Wanazuoni wamtaka Magufuli aache mawaziri watumie maarifa yao badala ya maagizo yake

BAADA ya Rais John Magufuli kutangaza Baraza la Mawaziri leo Mjini Dodoma,  baadhi ya wachambuzi, wakiwemo wanazuoni wawili, wamemtaka rais aache kulazimisha wateule wake kufuata maagizo yake; badala yake awaache watumie elimu, ujuzi na stadi zao katika utendaji.

Wamesema kuwa katika miaka mitano iliyopita, wateule wengi wa rais walijikita katika kutekeleza maagizo yake ili kumfurahisha badala ya kutumia maarifa yao. Utendaji wa aina hiyo, wanasema, unaua taaluma na talanta za wahusika; na unazalisha watendaji wanaojipendekeza, wanaotenda makosa wakijua, ilimradi yanabarikiwa na, au yanakubalika kwa, rais.

Dk. Azaveri Lwaitama anasema wengi walioteuliwa ni wageni, hawafahamiki utendaji wao, kwani hawakuwa katika baraza lililopita, lakini anadokeza kuwa wengi waliokuwa katika baraza lililopita, walionyesha uwezo mdogo mno kiutendaji kwa sababu rais hakuwapa nafasi, bali alikuwa anawaagiza na kuwasimamia, kwa maana kwamba hata makosa mengi waliyotenda, kimsingi ni makosa ya rais.

“Ukiangalia baraza jipya,  Magufuli amewaacha wengi (waliozoeleka), na umesikia akiwasema baadhi yao kwamba walikuwa wakienda kustarehe mbugani kwa gharama za walipakodi wa Tanzania. Sasa hao walikuwamo wengi. Ni matarajio kwamba hawa wapya watachapa kazi zaidi.

Lwaitama ni mhadhiri mstaafu wa vyuo vikuu kadhaa Tanzania vikiwamo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Josiah Kibira University College cha Kagera.

Mwanazuoni na mchumi aliyebobea, Hamis Lugale wa KM Law Chambers, amekosoa tabia ya rais kusuta hadharani baadhi ya wasaidizi wake waliopita wakati amekuwa nao muda wote serikalini.

Anasema mawaziri ni “mkono wa rais,” na kwamba wanapokosea, ni wajibu wake kuwasahihisha bila kusubiri kuwasuta hadharani, tena baada ya kumaliza kipindi chao. Mmoja wa mawaziri waliosutwa leo ni Hamis Kigwangwalla ambaye alitumikia wadhifa wake wa waziri wa maliasili na utalii hadi mwisho wa uchaguzi mkuu wa 2020.

“Nimemsikia Rais Magufuli akisema kuna waziri mmoja alikuwa anachukua ndege za serikali kwenda kustarehe. Sasa nashangaa kwanini alimuacha tu afuje mali hadi leo,. Hii tabia aiache. Mtu akivuruga, atimuliwe haraka,” amesema msomi huyo.

Mchumi huyu haoni sababu ya rais kumwacha msaidizi wake akavuruga hadi mwisho, halafu yeye akajitokeza hadharani kumsuta.

Hata hivyo, anasema kuwa kwa jinsi alivyofuatilia sifa za kazi za mawaziri wapya, ana imani watafanya kazi nzuri ya kumsaidia Rais Magufuli. Amewataka kujiamini na kutenda kwa maarifa badala ya kusukumwa na mamlaka iliyo juu yao.

Kauli zao wanazuoni hao zinaungwa mkono na mchumi na mwanasiasa wa upinzani, Zitto Kabwe, ambaye ni Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo.

Hata hivyo, yeye anajielekeza katika hoja ya baraza kutokuwa na waziri Mzanzibari. Anasema inashangaza, na ni kwa mara ya kwanza Baraza la Mawaziri halina waziri kutoka Zanzibar, kama ambavyo imezoeleka tangu kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964.

“Baraza la Mawaziri la Tanganyika limekula kiapo siku ya uhuru wa Tanganyika. Haijapata kutokea tangu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa Baraza la Mawaziri la Muungano kuwa na mawaziri kutoka Tanganyika pekee. Katiba inalazimisha uteuzi kuzingatia uwiano wa pande mbili za Muungano,” ameandika katika wa Twitter.

Katika hali isiyozoeleka, Rais Magufuli amesema atatengua uteuzi wa Francis Ndulane, ambaye aliteuliwa kuwa naibu waziri wa madini, kwa kuwa mteule huyo amesitasita wakati anasoma kiapo mbele ya rais. Tafsiri ya rais ni kwamba Ndulane ameshindwa kuapa vizuri. Rais amesema pia kuwa serikali itachunguza vyeti vya Ndulane ili kuthibitisha kiwango chake cha elimu.

Ndulane ni mtumishi wa serikali mzoefu. Amewahi kuwa Mhasibu Mkuu wa Tanroads Mkoa wa Lindi na Mkurugenzi Mtendaji wa Mji wa Ifakara kwa nyakati tofauti. Ana Shahada ya Uzamili ya Uhasibu na Fedha kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe.

Like