UHUSIANO wa Tanzania na Kenya uliodumu miaka mingi, huenda ukavurugwa na chakula, hasa mahindi ambayo sasa yanadaiwa kuwa na sumu.
Kenya inadai kuwa mahindi kutoka Tanzania hayafai kwa matumizi ya binadamu, kwamba yana sumukuvu iitwayo “aflatoxin).”
Tayari Kamishna wa Forodha wa Mamlaka ya Kodi ya Kenya (KRA), Pamela Ahago, amesitisha kuagizwa kwa mahindi yatokayo Tanzania na Uganda. Serikali hiyo imesema haiwezi tena kuruhusu kuingia kwa nafaka hiyo kwa kuwa imethibitishwa si salama kwa chakula cha binadamu.
Kenya imeeleza kuwa kwa miaka mingi, wakati mahindi yanaingizwa nchini humo kutoka Tanzania, yamechangia kuathiri afya za wananchi wake.
Naibu Waziri wa Kilimo wa Tanzania, Hussein Bashe amesema Tanzania inafuatilia kwa karibu tuhuma hizo za Kenya ili kujua hatma yake.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya miaka 60 sasa, Kenya imekuwa ikitegemea mahindi kutoka Tanzania. Ugali – ambao hutokana na unga wa mahindi – ni chakula kikuu cha Wakenya wengi.
Idadi kubwa ya Watanzania wametumia mitandao ya kijamii kueleza wasiwasi wao kuhusu hatua ya Kenya, huku wakihoji iweje mahindi kutoka Tanzania yaonekane kuwa na sumu na hayafai kuliwa na binadamu, wakati kwa miaka ‘nenda-rudi’ Wakenya wamekuwa wakitumia nafaka hiyo.
“Haya madai ya Kenya kuwa mahindi yetu hayako salama ni danganya toto, waseme sababu zingine, inakuwaje hata kabla ya uhuru wao – mwaka 1962, walikuwa wanachukua mahindi kwetu na hawajaathirika, iweje leo wanasema mahindi ya Tanzania hayafai,” anaandika Lazaro Kilambe katika akaunti yake ya Twitter.
Chama cha ACT-Wazalendo kimejitosha katika mgogoro huu, na tayari kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe, amesema hatua hiyo ya Kenya ni kuvunja itifaki ya soko la pamoja la Afrika Mashariki na kushauri Tanzania ichukue hatua.
Zitto anabainisha kuwepo kwa kiwango cha sumukuvu ambacho hata kama kimo ndani ya mahindi na nafaka zingine, hakiwezi kuathiri afya ya binadamu. Kiwango kinachokubalika kimataifa kuwemo kwa sumukuvu katika nafaka huthibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO).
Mwaka 2017, Tanzania ilizuia wananchi wake kuuza mahindi Kenya, hatua ambayo ilisababisha njaa na taharuki. Ukosefu wa unga wa mahindi nchini humo ulipewa jina la – “sembe crisis” na bei ya nafaka hiyo ilipanda maradufu. Kenya ililazimika kuagiza mahindi kwa bei kubwa kutoka Zambia.
Yapo maoni pia kuwa hatua hii ni moja ya vielelezo vya mgogoro wa chini chini wa kidiplomasia kati ya Kenya na Tanzania ambao umesababishwa na masuala mbalimbali hasa katika utawala wa Rais John Magufuli na Rais Uhuru Kenyatta.
Mwanzoni mwa utawala wa Magufuli, mamlaka za wilaya ya Arumeru mkoani Arusha ziliagiza kutekeketezwa kwa malefu vifaranga vya kuku vya wafanyabiashara wa Kenya vilivyokuwa vinaingizwa Tanzania kupitia mpaka wa Namanga.
Tukio hilo liliibuka husia hasi kidiplomasia na kisiasa, na lilifuatiwa na uchomaji wa mifugo kutoka Tanzania iliyoingizwa nchini Kenya.
Tangu mwaka jana baada ya mlipuko wa virus vya Corona, Tanzania na Kenya zimekuwa katika mzozo wa chini chini kutokana na Tanzania kukataa kutoa taarifa za maambukizi ya Corona kwa kisingizio kuwa “Mungu aliondoa Corona” baada ya ibada ya kitaifa ya siku tatu.
Mzozo huo ulisababisha ndege za Kenya Airways kupigwa marufuku Tanzania, na za Air Tanzania kuzuiwa kutua Kenya; huku Kenya ikiweka pia ulinzi mkali mipakani dhidi ya abiria watokao Tanzania.
Mzozo huo wa awali ulitatuliwa, lakini hatua hii ya Kenya kuzuia biashara ya mahindi kutoka Tanzania inaelekea kurudisha hisia za ugomvi wa kidiplomasia kwa jicho la kibiashara.
Baadhi ya Wakenya wameshtushwa na zuio hili, huku wakidai kuwa ni mbinu ya wakubwa kuingiza shehena zao za mahindi kutoka nchi nyingine ambako wamewekeza.
Baadhi ya maofisa wa serikali ya Tanzania waliozungumza na SAUTI KUBWA wamesema huu ni mzozo wa kidiplomasia unaojitokeza kibiashara, na unatokana na kile wanachoita “uzembe wa wakubwa katika diplomasia za ujirani.”