Watanzania sasa kupata chanjo ya Corona Desemba 2021

BAADHI ya Watanzania maarufu wakiwamo waandishi wa habari, wanamichezo, wanasiasa na wafanyabiashara ambao tayari wamechanjwa dhidi ya maambukizi ya COVID-19, wamehimiza serikali ya Tanzania ifanye haraka kuleta chanjo nchini ili kupunguza vifo na madhara ya kiafya, kijamii na kiuchumi.

Watanzania hao wamehojiwa na SAUTI KUBWA kwa nyakati mbalimbali wakiwa nje na ndani ya nchi, hasa waliorejea kutoka ng’ambo ambako walipatiwa chanjo hiyo inayotajwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa njia sahihi – angalau kwa sasa – ili kupunguza makali ya virusi vya Corona.

Tayari serikali ya Tanzania imeeleza kwamba itapokea shehena yake ya kwanza ya chanjo ya Corona Desemba mwaka huu, na kazi ya kuchanja itaanza mara moja.

Kwa upande wa Zanzibar, tayari wamepokea chanjo na wameanza kuitumia.

Leo Jumanne, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, amesema serikali imeridhika na ubora wa chanjo zinazotolewa duniani na imekamilisha taratibu zote za kupokea shehena ya chanjo ambayo inatarajiwa ianze kutolewa mwishoni mwa mwaka huu.

“Kila vita hupiganwa kulingana na ukubwa wa vita, mwanzoni tuliona vita ya kupambana na COVID-19 ni kutumia nyungu, maombi na dawa za asili, lakini kadri virusi vinavyobadilika, mapambano yanabadilika pia, hivyo sasa chanjo hii itatolewa kwa hiari,” amesema Dk. Gwajima.

Maulid Kitenge, mtangazaji na mkuu wa idara  ya michezo, Wasafi FM, Dar es Salaam – ambaye amepata chanjo hiyo huko California, Marekani wiki iliyopita – ameiambia SAUTI KUBWA kwamba tangu adungwe chanjo hiyo, hajaona mabadiliko yoyote katika mwili wake.

Akiwa bado nchini Marekani, Kitenge ameendelea kuhimiza Watanzania “kuchangamkia” kuchanjwa ili kujikinga na kukinga watu wengine dhidi ya maambukizi ya Corona.

“Ili kuokoa kuporomoka kwa uchumi na kulinda afya za Watanzania, ni vyema kila mmoja akachanjwa wakati chanjo zitakapoanza kutolewa nchini, watu wasidanganywe na propaganda za kutishwa juu ya madhara unapochanjwa,” amehimiza na kuonya.

Oscar Oscar, Mtanzania mwingine ambaye amechanjwa tayari, akiwa California, Marekani, amesema tangu kuchanjwa kwake hajasikia lolote baya katika mwili wake na amehimiza Watanzania kuchanjwa pindi chanjo hizo zitakapowasili nchini. Oscar ni mtangazaji wa michezo wa EFM, Dar es Salaam.

Alhaj Ismail Aden Rage, rais mstaafu wa Klabu ya Simba na aliyewahi kuwa Mbunge wa Tabora Mjini, ni Mtanzania mwingine ambaye amechanjwa akiwa nje ya nchi na kupitia mitandao ya kijamii, alihimiza Watanzania kuhakikisha wanapata chanjo ili kujikinga dhidi ya virusi vya Corona na madhaya ya uchumi na afya yanayosababishwa na janga hilo.

Mtanzania anayeishi Auckland, California, Priscilla Mkenda ambaye alipata chanjo Machi, mwaka huu anasema kuwa hadi sasa Marekani na nchi zingine zinazoenelea ambako wananchi wake wamechanwa, hakua madhara makubwa yaliyorekodiwa na kuthibitishwa kitaalamu.

“Nawahimiza Watanzania wenzangu wajiandae kupokea chanjo na wajitokeze kuchwanjwa kwani itaokoa maisha yao na kuondoa wasiwasi wa vifo,” amehimiza binti huyo anayefanya biashara zake Auckland.

Rais na Mhariri Mkuu wa SK Media, Ansbert Ngurumo, ambaye pia ni mhariri mkuu wa SAUTI KUBWA ni miongoni mwa Watanzania ambao tayari wameshachanjwa. Amesema kwa kuwa serikali imebadii sera yake kuhusu Corona, ni vema ifanye haraka kutoa chanjo hiyo ili kulinda afya za wananchi wake.

“Miezi kadhaa iliyopita, Tanzania ilikuwa imefikishwa mahali pa kupuuza sayansi na kuendekeza ushirikina uliovalishwa koti la imani ya dini, na watu walifuata kauli za rais kwa sababu ya mazoea yao kusikiliza na kuamini watu wenye mamlaka.

“Bahati mbaya, baadhi ya watu wale wale waliosema hakuna Corona wala hakuna haja ya chanjo, wameshatangulia mbele ya haki. Hilo nalo ni somo. Sasa kwa kuwa Rais Samia amebadili mwelekeo kisera, inatubidi tuzingatie misingi ya sayansi ili kunusuru wananchi wengi,” alisema Ngurumo.

Tangu kuibuka kwa maradhi haya, Tanzania imepitia wakati mgumu kwa sababu ya msimamo wa kisiasa na kauli za Rais aliyekuwa madarakani wakati ule, John Magufuli, ambaye alidiriki kutangazia dunia kuwa Tanzania haikuwa na Corona kwa sababu Mungu aliiondoa baada ya ibada ya kitaifa ya siku tatu.

Baadaye Magufuli alisisitiza kuwa Tanzania haitapokea Corona kwa sababu haamini kama “wazungu” wanaweza kutengeneza chanjo ya Corona kabla hawajatengeneza chanjo ya UKIMWI, Kansa au Malaria.

Hata hivyo, baada ya kifo chake Machi 17 2021, sera ya serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu Corona imebadilika. Sasa hivi wananchi wanahimizwa kuchukua tahadhari, na chanjo imeagizwa.

Janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 likiwa lina miezi 18 sasa duniani, idadi kubwa ya watu katika nchi zilizoendelea tayari wamepata chanjo dhidi ya ugonjwa huo.

Baadhi ya nchi zimeonyesha kuridhishwa na maendeleo ya afya za raia wao, na tayari zimelegeza baadhi ya masharti yaliyokuwa yamewekwa kama njia ya kuukabili ugonjwa huo.

Upatikanaji wa chanjo katika nchi hizo zilizoendelea umekuwa ni rahisi  kwani baadhi ya watu wamepata chanjo – iwe dozi mbili za ‘Pfizer’ au ‘Moderna’ au chanjo moja ya ‘Johnson and Johnson.’

Dk. Soumya Swaminathan, mwanasayansi mkuu wa WHO anasema, chanjo dhidi ya virusi vya Corona zinaonyesha ubora mkubwa na kwamba kwa sasa njia pekee ya kudhibiti madhara na kusambaa kwake ni chanjo.

WHO imesema Corona bado ni janga kwa ulimwengu, hivyo nchi zinapaswa kuwahimiza wananchi wake kujilinda na kulinda wale walio katika hatari zaidi ya kupata maambukizi katika jamii zao kwa kuwa wasipofanya hivyo hospitali zitazidiwa kupokea wagonjwa.

Oscar Oscar na Maulid Kitenge wakionyesha vyeti vya kuchanjwa dhidi ya Corona
Like