ELIMU kuhusu Sheria ya Ununuzi wa Umma (PPRA) No 10. ya mwaka 2023 inayozielekeza halmashauri nchini kutenga asilimia 30 ya zabuni zake kwa ajili ya makundi maalum bado ni changangamoto kwenye Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani.
Pia ukosefu wa elimu ya Mfumo wa Kitaifa wa ununuzi serikalini (NeST) kwa makundi maalum unavifanya kukosa fursa za kuomba zabuni zinazotolewa na halmashauri, hivyo kushindwa kujikwamua kiuchumi kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na manispaa yao.
Sheria hiyo sambamba na kanuni zake imeainishwa kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Sheria N0 10 ya mwaka 2023 kupitia kifungu cha 64 (1-2)c inaweka sharti kwamba asilimia 30 ya kila manunuzi yanayofanywa na taasisi zake zifanywe na vikundi vya wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu.

Uchunguzi uliofanywa na SAUTI KUBWA katika mitaa ya Vikawe Shule, Vikawe Bondeni, Mailimoja B, Tangini na Kongowe Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani, umebaini wananchi wengi kupitia vikundi mbalimbali vya ujasiliamali hawana taarifa ya kuwapo kwa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 kifungu cha 64 (1-2)c.
Vikundi vinne vya ujasiliamali kati ya vitano nilivyozungumza navyo kwenye mitaa tofauti, vinne havina taarifa yoyote kuhusu fursa zinazopatikana kupitia zabuni za manispaa ya Kibaha.
Mwanaisha Salum Magomba, anamiliki duka la vifaa vya maofisni Mtaa wa Vikawe bondeni, anasema hajui nikwa vipi anaweza kunufaika na Sheria ya Ununuzi wa Umma kwenye eneo lake. Anasema ingawa yupo kwenye kikundi cha wanawake wajasiliamali kiitwacho ‘Vikawe Tujitambue’, lakini hawajui kama kuna fursa zinazopatikana kupitia zabuni za manispaa yao.
“Mwanaisha ambaye amesema ni muhitimu wa chuo cha ukunga huko Kigoma, anaiomba serikali kupitia PPRA kuweka utaratibu wa kuwafikia wajasiliamali wa mtaani kuwapa elimu ya matumizi ya NeST ili waweze kujaribu bahati yao.
“Nimekuwa nikisikia suala la manunuzi, najua linahusu makampuni makubwa ya ujenzi wa miundombinu kwenye miradi mikubwa, sijui sisi wa chini tunafikiwaje, huo mfumo wa NeST ndiyo kwanza nasikia kwako.” anasema Mwanaisha.
Mwenyekiti wa Kikundi cha wajasiliamali wa Mtaa wa Vikawe shule cha ‘Familia moja’, Meshak Mgaya anasema kikundi chao kimepata usajiri na kinajihusisha na kazi za mapambo, kukodisha turubahi na viti kwenye shughuli mbalimbali za kijamii, lakini suala kuhusu zabuni za manispaa ya mifumo mingine hawazifahamu.
“Kikundi chetu kina wanachama 45, tunachokifahamu ni ile mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri, na tayari tumenufaika nayo, lakini kuhusu zabuni hilo ni jambo geni sana kwetu, ni vema wahusika waje watuelimishe ili tuone namna ya kushiriki” alisema Mgaya.
Mgaya ambaye pia ni mjumbe wa serikali ya mtaa huo wa Vikawe, anasema elimu kuhusu Sheria ya Manunuzi ya Umma No 10 ya mwaka 2023 inayoweka sharti la kutengwa kwa asilimia 30 ya zabuni kwa ajili ya makundi maalum bado haijawafikia wananchi wakiwamo viongozi wanaounda kamati ya uongozi wa mtaa.
Mgaya alitolea mfano, mradi wa ujenzi wa tenki la maji uliopo kwenye mtaa huo, kwamba ulitekelezwa na serikali mwaka 2019 hadi 2021 na vijana wa mtaa huo walishiriki kwenye shughuli za ulinzi wa vifaa na uchimbaji mitaro kwa mtu mojamoja na sio kama kikundi.
Hata hivyo, alisema kwa upande wa wanawake wanaofanya biashara ya mama lishe mradi huo haukuwaendea vizuri kwani walidhulumiwa fedha zao.
“Kwa mfano, hapa ofisini tulipokea malalamiko, mama lishe waliokuwa wanahudumia chakula kwenye mradi huo wa maji hawakulipwa ujira wao, kuna watu walikimbia na fedha zao. “alisema Mgaya.
Aidha Mwenyekiti wa Mtaa wa Vikawe Shule, Kata ya Pangani Manispaa ya Kibaha, Shabani Shabani ameiambia SAUTI KUBWA kuwa hakuna tenda yoyote imewahi kutolewa kwenye mtaa wake kwa makundi maalum, isipokuwa mradi ukitokea vijana huwa wanapewa kazi ndogondogo kwa wale wanaohitaji tu.
Akitolea mfano, alisema zahanati iliyojengwa Mtaa wa Kidimu Kata ya Pangani, mkandarasi alitoka halmashauri na vijana walichukuliwa kama vibarua wa kusaidizi mafundi kwa mtu mmoja mmoja sio kama kikundi rasmi.
Kuhusu watu wenye ulemavu, alisema hana taarifa za kuwapo kikundi cha aina hiyo tofauti na vikundi vingine vya wajasiliamali.
“Zahanati mpya iliyojengwa Mtaa wa Kidimu, Kata ya Pangani ilijumuisha nguvukazi kutoka kata nzima, mkandarasi alitoka manispaa, lakini vijana na akina mama walishirikishwa kama mtu mmoja mmoja na sio kikundi.” alisema Shabani.
Mtendaji wa Kata ya Tangini Manispaa ya Kibaha, Idd Hassan anasema hafahamu chochote kuhusu sheria ya Ununuzi wa Umma ya 2023 inayohusu asilimia 30 ya zabuni zote kutengwa kwa ajili ya makundi maalumu.
Anasema hata kama sheria hiyo imetungwa na kupitishwa bungeni na kuanza kutumika, yeye binafsi haijui na anaamini hata wananchi wa kawaida hawaijui, hivyo hawawezi kunufaika nayo kwa namna yoyote.
“Sheria hiyo ya asilimia 30 kutakiwa kuyafikia makundi maalum, hata kama imepitishwa, kutungwa na Bunge na baadaye kuanza kutumika, ni wazi baadhi ya wananchi kwenye mtaa ninaouongoza hawaijui hivyo fursa ni bora elimu iwe inatolewa mapema.

Pia Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mailimoja B, Shauri Yombayomba. Yeye anasema hafahamu chochote kuhusu kutengwa kwa asilimia 30 ya miradi yote ya ununuzi kwa ajili ya makundi ya wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu kwa kila zabuni inayotolewa kwenye manispaa yao.
Anashauri sheria au miongozo yoyote inayogusa moja kwa moja maslahi ya wananchi ikishapitishwa bungeni basi iende sambamba na utoaji wa elimu kwa wananchi kupitia kwa viongozi wao, vinginevyo fursa kama hizo za kupunguza umasikini na ustawi wa jamii watazikosa.
“Kama unavyosema kuna sheria ya ununuzi wa umma ianyotaka itengwe asilimia 30 kwa ajili ya makundi maaalum, sheria hiyo hata kama imepitishwa na bunge na imeanza kutumikaa, sisi viongozi wa chini hatuna taarifa nayo.
“Ni vema sheria kama hizo zikishapitishwa bungeni, ziende sambamba na elimu iwafikie viongozi ili nao waishushe moja kwa moja kwa wananchi” alisema Yombayomba.
Walionufaika
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kongowe, Hamis Shomari anasema Manispaa ya Kibaha imeanza kutekeleza Sheria No. 10 ya mwaka 2023 kifungu cha 64 (1-2)c. huku akisisitiza kuwa jambo hilo nila lazima kwenye manispaa hiyo na tayari limeanza kulitekeleza kwa vitendo.
Shomari anatolea mfano kuwa mwaka jana 2025 kikundi cha vijana cha Picha ya ndege kijulikanacho kama ‘Vijana Family group’ kilishinda zabuni ya kusambaza vifaa vya ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa katika Shule ya Sekondari Mwamsisi Forest iliyopo Manispaa ya Kibaha.
Ingawa amesema hajui thamani ya vifaa hivyo kwa ujumla wake, lakini mradi mzima wa vyumba hivyo vya madarasa manne ilikuwa ni shilingi milioni 88 na vilikamilika kwa ufanisi mkubwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kikundi cha Vijana Family group, Jackson Msimbe amesema walifanikiwa kupata tenda hiyo baada ya kuomba tenda ya kusambaza vifaa vya ujenzi wa madarasa manne kupitia Mfumo wa Ununuzi wa kitaifa wa serikali (NeST).
Anavitaja vifaa hivyo kuwa ni pamoja na kokoto, kifusi, mchanga msafi, simenti na tofali.
Msimbe ambaye ni mchumi kitaaluma, anasema semina ya Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA) iliyofanyika Januari mwaka huu mkoani humo kupitia Ofisi ya Maendeleo ya jamii ya halmashauri hiyo, imewafungua macho zaidi kuhusu Sheria ya Ununuzi wa Umma N0. 10. 2023 inayozilazimisha hamlashauri zote nchini kutenga asilimia 30 ya zabuni kwa makundi maalum.
“Januari mwaka huu tulipata semina ya PPRA ambao walisema mradi kwenye halmashauri, shairti utenge asilimia 30 kwa jili ya vikundi maalulm vya wajasiliamali wadogo. Awali hatukujua kama tunapaswa kutengewa kiwango hicho cha zabuni. Sharti hilo ni muhimu kuzingatiwa kwa sababu sisi wajasiliamali wadogo hatuna mitaji ya kushindana na matajiri wazoefu wenye mitaji.
“Tunajua lengo la serikali ni kurudisha fedha kwenye mzunguko wa jamii na kuinua uchumi, hivyo elimu zaidi itolewe kwa wananchi na vikundi hivi vidogo tuweze kupata zabuni kwenye taasisi na mashirika ya serikali kama vile Tanesco, TRA, Tanroads, Tarura na kwingineko.”anasema mjasiliamali huyo.
Ofisa Maendeleo ya Kata ya Pangani, Rose Ngalai alipoulizwa kuhusu mwitikio wa jamii katika kusajiri vikundi kwenye kata yake, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo mpaka apate kibali kutoka kwa mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha.

Wakati hali ikiwa hivyo, ripoti ya Ukaguzi na utendaji wa PPRA mwaka 2020/21 utengaji wa asilimia 30 ya bajeti ya manunuzi kwa ajili ya makundi maalum haikutekelezwa ipasavyo. Ripoti hiyi inasema kati ya taasisi 86 zilizofanyiwa tathmini, ni mbili tu zilizingatia mataka ya sheria huku zilizobaki zikiwa hazikuitekeleza kabisa.
Sheria ya Ununuzi ya Umma ya mwaka 2023 (PPA 2023) na kanuni zake za mwaka 2024 zinaelekeza upendeleo wa pekee kwa makundi maalum, ambapo taasisi zote za ununuzi zinapaswa kutenga asilimia 30 kila mwaka kwa ajili ya wanawake, vijana, wazee, na watu wenye ulemavu.
Mgawanyo huo unapaswa kutenga asilimia 10 kwa watu wenye ulemavu, 10 kwa vijana, 5 kwa wanawake, asilimia 5 kwa wazee na vikundi lazima visajiliwe na SGSE na kuingizwa kwenye mfumo wa NeST ili kushiriki. Na sifa nyingine ya kikundi kushiriki fursa hizo ni lazima kiwe kimesajiliwa na mamlaka inayosaidia makundi maalum (SGSE) ikiwemo SIDO au VETA na kuingizwa kwenye kanzidata ya PPRA.
Aidha kwa mujibu wa sheria hiyo, upendeleo huu hukoma pindi kikundi kinapofikisha mikataba ya thamani ya shilingi bilioni moja.
Walati elimu ya mifumo ya ununuzi ikionekana bad oni changamoto, taarifa ya PPRA ya mwaka 2024 inaonyesha mafanikio makubwa kupitia mfumo wa (NeST), ambapo inasema tangu kuanza kwake, zabuni zenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 5.29 (sawa na watani wa shilingi bil. 1.3) zilitolewa kwa makundi maalum ya wanawake, vijana, wazee, na watu wenye ulemavu.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa katika kipindi cha hivi karibuni, matumizi ya teknolojia yamepunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa (CO2) kwa kiasi cha tani 617.85 ndani ya mwaka mmoja kutokana na kuacha kutumia makaratasi na wino.







