Asha Abdallah Mussa: Mfano halisi wa mapambano ya mwanamke

ASHA Abdallah Mussa ni mshindi. Miongoni mwa wanachama wenzake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), yeye anatajwa kama mmojawapo wa kinamama waliobwaga wanaume katika mchuano wa kisiasa, hasa katika kura za maoni.

Si msomi. Changamoto za kifamilia zilimzuia kupata kiwango cha elimu aliyotaka. Lakini hicho haikuwa kikwazo cha kumkatisha tamaa katika nia yake kusonga mbele.

Anasema: “Nimeshindwa kuendelea na masomo. Wazazi wangu hawakuwa na elimu, lakini kwenye siasa nawashinda waliosoma.”

Asha alizaliwa mwaka 1981 Kiwengwa, Zanzibar. Alipata elimu yake huko Tanzania Bara, baadaye akarudi Zanzibar na kuendelea na masomo. Bahati mbaya aliishia sekondari.

Hata hivyo, aliendelea kuamini kuwa elimu ni muhimu, na kwamba ukiikosa upande mmoja unaweza kuipata kwingine, kwa namna nyingine. Anaamini kwamba kiwango chochote cha elimu alichonacho mtu yeyote kikitumiwa vema kinaweza kufanya mambo makubwa.

Kwa imani hiyo na ujasiri, Asha amefaulu kutambua karama yake, ikamvusha kutoka mwanachama wa kawaida wa CCM hadi kuwania nafasi za uongozi wa shina, tawi na udiwani.

Mwaka 2010-2015 alikuwa diwani wa Wadi ya Upenja. Mwaka 2015 akawania nafasi ya uwakilishi wa Jimbo Kihengwa akichuana na wanawake wenzake wawili na wanaume wanne.

Mwaka 2020 aliondoka Kiwengwa na kuwania uwakilishi wa Jimbo la Mahonda, wakiwa washindani 15. Miongoni mwao, wanaume walikuwa 12. Aliwashinda.

Anasema mafanikio yake, kwa kiasi kikubwa, yamechangiwa pia na mumewe. “Namshukuru mume wangu kwa kunivumilia. Wakati mwingine shughuli za chama ni za kujitolea mno, hivyo bila ushirikiano kutoka kwake nisingefikia hapa nilipo.” Asha ni mama wa watoto wanne.

Anajivunia mafanikio yake akisema: “Nilitekeleza ahadi nilizozitoa kwenye jimbo langu kwa asilimia 95. Naamini nitafanya vema pia katika jimbo jipya la Mahonda. Ninawashukuru sana TAMWA kwa kunijengea uwezo, na sasa nimekuwa mpambanaji nisiyekubali kushindwa.”

(Asha)

Chapisho hili fupi juu ya Asha ni kwa heshima ya SIKU YA WANAWAKE DUNIANI.

Like
2