Vita dhidi ya ufisadi: Magufuli awakingia kifua vigogo, maswahiba

Lugumi - File photo

VITA dhidi ya ufisadi ambayo Rais John Magufuli amekuwa anajitapa nayo, imeingia dosari baada ya kubainika kuwa ukali wake unaelekezwa kwa baadhi ya watu huku akikwepa kugusa wengine.

Baadhi ya wachambuzi wanasema Magufuli anabagua yupi wa kukamata, yupi wa kufilisi na yupi wa kufikisha mahakamani.

Kwa miaka mitano aliyokaa madarakani tangu 2015, Magufuli amenusuru baadhi ya mafisadi wakuu wanaotuhumiwa kufisidi nchi kupitia idara na taasisi kadhaa za serikali.

Hata “mahakama ya mafisadi” iliyoanzishwa kisiasa ili kuonyesha dunia kuwa alikuwa anadhamiria kuchukua hatua kali dhidi ya watuhumiwa wa aina hiyo ili kuharakisha hukumu dhidi yao. Hata hivyo, hadi leo imehusika na uamuzi wa watuhumiwa watu wachache, ambao, hata hivyo, si majina makubwa ambayo yamekuwa yakihusishwa na miradi minono kwa njia za kifisadi – tena wahusika wakisaidiana na baadhi ya viongozi wa serikali wasiokuwa waaminifu.

Tangu mahakama hiyo ya mafisadi ianzishwe mwaka 2016 jumla ya kesi za uhujumu uchumi 119 zimesajiliwa na 90 zimemalizika kwa kutolewa hukumu mbalimbali ikiwamo vifungo na faini.

Mmoja wa maofisa wa ofisi ya msajili wa mahakama hiyo, Dar es Salaam, amesema kuwa hadi mwishoni mwa mwaka jana, zaidi ya Sh. bilioni 44.2 zimekusanywa na serikali, kupitia uamuzi wa mahakama hiyo ikiwani ni faini na fidia kutoka kwa watuhumiwa wa uhujumu uchumi.

Huku akiomba kutotajwa jina kwenye chombo cha habari, ofisa huo alisema; “waliofikishwa hapa na kusajiliwa mashauri yao, hawana majina makubwa na hawajulikani sana, lakini wengi wao ndiyo hao walikutwa na hatia na kuamriwa kulipa fidia na faini kwa makosa yao.”

Rais Magufuli anawaogopa hawa

Pamoja na kuwepo kwa mahakana hiyo na mahakama nyingine, sambamba na tambo na ukali wa Rais Magufuli, bado wapo wananchi wawili waliokwapua kifisadi zaidi ya Sh. bilioni 74, “hawagusiki.”

 Taarifa za kiuchunguzi zinaeleza kuwa watu hao licha ya kuhojiwa na vyombo vya ulinzi na usalama kwa zaidi ya mara tano (kila mmoja) hawawezi kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kuwa walifanya ufisadi huo kwa kushirikiana na baadhi ya vigogo waliokuwa ndani ya serikali iliyopita.

Uchunguzi wa SAUTI KUBWA umebaini kuwa watu hao wawili, Said Lugumi ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Lugumi Enterprises na Angela Kizigha, mmiliki wa Daissy General Traders zote za Dar es Salaam, wameelekezwa na baadhi ya viongozi wa taasisi za uchunguzi na usalama, “kujificha” na kutopiga kelele kwa muda. Angela Kizigha aliwahi kuwa Mbunge wa Afrika Mashariki.

Chanzo cha habari kimedokeza: “Angela na Lugumi ni kweli wamehojiwa mara kadhaa lakini kuna maelekezo kutoka juu yaliyotutaka kuchukua taarifa zao na kupeleka majalada yao huko kwa wakubwa.”

Uchunguzi wetu umebaini kwamba Angela aliagizwa kutojichanganya zaidi mitaani na kuepuka kunaswa na vyombo vya habari, masharti ambayo pia alipewa Lugumi.

Tulipofuatilia kutaka kujua kama anayewalinda watu hawa ni Rais Magufuli, chanzo chetu kilidokeza kuwa; “Mimi sijui, lakini elewa kuwa wametakiwa kutoonekana kwenye kadamnasi mpaka hali itakapopoa.”

Uhusiano na vigogo

Taarifa zinaonyesha kuwa Said Lugumi amekuwa rafiki mkubwa wa Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete na kwamba ni mshirika wake kibiashara katika kampuni ya Lugumi.

Ridhiwani, ambaye pia ni mtoto wa Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete, anatajwa na vyanzo vyeu kwamba ndiye alikuwa “mchora ramani” wa shughuli nyingi za kampuni hiyo iliyokuwa na ofisi zake katika jengo la ATCL, Mtaa wa Ohio na Garden, Dar es Salaam.

Inadaiwa kuwa Ridhiwani ndiye alikuwa akifanya ‘michongo’ mingi kwa kuunganisha kampuni yao na viongozi wa taasisi za serikali ili kupata zabuni na hatimaye kulipwa fedha nyingi, zikiwamo zile za ujanjaujanja.

Inaelezwa kwamba Lugumi asingeweza kufanya mawasiliano na kampuni za nje au hata kuandika mikataba, mingi ikiwa kwa lugha ya Kiingereza, kwa kuwa ni mhitimu wa darasa la saba tu. Ridhiwani ni mwanasheria mweye shahada mbili.

Alipoulizwa kwa njia ya simu kama kampuni yao bado ipo na inaendelea na kazi zake, Ridhiwani alijibu kwa kifupi, “siijui, wala sihusiki nayo, mniache nitumikie wananchi.” Akakata simu.

Mbali na Ridhiwani, pia zipo taarifa kwamba Lugumi ni mkwe katika familia ya aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, ambaye kwa sasa ni mstaafu.

Kama ilivyokuwa kwa Lugumi, Angela naye anaelezwa kuwa na uhusiano wa karibu zaidi na Mwema, Ridhiwani na aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa makosa ya jinai (DCI), Robert Manumba, pamoja na maofisa kadhaa wa ofisi ya Hazina.

Simu za Angela na Lugumi hazikupokelewa; na hata ulipopelekwa ujumbe wa maandishi, haukujibiwa. Ujumbe wa WhatsApp, licha ya kuonyesha umesomwa na wahusika kwa kuwa na alama mbili za vyema za bluu, lakini hakuna majibu yaliyorejeshwa.

 Lugumi ajichimbia kijijini, Angela yupo Dar es Salaam

Angela Kizigha

Imebainika, kwa sasa Lugumi ameweka makazi yake wilayani Magu, Mwanza, wakati Angela “amejifungia” nyumbani kwake Kijitonyama, Dar es Salaam.

Watanzania hawa wawili tu katika kipindi cha miaka miaka minne, 2014-15 na 2011-12 wanadaiwa kukwapua, kwa manufaa binafsi na washirika wao na baadhi ya wakubwa serikalini, kiasi hicho kikubwa cha fedha kwa njia ya udanganyifu wa kuhudumia zabuni katika Jeshi la Polisi.

 Pesa wanazotuhumiwa kukwapua zingesaidiaje taifa?

Kiasi cha fedha kinachoelezwa kwa ushahidi wa nyaraka na rekodi mbalimbali zilizoko mikononi mwa vyombo vya usalama ni takribani 74,000,000,000 (Sh. bilioni 74).

Endapo kingetumika leo wa ajili ya maendeleo, kingeweza – kwa mfano – kununua magari ya wagonjwa 1,121 na kuyasambaza kila hospitali za rufaa, za mikoa na wilaya; na mengine yangebaki kwa ajili ya zahanati na vituo vya afya.

Tanzania ina jumla ya hospitali 320; zikiwamo za serikali, binafsi na taasisi za dini na mashirika. Gari moja la wagonjwa la kisasa aina ya YinHe kutoka China au Ford Galaxy huuzwa kwa takribani Tsh. milioni 66.

Fedha hizo, endapo zingeingizwa katika mfumo na mzunguko rasmi wa serikali, zingeweza kuhudumia bajeti ya wizara mbili na kiasi kingine kingebaki kwa ajili ya shughuli nyingine za maendeleo na kupambana na umasikini wa Watanzania.

Katika bajeti ya Serikali ya 2020/21, iliyosomwa Bungeni Dodoma mwaka jana, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, imepanga kutumia Sh. bilioni 40.2, huku Wizara ya Muungano na Mazingira ikipanga  kutumia Sh. bilioni 27.9, fedha hizi zikijumulishwa, zinafikia kiasi cha Sh. bilioni  68.1. Fedha hizi ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo na mengineyo, ikiwa ni pamoja na mishahara ya wafanyakazi wanaofikia 234 wa wizara hizo kwa mwaka mzima.

Fedha hizo pia zingeweza kujenga barabara ya kilometa nane, na kuhudumia idadi kubwa ya watu, lakini ziliishia kufaidisha familia chache zisizozidi sita, zikiwamo za maofisa kutoka Hazina, Wizara ya Mambo ya Ndani, Jeshi la Polisi na Idara moja nyingine nyeti.

 Pesa ilivyopigwa

Kampuni ya Daissy General Traders ilipewa zabuni za Sh bilioni 40 na kulipwa kiasi chote hata kabla ya kusambaza bidhaa. Ilitakiwa kusambaza kofia, sare na makoti ya mvua kwa Jeshi la Polisi, lakini vifaa hivi havikuwahi kuwafikia Polisi hadi sasa.

 Taarifa za nyaraka mbalimbali zinaonyesha kuwa Juni 19, 2014 serikali iliingia mkataba na Daissy kwa kupata zabuni namba ME.014/PF/2013/2014/G/34-Lot 11 yenye thamani ya Sh. 21,463,750,000. Zabuni hii ilikuwa ni kwa ajili ya sare za polisi na mavazi mengine.

Pia Mei 30, 2015, serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ilipoipatia Daissy zabuni namba ME.014/PF/2013/2014/G/3I-Lot 1 yenye thamani ya Sh. 716,614, kwa ajili ya sare zinazovaliwa na askari kwa ajili ya sherehe za kitaifa.

Kana kwamba kampui hiyo ina hatimiliki, Juni 12, 2015 ilipata tena “kazi” ya kusambaza sare hizohizo zilizotajwa awali. Safari hii Jeshi la Polisi likitoa hati ya mahitaji (kwa mkataba maalum) Na. MOHA/PF/2014/2015/338 na baadaye kukwekwa kuwa zabuni yenye namba ME.014/PF/2014/2015/G/31-Lot 1 yenye thamani ya Sh 3,524,570,234.

“Bahati” hiyo  kwa Daissy iliendelea ambapo Juni 15, 2015 Jeshi la Polisi lilitoa hati ya mahitaji Na. MOHA/PF/2014/2015/337 na baadaye kuwa zabuni ME.014/PF/2014/2015/G/31-Lot 1 yenye thamani ya Sh 3,524,570,234 kwa kuagiza sare hizohizo.

Hati nyingine ya mahitaji -Na. MOHA/PF/2015/2016/108 ilitolewa Novemba 4, 2015 na Jeshi la Polisi  na baadaye kuwa zabuni ME.014/PF/2015/2016/G/30-Lot 2 yenye thamani ya Sh. 22,918,880,600. Na Novemba 2, 2015 Wizara ya Mambo ya Ndani iliipatia Daissy zabuni namba ME.014/PF/2015/2016/G/30-Lot 2 yenye thamani ya Sh 716,614.

Bahati hiyohiyo ikaiangukia tena Daissy tarehe Mosi, Oktoba, 2015 ambapo ilipata zabuni namba ME.014/PF/2013/2014/G/30-Lot 2 yenye thamani ya Sh. 532,631.

SAUTI KUBWA imeona sehemu ya mikataba hiyo na kwamba mchanganuo wa gharama ambazo kampui hiyo iliweka na hatimaye kukubaliana na kulipa zilikuwa kubwa ikilinganishwa na bei halali za soko kwa wakati huo

Mfano kofia moja nyeusi (Beret), kampuni ya Daissy ilieleza kuwa itaiuzia serikali kwa Sh. 74,340 wakati bei halisi kutoka kiwandani China ambako kampuni ilisema inaagiza ilikuwa ni Sh. 34,200. Pia kampuni hiyo ililipwa Sh. 80,691 kwa kila koti la mvua moja lililoelewa kuagizwa, wakati bei halisi kutoka kiwandani China ilionyesha kuwa ni Sh. 31,000.

Kampuni ya Daissy General Traders inajieleza kuwa na Ofisi Wilaya ya Ilala Mtaa wa Swahili na Uhuru ambayo ilipatiwa leseni ya biashara Julai 21, 2015 namba 01033836 na namba ya ushuru wa mapato 103-758-122.

 Lugumi Enterprises

Kampuni ya Lugumi Enterprises, inadaiwa ilijipatia kwa njia ya udanganyifu Sh bilioni 37 ili kufunga vifaa vya kutambua alama za vidole katika wilaya 108 nchini, lakini kampuni hiyo ilifunga vifaa katika wilaya 12 tu na kubainika kuwa kati ya hizo, ni wilaya nane tu ndiyo zilikuwa zikitumia mfumo huo.

Kupitia mkataba huo wa Julai 18, 2011, ambao SAUTI KUBWA imeona sehemu yake – ME.013/PF/2011.12/G/30 – 2, Kampuni ya Lugumi Enterprises ilipewa zabuni ya kufunga mashine hizo kwa gharama ya Sh bilioni 37, ingawa haikuweza kukamilisha kazi hiyo pamoja na kwamba sehemu kubwa ya fedha hizo zilikwa zimelipwa.

Tayari kampuni hiyo ilipokea Sh bilioni 34 sawa na asilimia 99 ya fedha zote, huku ikiwa imefunga mashine chache katika jiji la Dar es Salaam na kwamba baadhi ya vifaa hivyo vilikuwa havijaanza kufanya kazi kwa maelezo kwamba havikuwa na ubora ulitakiwa.

Like
3