Serikali yampa Musiba “talaka mbili” kwa kukosea kazi aliyopewa dhidi ya wakosoaji wa Rais Magufuli

Cyprian Musiba- file photo

VYOMBO vya habari vilivyoanzishwa na dola kimkakati kwa ajili ya kushambulia, kutukana, kudhalilisha na kudhihaki wakosoaji wa Rais John Magufuli, viko mbioni kufungwa baada ya “kumaliza kazi,” SAUTI KUBWA imefahamishwa.

Tayari dola imeanza kujiondoa taratibu kwa kupunguza pesa ambazo ilikuwa inavifadhili, na sasa imevitaka vijiendeshe au vife, baada ya taarifa za kikachero kubaini kuwa hata kazi yenyewe ambayo vilipewa havikuifanya kwa weledi. Watoa taarifa wanasema dola imegundua kuwa vyombo hivyo vilichangia kuongeza chuki ya wananchi dhidi ya Rais Magufuli.

Vyombo hivyo pia vilisababisha chuki ya chini chini ya wanatasnia ya habari dhidi ya serikali, kwani kiwango cha uandishi wa habari cha vyombo hivyo, kwa mantiki na lugha inayotumika, kinadhalilisha taaluma ya habari ambayo vyombo makini vimekuwa vinaitetea kwa vitendo huku vikikabiliana na rungu la serikali.

Wakati serikali imekuwa inachukua hatua kali dhidi ya magazeti makini, hata kwa kuonea baadhi yao, imekuwa inafumbia macho makosa ya wazi ya “vyombo hivyo vya kimkakati.”

Vyombo hivyo ni pamoja na magazeti yajulikanayo kama Fahari Yetu na Tanzanite, Tanzania Perspective na televisheni-mtandao ya Tanzanite TV ambavyo vilisajiliwa kama mali za mtu binafsi – Cyprian Musiba – ambaye dola imekuwa inamtumia na kumlipa huku akijitambulisha kama mwanaharakati huru wa kumtetea Rais Magufuli.

Katika uchaguzi mkuu 2020, Musiba alitia nia ya kugombea ubunge wa Jimbo la Mwibara, akaangushwa katika kura za maoni. Matarajio yake kuwa Rais Magufuli angemkumbuka na kumpitisha kama walivyofanyiwa akina Askofu Josephat Gwajima, Patrobas Katambi na David Silinde – waliopata kura ndogo za maoni lakini wakabebwa – yaliyeyuka.

Wajuzi wa masuala haya katika duru za kikachero nchini wameiambia SAUTI KUBWA kuwa hata kabla ya dola kufikiria hatua hii, Rais Magufuli amekuwa anahoji mara baada ya uchaguzi mkuu, “kwanini wananchi wananichukia wakati nimefanya mambo mengi makubwa ndani ya muda mfupi?” Moja ya sababu zinazotajwa kuamsha chuki ya umma dhidi ya Rais Magufuli ni “kazi chafu za watu kama Musiba na Paul Makonda.”

Taarifa za uhakika zilizopatikana kutoka ofisi nyeti za serikali – ikiwamo Idara ya Habari (MAELEZO) – zinaeleza kuwa bajeti iliyokuwa imepangwa kwa ajili ya kazi hiyo inaelekea kuisha na hakuna dalili ya kuongezwa.

Mbali na kushambulia wakosoaji wa rais, kazi nyingine kubwa ya vyombo hivyo imekuwa ni kumtukuza rais na kumsifu, hata kwa kutangaza uwongo kwa jina lake hasa kuhusu mafanikio ya serikali, shabaha ikiwa ni kuhadaa jamii na kumfurahisha rais.

Tayari baadhi ya vyombo hivyo vimeanza kupunguza wafanyakazi, na wengine wamejiondoa baada ya kupewa taarifa za kupunguzwa mishahara au kutumika bila malipo ya uhakika, hasa kwa kutegemea posho tu.

SAUTI KUBWA ina taarifa kuwa wafanyakazi watatu kati ya wanne waliokuwa wakiendesha Tanzanite TV, wameondoka na sasa televisheni hiyo ya mtandaoni inasimamiwa na mtu mmoja tu.

Miongoni mwa waandishi wa magazeti hayo, waliokuwa wanafikia 23 – katika ofisi zake Dar es Salaam – waliokuwa wakilipwa mishahara kati ya Sh. 500,000 hadi 700,000 kwa mwezi, wanane tayari wameondoka, na waliobaki wameambiwa kuwa watapokea Sh. 350,000 kwa mwezi.

Uchunguzi wa SAUTI KUBWA umebaini kuwa, tofauti na vyombo vingine vyote, magazeti hayo yamekuwa yakichapwa na mitambo ya serikali na kupewa bajeti ya kusafirisha na gharama nyingine zinazofikia Sh. 15,000,000 kila mwezi. Sasa fedha hiyo itapunguzwa hadi Sh. 5,000,000. Gharama hizi ni nje ya mishahara ya watendaji wake.

Inaelezwa kuwa tarehe 12 Desemba 2020, Musiba alikuwa na kikao na baadhi ya wafanyakazi akawaeleza hali halisi ya biashara na utendaji kazi wa vyombo hivyo vya kimkakati, huku akieleza kwamba, “mfadhili anajiandaa kutuacha tujitegemee.”

Musiba alisema kuwa ofisi imelazimika kupunguza wafanyakazi na kubakiza wachache ili kuvinusuru visifungwe kabisa kwa kushindwa kujiendesha kibiashara.

Hata hivyo, SAUTI KUBWA inazo taarifa za uhakika kuwa magazeti hayo ya kimkakati hayakuhitaji kuuzwa kwani gharama zote – zikiwamo za kutafuta, kuchakata habari, kuchapa magazeti na usambazaji – zilikuwa zinalipwa na serikali. Ni vyombo pekee vya habari ambavyo havikutegemea wasomaji ili kubaki sokoni.

Wakati serikali ikivinyima matangazo ya biashara vyombo vingi vinayosomeka au vinavyotazamwa na wananchi wengi, ilitenga fungu nono la matangazo ambayo yalipelekwa kwa vyombo hivi visivyo na watazamaji wengi – kwa sababu za kisiasa tu – jambo ambalo wachambuzi wanasema ni kielelezo cha ufisadi wa serikali ya awamu ya tano.

Taarifa zinaeleza kuwa ofisi za vyombo hivyo vya kimkakati, zilizo katika ghorofa ya 25 kwenye Jengo la LAPF, Kijitonyama – eneo la Makumbusho – zitahamia jengo jingine la serikali, katikati ya Jiji la Dar es Salaam ili kupunguza gharama za pango, ambazo pia zimekuwa zikilipwa na serikali badala ya “mmiliki wa vyombo.” Katika ofisi za sasa, vyombo hivyo vya habari vilikuwa na ulope (floor) mzima wa ghorofa ya 25.

Musiba alipoulizwa kuhusu suala hili, aling’aka: “Wewe umetumwa na mabeberu, na mtasubiri sana kuiangusha serikali ya Magufuli.” Akakata simu.

Vyombo hivyo vya kimkakati, licha ya serikali kuvipatia matangazo na vifaa vya kisasa, havina ushawishi mkubwa kwenye mitandao ya kijamii inayotembelewa zaidi na wasomi na watambuzi wa masuala ya kitaifa na kimataifa.

Kwa mfano, akaunti ya Twitter ya vyombo hivyo, vikitumia anwani ya @tanzanitenews, iliyoanzishwa Januari 6, 2019, inafuatiliwa na watu 144, huku akaunti Facebook, iliyoanzishwa siku hiyo hiyo inafuatiliwa na watu 2,462, hadi jana saa 5.43 usiku.

Vyombo hivyo vya kimkakati vilianzishwa kuwashambulia, kuwatukana na kuwadhalilisha wakosoaji wakubwa wa serikali na uendaji wa Rais Magufuli wakiwamo Maria Sarungi – mwanaharakati na mtetezi wa uhuru wa kujieleza, Benard Membe – waziri mstaafu aliyefukuzwa uanachama CCM baadaye akajiunga na ACT-Wazalendo na kugombea urais (2020) kupitia kupitia chama hicho, Ansbert Ngurumo – mwandishi wa habari mwenye safu ya Maswali Magumu iliyokosoa marais kwa miaka zaidi ya 15 mfululizo, ambaye alikimbilia uhamishoni kunusuru maisha yake, Freeman Mbowe – mwenyekiti wa Chadema, Zitto Kabwe – kiongozi wa ACT- Wazalendo, Tundu Lissu – mbunge mstaafu na mwanasheria mahiri na mgombea urais kupitia Chadema (2020), Godbless Lema – aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, John Heche aliyekuwa mbunge wa Tarime Vijijini, na wengine wengi wakiwamo waandishi wa habari za uchunguzi.

Like
8