mpango wa COVAX unaosimamiwa na Shirika la Afya Duniai (WHO) na kutolewa bure kwa chanjo kwa nchi masikini.

Hadi sasa chanjo ambazo zinasambazwa bure kwa nchi masikini, kupitia utaratibu huo maalum wa WHO ni pamoja na chanjo ya Pfizer-BioNTech – kutoka Marekani (inayotolewa kwa dozi mbili; baada ya siku 21 kutoka kupata ya kwanza); chanjo ya Moderna – kutoka Marekani yenye dozi mbili (ya pili baada ya siku 28) na chanjo ya Johnson & Johnson – kutoka marekani na Uholanzi yenye dozi moja tu.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, haijaweka bayana kuanza kupokea chanjo hizo, licha ya kuonyesha utayari wa kukubali na kuridhia matumizi yake kwa binadamu.

Msimamo huo wa serikali ya sasa ni kinyume na mtazamo wa Rais John Magufuli aliyeamini kutofanya kazi vyema kwa chanjo hizo, huku awali akipinga kuwepo kwa Corona nchini mwake. Rais Magufuli alifariki dunia Machi 17, 2021 kwa ugonjwa unaoelezwa na baadhi ya vyanzo kuwa ni Corona, ingawa serikali ilieleza chanzo cha kifo kuwa matatizo yake ya moyo kwa muda mrefu.

Like