CHINA imemweka mtegoni Rais John Magufuli. Taarifa zinasema yupo njiani “kulamba matapishi” yake na kuridhia ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, ambayo aliigomea na kutengua makubaliano ya uendelezwaji wake kwa sababu za kisiasa.
Awali ilikuwa iendelezwe kwa ubia wa kampuni za China na Oman. Rais Magufuli alitengua ujenzi wa bandari hiyo mwaka jana.
Vyanzo vyetu vinasema kuwa maslahi mapya kati ya Magufuli na China yamemfanya anywee, na sasa ameridhia Wachina wapewe tenda ya kuendeleza bandari hiyo kwa makubaliano ya siri, ambayo huenda yanaweka mazingira mengine ya kukubaliana kwa baadhi ya mambo mapya au yaliyokwama.
Awali, wakati anatengua mradi huo, Magufuli alisema kuwa “kichaa tu ndiye anayeweza kukubali masharti ya mradi huo.”
Wakati Magufuli akipinga ujenzi wa mradi huo, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema wanaopinga mradi huo ni sawa na watu wanaoweka “mkokoteni mbele ya farasi” wakitarajia ataukokota.
Taarifa zilizoifikia SAUTI KUBWA zinaeleza kuwa ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, ambaye amewasili nchini Januari 7, 2021 na kufikia Chato, nyumbani kwa Rais Magufuli, ni moja ya mikakati ya nchi hiyo kumshawishi Magufuli arejeshe ujenzi wa bandari hiyo ambayo tayari ilikuwa ianze kujengwa kwa gharama ya Sh. trilioni 23.5 (dola za Marekani bilioni 10).
Mradi huo ulianzishwa na serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete. Serikali ilifunga mkataba na kampuni za China Merchants Holding International ambayo iliridhia mkopo mkubwa – kwa udhamini wa Tanzania kutoka Mfuko wa Taifa wa Akiba ya Fedha wa Oman (SGR), Falme za Kiarabu. Mradi huo ulianza kujadiliwa rasmi mwaka 2013 na ulisainiwa kwa mbwembwe – huko Bagamoyo.
Magufuli alipoingia madarakani mwaka 2015 alisema mradi huo ni wa kinyonyaji, akaagiza usitishwe. Hata hivyo, taarifa zinasema hatua ya Magufuli ilikuwa mkakati wa kujijenga binafsi kisiasa kwa “kumshushua Kikwete” ili kuhadaa umma kuwa anapiga vita ufisadi. Bagamoyo ni bandari ya nyumbani kwa Kikwete.
Hata hivyo, baada ya wananchi na wachambuzi kulalamika kuwa Magufuli anapiga vita mradi huo wakati anahamishia miradi mingi mikubwa nyumbani kwake Chato, sasa amelainika, na ameridhia China ifanye ujenzi wa bandari hiyo., kwa maslahi ambayo wahusika wanasema yatawekwa hadharani baadaye.
Waziri huyo wa mambo ya nje wa China sasa amefikia Chato, mkoani Geita, nyumbani kwa Magufuli, kufanya mazungumzo – yakiwamo ya siri kuhusu mambo mengi ikiwa ni pamoja ma mradi huo wa Bagamoyo.
SAUTI KUBWA inasubiri kujua hatima ya mazungumzo yao. Mmoja wa watoa taarifa amesema makubaliano ya Tanzania na China yatategemea Magufuli ameamkaje, maana yeye huwa hatumii kanuni bali hisia. Akiamka vibaya mradi unakufa, alisema.
“Pamoja na mambo mengine, kuna vitu vikubwa viwili vitazungumzwa huko Chato kati ya bwana mkubwa (Rais Magufuli) na China. Moja ni ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, na jingine ni suala zima la mitaji ya baadhi ya kampuni za China kushikiliwa na serikali kupitia BoT (Benki Kuu ya Tanzania) baada ya benki yao hapa nchini kufungwa,” amesema kingozi mmoja mwandamizi wa serikali aliyeomba asitajwe jina wala cheo.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa mbali na waziri mkuu huyo mwandamizi wa China, pia mwishoni mwa mwezi huu wa Januari, kiongozi mwingine mwadamizi wa China, Wu Peng, anatarajiwa kuwasili nchini kwa ajili ya mashauriano juu ya hatua zaidi juu ya miradi kadhaa ya China ambayo inaelezwa kukwama kutokana na baadhi ya masharti magumu ya Tanzania juu ya wawekezaji wa nchi hiyo. Peng ni mwanadiplomasia anayehusika na masuala ya Afrika anayetajwa kuheshimika zaidi kwa Rais wa China, Xi Jinping.
“Kimsingi, kwa masikitiko makubwa, China ndiye beberu mpya wa Tanzania,” alisema kiongozi huyo.
SAUTI KUBWA imeelezwa kuwa waziri huyo wa mambo ya nje wa China amebeba ujumbe kwa Rais Magufuli kutoka kwa Rais Jinping ukieleza kuwa China iko radhi kusaidia Tanzania – kwa fedha na utaalamu kwa baadhi ya miradi mikubwa ya kimkakati ambayo imekuwa ikisuasua kutokana na serikali kukosa fedha – wakati rais alishatangazia wananchi kuwa, “tunajenga miradi kwa fedha zetu za ndani.”
Rais Magufuli amekuwa ikitamba kujenga miradi hiyo kwa makusanyo ya fedha za ndani, hali ambayo inaonekana sasa kuielema serikali baada ya kuwepo mkwamo wa makusanyo ya kodi.
Wataalamu wa China na Tanzania walianza mazungumzo juu ya miradi hii kuanzia Juni 2012 na makubaliano ya awali yalisainiwa Machi 14, 2013. Makubaliano ya kimkakati yalisainiwa Desemba 2013. Makubaliano ya kuanza utekelezaji yalisainiwa Oktoba 2015 na jiwe la msingi la kuanza ujenzi liliwekwa mwaka huo.
Katika miaka mitano ya kwanza ya utawala wake, Magufuli amekuwa akikosoa baadhi ya mipango na miradi ya mtangulizi wake, Kikwete, huku akidhani ingemsaidia kujitafutia uhalali na umaarufu wa kisiasa. Miongoni mwa miradi anayoikosoa zaidi ni huo wa Bagamoyo (ambao sasa unajadiliwa na Wachina) na ule wa gesi asilia Mtwara, uliokuwa ukihusisha pia kuzalsiha mitungi ya gesi na kusafirisha nje ya nchi, ambao sasa umesitishwa.
Bahati mbaya, jitihada hizi hazikumsaidia kupata umaarufu kutokana na aina ya siasa alizoasisi, za ukatili na mateso kwa raia wa makundi mbalimbali ambao hawaoni nafuu ya maisha chini ya utawaka wake.
Hatua ya serikali yake kubeza na kuvuruga mradi wa Bandari ya Bagamoyo (nyumbani kwa Kikwete) huku ikipeleka miradi ya mabilioni Chato (nyumbani kwa Magufuli), imesababisha wananchi wengi kumtazama Magufuli kama “fisadi mwenye fitina na wivu” dhidi ya mtangulizi wake.
Licha ya udhaifu wa Kikwete wa kiuongozi kwa miaka 10 katika maeneo kadhaa, hakujipendelea kwa miradi mingi ya kimkakati kama Magufuli alivyofanya katika miaka mitano tu ya awali.
Kiongozi mmoja mstaafu ameiambia SAUTI KUBWA: “Miaka mitano ya kwanza ya Magufuli imedhihirisha kuwa marais wote waliomtangulia walikuwa waadilifu.”