Watanzania wamlima barua ya wazi Mwanasheria Mkuu Kilangi dhidi ya “udikteta nyemelezi”

Adelardus Kilangi

Ndugu Dk. Adelardus Kilangi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali,

Tunakupa pole kwa majukumu na mazito yaliyo mbele yako.

Tunatambua kuwa leo umewasilisha muswada bungeni utakaobadili kabida mfumo wetu wa kidemokrasia nchini Tanzania.

Wapo watanzania waliamini wakati wa uteuzi wako waliposikia cheo chako cha udaktari kuwa hatimaye sekta ya sheria imepata mkombozi. Wengi walidhani kuwa kwasababu wewe haukutokana na mfumo wa serikali basi labda ungeleta katika tasnia changamoto mpya na nzuri na kutusaidia kuondokana na miaka mingi ya sheria kandamizi dhidi ya wanyonge wa nchi yetu.

Sio wengi waliojua kuwa uteuzi wako wenyewe ulikikuka matakwa ya ibara ya 59 ya katiba yetu. Si wengi wanaofahamu kuwa wewe hukuwahi kuwa wakili kwa kipindi cha miaka kumi mfululizo kama katiba inavotaka. Wengi hawafahamu kuwa hukuwahi kuwa mtumishi wa serikali mwenye sifa za kuwa wakili kwa kipindi cha miaka kumi kama katiba inavotaka. Watanzania hawafahamu kuwa wewe ni zao la uvunjifu wa katiba.

Hata walipotokea Watanzania wanaoelewa dhahma ya uteuzi wako na kuamua kukupeleka wewe na Mheshimiwa Rais aliyekuteua mahakamani wamekutapa na udhalimu wa hali ya juu. Huko mahakamani Jaji Kiongozi amejipa mamlaka ya kimungu na kumsimamisha wakili aliyekwenda kwa niaba ya wananchi kuhoji uteuzi wako.

Ndugu Kilangi, Watanzania wengi wasingejishughulisha sana na wewe lakini umekuwa maarufu kuwahadaa na kuwafanyia madhali na uovu kwa kupitia kazi yako. Leo hii chini ya usimamizi wako tangu mwaka 2017 nchi yetu imepitisha sheria nyingi za ajabu ajabu. Asasi za kiraia zimetungiwa sheria ambazo hazikuwahi kuonekana kokote duniani, watafiti wametungiwa sheria zilizowazuia kufanya kazi yao ya kutafiti na kuhoji, vyama vya siasa vimefungwa kitanzi kwa sheria ulizoleta wewe. Wawekezaji wa madini uliwatungia sheria za ajabu ajabu na baada ya wao kuwabana ukaidhalilisha nchi kwa kuwaruhusu wawekezaji hao kuingia mkataba na serikali unaokiuka sheria ulizozipeleka mwenyewe bungeni.

Ndugu Kilangi, wewe umekuwa nguzo muhimu sana ya kuchochea na kuikita mizizi ya udikteta nchini kwetu. Umeifanya kazi hiyo kwa uaminifu mkubwa kwa Rais aliyekuteua lakini kwa udhalimu mkubwa kwetu sisi wananchi na zaidi kwa katiba uliyoapa kuilinda. Ushujaa wako katika kuleta sheria kandamizi na kulinajisi bunge letu tukufu utakumbukwa kwa muda mrefu sana.

Naomba kukumbusha kuwa utawala ni jambo la wakati. Rais Magufuli aliyekuteua tuna uhakika atapita aidha kwa kumaliza muda wake au kwa kufariki dunia. Atakapoondoka, watanzania tutakukumbuka kama mtu uliyemuwezesha Magufuli kuinajisi katiba yetu na kuyanajisi matumaini yetu ya kuishi kwa uhuru na kwa mamlaka tuliyojipa kupitia ibara ya 3 ya katiba yetu.

Ni imani yetu kuwa utahukumiwa mwisho wa muda wako kulingana na haki na dhulma uliyotuletea nchini kwetu.

Wakatabahu,

Watanzania wanyonge tunaokereka na udikteta nyemelezi.

Like
29

Leave a Comment

Your email address will not be published.