WASIOJULIKANA WAIBA MTOTO MWENYE UALBINO KAMACHUMU

SAUTI KUBWA imeamua kutumia picha ya mtoto huyo, Asiimwe Novati, kwa sababu maalumu ili kusaidia jitihada za uchunguzi na utafutaji. 

WATU wasiojulikana wamenyakua mtoto wa miaka miwili na nusu mwenye asili ya albino, na kutokomea naye, baada ya kumkaba koo mama yake.

Mama aliyeporwa mtoto amefahamika kwa jina la Kebyera Richard, mkazi wa Kijiji cha Bulamula, Kitongoji cha Mbale, Kata na Tarafa ya Kamachumu wilayani Muleba mkoani Kagera. 

Mtoto ambaye amechukuliwa na watu wasiojulikana anaitwa Asiimwe Novati.

Jirani wa familia hiyo, Hamad Rashid, ameiambia SAUTI KUBWA leo Mei 31, 2024 kuwa tukio hilo lilitokea jana, Mei 30,2024 muda wa saa 2:15 usiku.

Ameeleza kuwa vijana wawili ambao hadi sasa hawajafahamika, walifika nyumbani hapo kwa Kebyera, wakapiga hodi na kuomba chumvi. Walidai kuwa mwenzao amengongwa na nyoka; hivyo walitaka kumpa matibabu ya dharura kwa kutumia chumvi. 

Rashid anasema, mama wa mtoto huyo ambaye wakati huo alikuwa nyumbani na mtoto wake, alifungua mlango na kuwapelekea chumvi huku akiwa amewasha tochi ya simu.

Hata hivyo, wakati anawapa chumvi, mmoja wao alimkamata mama huyo na kumkaba koo; huku mwenzake akiingia ndani kwa haraka na kumchukua mtoto aliyekuwa akicheza sebuleni; na akatokomea naye kusikojulikana.

Rashid amesimulia kuwa kijana aliyekuwa amemkaba mama wa mtoto huyo, baada ya kuona mwenzake ameshamkwapua mtoto na kutoka naye nje, alimwachia mama huyo na kukimbia, huku mama mtoto akibaki kupiga yowe kuomba msaada kwa majirani.

Rashidi amesimulia kuwa, baada ya wananchi kusikia yowe na kukusanyika nyumbani kwa Kebyera, walipiga simu polisi; na polisi walifika hima, kufanya mahojiano na kuanza upelelezi.

Bibi wa mtoto huyo, Odina Richard, ambaye anaishi Kanoni Kata ya Kamachumu, amesema kuwa alipigiwa simu na Kebyera binti yake – saa 2:30 usiku, na kuelezwa tukio  lilivyokuwa.

Bibi huyo anasimulia kuwa bintiye alimweleza kuwa ilikuwa muda huo wa saa 2:15 wakati mume wake, Novati, hajatoka kazini, watu hao wasiojulikana waliposikika nje ya nyumba yao.

Anasimulia kuwa binti yake alimweleza kwamba kabla wanyang`anyi hawajapiga hodi, walianza kuita: “Mama Asiimwe! Mama Asiimwe” – kama majirani wanaofahamiana.  

Mmoja wa watu hao wasiojulikana alikuwa akimwambia Mama Asiimwe kuwa amengongwa na nyoka mguuni na kwamba anaomba chumvi ili imsaidie kuondoa sumu.

Huku akibubujikwa machozi, Bibi Asiimwe haachi kupaza sauti na kauli za kujuta, akisema “inauma sana, inauma sana,” na kwamba hajui kama atamwona tena mjukuu wake. Anaomba Serikali imsaidie kumpata mjukuu wake akiwa hai.

Akihojiana na SAUTI KUBWA leo Mei 31, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Gabriel Makungu amethibitisha kuwepo tukio hilo na kusema timu yake ya polisi imeanza uchunguzi juu ya tukio hilo.

Kamanda Makungu amerejea kauli ya mama na bibi wa mtoto huyo albino kwamba mtu asiyejulikana aligonja mlango wa mama Asiimwe, akiomba apewe chumvi ya kuweka kwenye mguu wake, kwa madai kuwa amengongwa na nyoka. 

Lakini alipofungua mlango na kutoka nje, mtu huyo alimkaba koo na mwenzake kupata upenyo wa kuingia ndani kumpora mtoto Asiimwe. Amesema jeshi la polisi tayari limefika eneo la tukio na timu yake inaendelea na upelelezi.

Matukio ya kuvamiwa, kutekwa na kukatwa viungo, watu wenye ualbino, yalikuwa yametoweka kwa karibu miaka 10 hivi. Waliokuwa wamethibitika kuhusika na matukio hayo, bado wanaendelea kutumikia vifungo vya maisha jela.

SAUTI KUBWA imeamua kutumia picha ya mtoto huyo kwa sababu maalumu ili kusaidia jitihada za uchunguzi na utafutaji. 

 

Like
2