Sakata la Shule ya St. Jude laibua hoja ya sheria mbaya za kodi na athari zake kwa elimu, afya

SHERIA mbaya ya kodi nchini Tanzania kwa mashirika na taasisi zisizotengeneza faida, huenda ikaendelea kukwamisha ustawi wa jamii kupitia kada za elimu na afya.

Taasisi, mashirika ya dini na jumuia zimekuwa, kwa miaka mingi, tangu huru hadi sasa, zimekuwa chachu na wadau wakubwa wa maendeleo kwa kumiliki shule, vyuo, zahanati na hospitali ambazo huendeshwa kwa njia ya kutoa huduma zaidi kwa jamii na sio kwa kutafuta faida.

Hata hivyo, kuwepo kwa sheria inayoruhusu ukusanyaji wa kodi ya taasisi kutoka kwenye mashirika yanayotoa huduma za kijamii bure, huenda kukazifanya kufunga shughuli zake mpaka hapo sheria mbaya ya kodi itakapobadilishwa.

Mfano mzuri katika muktadha huu ni hatua ya uongozi wa Shule ya Mtakatifu Jude, Arusha kufunga shule zake kwa kuwa serikali, kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ‘imekausha’ akaunti za benki kwa kuchota Sh. Milioni 500 ikiwa ni kile kinachoelezwa na serikali kuwa ni malimbikizo ya kodi ya kitaasisi ambayo haijalipwa na shule.

Kuchotwa kwa kiasi hicho kikubwa cha fedha kumefanya uongozi wa shule hiyo kusitisha masomo na wanafunzi kurejeshwa makwao, wafanyakazi kupumzishwa na kuwepo kwa hatari ya kufungwa kabisa kwa shule hizo zilizokuwa zikiendeshwa kwa michango ya hiari kutoka kwa wafadhili wa ndani na nje ya Tanzania.

Kimsingi, kuchotwa kwa fedha hizo kunatokana na sheria ya kodi kushindwa kutofautisha  kati ya faida ya kitaasisi inayotengenezwa na aasisi zenye mtaji wa kufanya biashara (company limited by shares) na kwa kutumia mtaji huo, kwa upande mmoja, na faida ya kitaasisi inayotengenezwa na taasisi kwa kutumia mtaji unaotokana na michango ya wasamaria wema (company limited guarantee) lakini. Kwa mujibu wa sheria ya kodi ya sasa, ziada yoyote inayozalishwa kutokana na biashara inayofanywa na taasisi lazima itozwe kodi bila kujali mtaji umetoka wapi wala faida imepelekwa wapi.

Shule ya Mt. Jude, iliyosajiliwa na serikali, kupitia wakala wa usajili wa kampuni (BRELA), kama kampuni isiyo na mtaji wa biashara, wakurugenzi wake hawagawani faida yoyote inayotokana na shughuli za shule hiyo. Lakini bado, serikali inaitaka shule hii kulipa kodi inayotozwa kwenye mapato ya taasisi zinazofanya biashara na kugawanya faida kwa wakurugenzi.

Chimbuko la mgogoro

Mgogoro wa kikodi baina ya TRA na uongozi wa shule za Mt. Jude, ulianza mwaka 2012 wakati ambapo shule hiyo ilitakiwa kuanza kulipa kodi kwa serikali. Katika mawasiliano ya awali, uongozi wa shule na TRA haukuweza kufikia muafaka.

Agosti 23, 2012, uongozi wa Shule za Mt. Jude, ulipokea kutoka kwa Kamisha Mkuu wa TRA, taarifa iliyoonyesha tathmini ya kodi inayotozwa kwenye mapato ya taasisi zinazofanya biashara na kugawanya faida kwa wakurugenzi.

Shule ilielekezwa kulipa kodi ya kitaasisi ipatayo  Sh. 4,243,328,159 kutokana na ziada ya mapato iliyokuwa benki baada ya kutoa matumizi yote ya mwaka 2009 na mwaka 2010.

Kwa mujibu wa vitabu vya ukaguzi wa hesabu za fedha za shule, kwenye benki kulikuwa na akiba ya Sh. 3,006,347,431 kwa mwaka wa fedha ulioishia 2009 na akiba ya Sh. 4,114,741,021 kwa mwaka wa fedha ulioishia 2010.

Kwa hiyo, katika miaka hiyo miwili, Shule za Mt. Jude zilitakiwa kulipa kodi inayotozwa kwenye mapato ya taasisi inayofanya biashara ambayo ni sawa na asilimia 60 ya akiba iliyokutwa kwenye akaunti za benki zinazomilikiwa na shule hizo. Uongozi wa Shule za Mt. Jude ulipinga maelekezo hayo kutoka kwa Kamisha Mkuu wa TRA.

Tarehe 28 Agosti 2012 uongozi wa Shule za Mt. Jude ulisajili malalamiko rasmi dhidi ya uamuzi wa Kamishna wa TRA, ukimwomba Kamishna achunguze na kutoa hukumu inayothibitisha mambo mawili.

Katika sababu ya kwanza, uongozi wa Shule ulidai kwamba, kwa mujibu wa katiba yake,  wao ni tasisi ambayo imesajiliwa kama kampuni isiyo na mtaji wa biashara, lakini yenye mamlaka ya kukusanya zawadi, michango na fadhila kwa ajili ya kutoa huduma kwa jamii, hususani msaada wa kielimu kwa watoto maskini.

Na katika sababu ya pili, uongozi wa Shule ulidai kwamba, kwa kuangalia aina ya majukumu yanayotekelezwa shuleni kwao, kuna ushahidi mkubwa wenye kuthibitisha kwamba wanatekeleza kazi mbazo sio za kibiashara.

Maombi haya yalifanyika kwa kuzingatia mwongozo wa kifungu cha 131 cha Sheria ya Kodi ya Mapato Na. 11 ya mwaka 2004.

Katika uamuzi wake, Kamishna wa TRA alikataa sababu zote mbili na kusisitiza kwamba, Shule za Mt. Jude zinapaswa kulipa kodi inayotozwa kwenye mapato ya taasisi inayofanya biashara kwa sababu mbili, kama walivyoelekezwa hapo awali na Kamishna wa TRA.

Katika sababu ya kwanza, Kamishna wa TRA alidai kwamba, kwa mujibu wa katiba yake,  Shule za Mt. Jude ni tasisi ambazo zimesajiliwa chini ya kampuni isiyo na mtaji wa biashara, lakini yenye mamlaka ya kukusanya zawadi, michango na fadhila ambavyo ni vyanzo vya mapato vinavyotozwa kodi kwa mujibu wa sheria.

Na katika sababu ya pili, Kamishna wa TRA ilidai kwamba, Shule za Mt. Jude ni tasisi ambayo inayofanya biashara yenye kuzalisha faida kwa kuwafundisha wanafunzi ambao karo zao zinalipwa kwa njia ya zawadi, michango na fadhila kutoka kwa mtu wa tatu badala ya kulipwa na wazazi wa wanafunzi husika.

Uongozi wa Shule za Mt. Jude haukubaliana na uamuzi wa Kamishna wa TRA. Hivyo, uliamua kukata rufaa kwenye Bodi ya Rufaa ya Kodi. Rufaa yao ilitupwa, na uamuzi ya Kamishna wa TRA kuthibitishwa. Uongozi wa shule ukakata rufaa tena kwenye Mahakama ya Biashara. Rufaa ilitupwa tena, na uamuzi ya Kamishna wa TRA kuthibitishwa. Hatimaye, uongozi wa shule ulikata rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa. Bado rufaa ilitupwa, na uamuzi ya Kamishna wa TRA kuthibitishwa.

Uongozi wa Shule za Mt. Jude ulipoteza rufaa zake kutokana na tafsiri ya kisheria iliyotolewa kuhusu tafsiri sahihi ya vifungu vifuatavyo: maana ya neno “biashara” kwa mujibu wa fasili inayopatikana kwenye ibara ya 3 ya sheria ya kodi; aina ya mapato yanayopaswa kutozwa kodi chini ya ibara za  8(1), 8(2)(f) na 8(3) za sheria ya kodi na kifungu cha 1(k) katika nyongeza ya pili ya sheria ya kodi. Ilithibitika kuwa, kwa mujibu wa ibara za 8(1) na 8(2)(f) za sheria ya kodi, mapato yenye sura ya zawadi, michango na ufadhili yanapaswa kutozwa kodi.

“Mahakama ya Rufaa inakubaliana na Mahakama ya Kazi kwamba, gharama za elimu ya bure inayotolewa na Shule za Mt. Jude  zinalipwa na watu baki badala ya wazazi kiasi kwamba ziada inayopatikana kwenye akaunti za benki za shule ni ziada iliyotokana na biashara inayozaa faida kupitia sekta ya elimu, na ziada hii inapaswa kutozwa kodi inayotozwa kwenye mapato ya taasisi inayofanya biashara,” ilisema hukumu ya Mahakama ya Rufaa ya Dodoma (uk.18).

Hukumu hii ilitolewa tarehe 7 Julai 2018 chini ya majaji watatu, yaani: Jaji Mkuu, L.H. Juma; Jaji wa Mahakama ya Rufaa, A.G. Mwarija; na Jaji wa Mahakama ya Rufaa, R.E Mziray.

Utata wa sheria ya kodi  

Hukumu ya rufaa iliyokatwa na uongozi wa shule za Mt. Jude dhidi ya kamishna wa TRA ilitoka mwaka mmoja kabla ya kutungwa kwa Sheria ya Kurekebisha Vifungu Mbalimbali Katika Sheria za Tanzania, Namba 03 ya mwaka 2019; yaani “Written Laws (Miscellaneous Amendments) Act, No. 03 of 2019.”

Sheria hii ilifanya mabadiliko kadhaa katika sheria ya kampuni na sheria ya vyama vya kijamii, yaliyolenga kutatua baadhi ya matatizo kama yalilojitokeza kwenye mgogoro kati ya TRA na Uongozi wa Shule za Mt. Jude.

Kwa mfano, Sheria mpya ilitaja fasili mpya za maneno “kampuni,” “shughuli ya uwekezaji,” “shughuli ya kibiashara,” na “biashara.” Kwa mujibu wa sheria hii, “kampuni” ni taasisi ambayo inataka ama kufanya biashara” au “shughuli ya uwekezaji” au “shughuli ya kibiashara.” Pia sheria hii imebadilisha vifungu kadhaa kwenye sheria inayoratibu usajili wa kampuni.

Kwa mfano, kulingana na mabadiliko yaliyofanyika kupitia ibara mpya za 3(3), 3A na 14(6) kwenye sheria ya kampuni, ili taasisi isajiliwe chini ya BRELA lazima itimize vigezo angalu vitatu. Mosi, lazima iwe inakusudia kufanya ama biashara, au shughuli za kibiashara, au shughuli za uwekezaji au shughuli nyingine ambayo itaruhusiwa na waziri husika. Pili, lazima iwe ni

taasisi yenye mtaji wa biashara. Na tatu, moja ya malengo ya waanzilishi wake lazima liwe kutafuta na kugawana faida itakayopatikana.

Kama vigezo hivi havijatimia, taasisi inapaswa ikasajiliwe kwingineko. Yaani, ama kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani, kwenye Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kwenye Wizara ya Elimu au kwingineko. Wizara ya Mambo ya Ndani inasajili taasisi ambazo zinakusudia kuwahudumia wanachama wake pekee na sio vinginevyo. Mfano mzuri hapa ni usajili wa taasisi za kidini.

Lakini, kama taasisi za kidini zinataka kutoa huduma kwa jamii pana katika sekta ya afya, elimu au kwingineko, lazima huduma hizo zisajiliwe chini ya mamlaka inayoratibu sekta hizo.

Kwa mfano, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inasajili taasisi ambazo zinakusudia kuhudumia jamii bila kujali kama ni wanachama wake au hapana. Usajili wa hospitali zinazoendeshwa na taasisi za kidini unafanyika hapa, na sio BRELA, kwa kuwa wamiliki wa hospitali hizi hawakusudii kugawana ziada itakayopatikana baada ya kutoa matumizi ya taasisi.

Na Wizara ya Elimu inasajili taasisi zote zinazotoa elimu na mafunzo. Usajili wa shule zinazotoa huduma ya elimu kama vile shule za Mt. Jude unafanyika hapa, na sio BRELA, kwa kuwa wamiliki wa shule hizi hawakusudii kugawana ziada itakayopatikana baada ya kutoa matumizi ya taasisi.

Hata hivyo, sheria namba 03/2019, sheria ya kodi ya mwaka 2004 na marekebisho yake, pamoja na sheria ya makampuni na marekebisho yake havikujielekeza katika kutatua mgogoro wa ulipaji wa kodi ya kitaasisi unaotakiwa kufanywa kisheria na asasi za kiraia zinazofanya biashara kwa kutumia zawadi na misaada kwa lengo la kuzalisha faida ambayo itaingizwa kwenye utoaji wa huduma za bure badala ya wakurugenzi kugawana faida hiyo. Hili ndilo chimbuko la mgogoro kati ya shule ya Mt. Jude na TRA.

TRA yakausha akaunti

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliamua kuchota kiasi kikubwa cha fedha kutoka akaunti za Shule za Mt. Jude kwa sababu ya madai kwamba shule ilikuwa haijalipa kodi inayotozwa kwenye mapato ya taasisi zinazofanya biashara kwa muda mrefu.

Uongozi wa TRA Mkoa wa Arusha, Novemba 3, 2020, ulichukua “kwa nguvu” Sh. milioni 500 kutoka akaunti za benki za shule hizo  zinazosomesha bure watoto wa Watanzania.

Akizungumza na vyombo vya habari, Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha, John Mwigura, alikiri kuamuru fedha hizo zichukuliwe, lakini akatetea uamuzi huo kwa kutumia hoja kwamba, TRA walifanya uamuzi huo kwa mujibu wa hukumu ya mahakama.

Baada ya fedha hizo kuchotwa kibabe na TRA, Shule za Mt. Jude zilibakiza Sh. 5,777,658 za kitanzania pekee, wakati ambapo bajeti ya kuendesha shule kwa siku moja ni shilingi 35,229,752 za kitanzania. Hivyo, fedha iliyobaki ni sawa na asilimia 16 ya bajeti ya kawaida, jambo ambalo

ni sawa na kusema kwamba uongozi wa TRA umezifunga shule za Mt. Jude.

Baada ya kuona kwamba ni vigumu kuendesha shule katika mazingira haya, Bodi ya shule za Mt. Jude, iliyokutana mnamo tarehe 13 Novemba 2020 iliamua kwamba, wanafunzi wote wa shule ya msingi warudishwe nyumbani; kwamba, wanafunzi wote wa Kidato cha nne warudi nyumbani tarehe 8 Desemba, mara tu baada ya kumaliza mitihani yao ya Taifa; kwamba, wanafunzi wa kidato cha sita wanaotegemea kufanya mitihani yao ya majaribio ya mkoa (mock exams) hivi karibuni warudi nyumbani tarehe 14 Desemba 2020 mara tu baada ya kumaliza mitihani hiyo; na kwamba, wanafunzi wengine wote ambao hawana mitihani warudi nyumbani ifikapo tarehe 18 Novemba 2020.

Aidha, bodi ya shule ilifanya uamuzi kuhusu hatma ya wafanyakazi 307 wa shule hiyo. Bodi iliamua kwamba, wafanyakazi 199 wapewe likizo bila malipo kabla ya mwezi wa Disemba; kwamba, wafanyakazi 101 wapunguzwe kwa kunyimwa mikataba mipya mara tu baada ya mikataba yao ya sasa kufikia mwisho; na kwamba, wafanyakazi 62 wabaki shuleni kuendelea na majukumu yaliyo muhimu na lazima.

Uamuzi wa bodi ya shule hayakuishia hapo; wahitimu 116 wa kidato cha sita wanaojitolea kufundisha masomo mbalimbali kwenye shule 34 za serikali, pia walipewa likizo bila malipo. Kadhalika, malipo ya shilingi 68,997,205 kwa watoa huduma zaidi ya 50 kwa mwezi wa Oktoba na Novemba 2020 yalisimamishwa.

Pia, misaada mikubwa zaidi ya elimu, kama vile chakula, sabuni na vifaa vingine muhimu kwa wanafunzi maalum 90 wanaohudumiwa wanapokuwa nyumbani wakati wa likizo, na ambayo ilipaswa kutolewa mwishoni mwa mwaka huu, imesimamishwa.

Vile vile, marupurupu ya wafanyakazi 101 waliopunguzwa kwa kunyimwa mikataba mipya yamesitishwa hadi hapo shule itakapokuwa na fedha.

Na mwisho, Bodi ya shule iliamua kwamba, endapo TRA hawatarudisha fedha hizo na kuacha kuitaka shule ilipe kodi inayotozwa kwenye mapato ya taasisi inayofanya biashara (corporate tax), wakati shule hii haifanyi biashara, wanafunzi 340 waliokuwa wamechaguliwa kutoka kwenye shule za serikali ili wajiunge na shule za Mt. Jude mnamo Januari 2021, hawatapata fursa ya kusoma shuleni hapo wala kupewa ufadhili kwa sababu shule za Mt. Jude zitafungwa kabisa.

Uamuzi huu juu ya uwezekano wa kufungwa kwa shule unaunga mkono msimamo wa taasisi ambayo ni mfadhili mkuu wa shule. Shule za St. Jude za Arusha ni mradi unaofadhiliwa na asasi ya kutoa huduma zenye msingi wake katika ukarimu (charity organisation) iitwayo “The East African Fund Limited,” iliyosajiliwa nchini Australia na kupewa cheti cha usajili chenye namba CFN 1612. Wafadhili hawa wanaunga mkono bajeti ya mwaka ya shule kwa asilimia 90. Bajeti ya shule kwa mwaka ni Sh. 12,682,710,722.

Mnamo tarehe 4 Novemba 2020, Mwenyekiti wa Bodi ya wafadhili hawa, aliandika barua kuujulisha uongozi wa shule za Mt. Jude za Arusha kuwa wao hawako tayari kutuma fedha

zozote za ufadhili ambazo zinakusanywa kama zawadi na michango ya wasamaria wema,  halafu fedha hiyo itumike kulipa serikalini kana kwamba shule ya Mt. Jude ni kampuni inayofanya biashara, kupata faida na kugawana faida.

Kwa sababu hizi zote, taarifa ya shule iliyotolewa baada ya uvamizi wa TRA inabainisha kuwa, uamuzi wa TRA kuingilia akaunti za shule kwa nguvu, utaathiri moja kwa moja uhai na ubora wa shule tatu za Mt. Jude, na kuathiri kwa njia ya mzunguko uhai na ubora wa sekta ya elimu kwa ujumla, kwa njia mbalimbali.

Wasifu na shule za Mt. Jude

Shule ya Mt. Jude ilisajiliwa na serikali kupitia BRELA kama kampuni isiyo na mtaji wa biashara tangu mwaka 2002, baada ya raia wa Australian Gemma Sisia kuona kwamba elimu bora inayotolewa bure kwa watoto maskini wenye vipaji ndiyo dawa ya kutibu umaskini katika Afrika inayoshirikiana na ulimwengu wa nje. 

Shule za Mt. Jude zinayo miundombinu bora ya kielimu iliyotawanyika kwenye kampasi tatu. Shule inatoa elimu ya bure kwa watoto wenye vipaji na wanaotoka katika familia maskini mkoani Arusha. Kuna wanafunzi wa darasa la kwanza mpaka kidato cha sita. 

Kuna kampasi ya shule ya msingi, kituo cha wageni wa kimataifa, na jengo la utawala kwenye kijiji cha Mshono; mabweni kwa ajili ya wanafunzi wa shule ya msingi kwenye kijiji cha Moivoro; kampasi ya sekondari iliyo na mabweni yake iliyoko eneo la Usa River. Shule inayo mabasi 27 kwa ajili ya wanafunzi wa kutwa, maktaba mbili zenye vitabu zaidi ya 30,000, CD na DVD. Kuna maabara za sayansi, viwanja vya michezo, maabara ya kompyuta na chumba cha vifaa vya michezo.

Watoto wote hupaya chakula cha mchana shuleni. Wanafunzi wa bweni hupata kifungua kinywa na chakula cha jioni pia. Kwa wastani shule inatoa milo milioni moja kwa mwaka. Kuna waajiriwa wapatao 300 na wageni kadhaa wanaojitolewa. Asilimia 96 ya watoto wote shuleni hapo wanapatikana kutoka kwenye familia maskini wilayani Arusha, baada ya mchujo makini, na wanalipiwa gharama zote za elimu.

Mbali na kulipa gharama zote za elimu kwa watoto wapatao 2000 wanaotoka kwenye familia maskini, shule hii pia hutoa misaada kwa wanafunzi 326 walio kwenye vyuo 53 vilivyoko sehemu mbalimbali duniani, ikiwemo Tanzania.

Aidha, shule hii inayo program inayohusisha wahitimu 116 wa kidato cha sita wanaojitolea kufundisha masomo mbalimbali kwenye shule 34 za serikali. Wahitimu hawa hupewa fedha ya kujikimu shillingi 170,000 kila mmoja kwa mwezi, kwa ajili ya chakula na usafiri. Sasa wote wamepewa likizo bila malipo.

Kwa ajili ya kuendesha program hizi, bajeti ya shule ya kila siku ni shilingi 35,229,752 za kitanzania; bajeti ya mwezi ni shillingi 1,056,892,560 za kitanzania; na bajeti ya mwaka ni shilingi 12,682,710,722.

Kwa mujibu wa tovuti yake, shule ya Mt. Jude inamilikiwa ni Kampuni yenye Wakurugenzi tisa walio katika Bodi ya shule. Hao ni Gemma Sisia, Padre Festus Mangwangi, Dkt. Richard Masika, Profesa Patrick Ndakidemi, Bibiana Mardai, Mary Maeda, Nicholaus Duhia, Modest Akida, na Mark Cubit.

Like
1