Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke Sweden aliyejiuzulu juzi arejea madarakani

MAGDALENA Anderson, mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa Waziri Mkuu wa Sweden, ambaye alijiuzulu wiki iliyopita baada ya bajeti yake kukataliwa na Bunge, amechaguliwa tena kwenye wadhifa huo.

Kiongozi huyo wa chama cha Social Democrats amepata ushindi mwembamba baada ya kuungwa mkono na wabunge wengi kwenye kura zilizopigwa Jumatatu tarehe 29 Novemba 2021.

Sweden inafuata mfumo wa kibunge. Bunge ndilo huchagua waziri mkuu ambaye ndiye huunda serikali.

Bi Anderson anatarajiwa kuongoza serikali ya chama kimoja mpaka uchaguzi ujao utakaofanyika mwezi Septemba mwakani.

Alijiuzulu Jumatano wiki iliyopita baada ya muungano wa vyama aliokuwa akiuongoza kuvunjika kutokana na Bunge kupigia kura bajeti ya upinzani.

Uamuzi huo ulitokea saa zipatazo saba baada ya Bi Anderson kuteuliwa, lakini mambo yalimwendea mrama baada ya mpango wake wa kiuchumi wa kuwa na serikali ya muungano na chama cha kijani (Green Party) kusambaratika kutokana na pendekezo lake la bajeti kushindwa kupitishwa katika Bunge la nchi hiyo.

Badala yake, Bunge lilipitisha pendekezo la bajeti iliyopendekezwa na vyama vya upinzani vikiongozwa na chama cha Sweden Democrats chenye mrengo wa kulia.

Green Party kiliikataa bajeti iliyotengenezwa na chama cha upinzani na chenye mrengo wa kulia na hivyo kujiengua rasmi serikalini.

Hivyo, Bi Anderson alijiuzulu rasmi kwani, kisheria, waziri mkuu wa Sweden anapaswa kujiuzulu pale serikari ya muungano inapoachia ngazi.

Katika kura zilizopigwa siku ya Jumatatu, wabunge 101 kati ya 349 wa chama cha Riksdag walimpigia kura za ndiyo, huku 173 wakipiga kura ya hapana.

Bi Anderson anatarajiwa kuwa na wakati mgumu sana wakati wa kupitisha miswada bungeni kutokana na kutokuungwa mkono na vyama vingine vya kisiasa nchini humo kwani chama cha Social Democrats kina jumla ya viti 100 kati ya viti 349 bungeni.

Bi Anderson, ambaye ni bingwa wa zamani wa kuogelea kutoka chuo kikuu cha Uppsala, alianza rasmi mapambano yake kisiasa mwaka 1996 kama mshauri wa kisiasa wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa kipindi hicho, Goran Persson.

Kwa miaka saba iliyopita, alikuwa ni waziri wa fedha. Majuzi tu amekuwa mkuu wa chama cha Social Democrats mwanzoni mwa mwezi Novemba baada ya kuchukua nafasi ya Stephan Lofven ambaye alijiuzuru nafasi ya Waziri Mkuu baada ya kuhudumu kwa miaka saba.

Mpaka Bi Anderson anakaimu ofisi, Lofven alikuwa ameitumikia nchi hiyo kama waziri mkuu wa Sweden tangu Oktoba 2014 hadi Novemba 2021. Lofven aliplazimika kuondoka madarakani baada ya Bunge kumpigia kura ya kukosa imani na serikali yake.

Like