Leo 14 Oktoba 2021, katika kuadhimisha Siku ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, serikali imeamua kuunganisha siku hiyo na tukio la kuzima Mwenge ambalo linafanyikia Chato, mkoani Geita.
Kwanza, sijui kwanini serikali yetu inapenda kuadhimisha kifo cha Baba wa Taifa kuliko siku yake ya kuzaliwa. Kwa mtu mwenye sifa ya “Baba wa Taifa,” na kwa mengi mema aliyolifanyia taifa, siku ya kuzaliwa kwake ndiyo ingepaswa ipewe kipaumbele.
Lakini wenzetu CCM waliona waweke umuhimu katika kifo chake kana kwamba wanafurahia kufa kwake. Labda!
Labda mtu angenihoji, “mbona Wakristo wanaadhimisha kifo cha Yesu? Walitamani afe?” Jibu ni fupi. Kimsingi, Wakristo huadhimisha ufufuko wa Yesu (si kifo chake) kwa sababu kadiri ya maandiko, ufufuko wake ndio msingi wa Ukristo wenyewe.
Sasa, kuhusu Mwalimu Nyerere na Tanzania, wapo wachambuzi wengi ambao kwa kutazama mwenendo wa utawala wa nchi wanasema “Nyerere alikufa na Tanzania yake.” Kuadhimisha kifo chake kunaweza kuwa furaha kwa watu wanaofurahia kifo kuliko uhai. Kukumbuka kifo cha Mwalimu Nyerere kwa mbwembwe ni sawa na kuthubutu kusahau maisha na tunu za Mwalimu Nyerere.
Na jitihada za “kumuua Nyerere” zimekuwa nyingi siku hizi hadi watu wanalazimisha kumfananisha na kumlinganisha na watu wasiostahili hata”kufungua gidamu za viatu vyake.”
Mmoja aliyelinganishwa naye ni Hayati John Pombe Magufuli (JPM) – huyu huyu ambaye “alizimika ghafla” mwaka huu, na leo hii (Siku ya Nyerere) wenzake “wanazimia Mwenge jirani na kaburi lake.” Huu uzimaji ni ishara ya jambo gani?
Sijawahi kukariri hoja za hao waliomlinganisha na Mwalimu Nyerere, lakini nafahamu kuwa zilichochewa na hulka binafsi ya Magufuli mwenyewe kupenda ubabe wa kufanya mawazo yake yakae juu ya mawazo ya wengine.
Kama wapo waliodiriki kumuita “mheshimiwa mungu,” ni dhahir hawa wanaomlinganisha na Mwalimu Nyerere wana nafuu, lakini hawapo sahihi.
Wapo waliosema kuwa hata utekelezaji wa miradi mikubwa kwa muda mfupi ni kigezo cha kumlinganisha JPM na Mwalimu Nyerere. Ila hawa wanasema hivyo bila kuchunguza kilichokuwa nyuma ya miradi hiyo na kiwango cha ubora wa miradi yenyewe.
Sasa, kwa kuwa leo imekutanisha adhimisho la kifo cha Mwalimu Nyerere na kuzimia Mwenge Chato, nimeona nitumie fursa hii kuonya wanaomlinganisha Mwalimu na Magufuli. Nitatumia hoja tatu kwa sasa. Zitusaidie kutafakari na iwe mwisho kwa mtu yeyote kumlinganisha Mwalimu Nyerere na kiongozi mwingine yeyote wa kizazi hiki.
Kwanza, Mwalimu Nyerere alijenga taifa na utaifa. Na aliona kuwa kujenga taifa ni muhimu kuliko kujenga madaraja, majumba, mabwawa, vyoo na kadhalika. Mradi wa kujenga taifa ni muhimu na wa kudumu.
Jitihada zake kufuta uchifu, ukabila, udini, ukanda, matabaka ya kiuchumi na umangimeza ni kielelezo cha ujenzi wa utaifa. Alitengeneza programu kama JKT, Vijiji vya Ujamaa, na shule za sekondari na vyuo kuchukua watu wote kutoka kila kona ya nchi, na kadhalika. Shabaha yake ilikuwa kuondoa tofauti ambazo zingeweza kubomoa utaifa.
Sasa tazama huyu ambaye analinganishwa naye. Ndani ya miaka mitano, ametengeneza ukanda, akapandisha hadhi baadhi ya makabila na kushusha mengine, akaonea makabila mengine wazi wazi, akaendekeza upendeleo wa itikadi za vyama, nk. Katika miaka mitano tu, Magufuli alibomoa misingi yote ya utengamano wa kitaifa, akachochea chuki ya matabaka ndani ya nchi.
Magufuli amemega taifa letu, akathubutu kulitenga kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla. Tanzania iliyokuwa kimbilio la wakimbizi ikaanza kufukuza wakimbizi na ikageuka mahali pasipo salama hata kwa raia wake.
Tanzania ya Mwalimu Nyerere iliyokuwa chini ya chama kimoja ilikuwa na rekodi ya utetezi wa haki za binadamu kuliko Tanzania ya Magufuli yenye vyama vingi iliyogeuka adui wa haki za binadamu. Ndiyo maana Jenereli Ulimwengu alisema tumerudi nyuma miaka 50.
Pili, Mwalimu Nyerere alikuwa mjenzi wa taasisi ya urais. Aliiasisi na kuiheshimu sana. Katika miaka ya mwisho ya utumishi wake, wake akiwa mstaafu, aliwahi kusema hadharani kuwa IKULU NI MAHALI PATAKATIFU. Alilenga kukemea aina yoyote ya ufisadi iliyokuwa imeanza kuhusishwa na Ikulu.
Tusisahau kuwa kauli hii ilitolewa na mtu aliyekaa Ikulu kwa miaka 24. Kibinadamu, kwa mtu mwenye madaraka makubwa namba hiyo, kuna uwezekano mkubwa wa kufanya mambo yanayoiondolea Ikulu utakatifu wake. Mwalimu Nyerere alikuwa na sababu za msingi sana kutamka na kuamini kuwa Ikulu ni MAHALI PATAKATIFU.
Lakini katika miaka mitano ya Magufuli, utakatifu wa Ikulu umetiwa doa lisilofutika. Wanaojua wanajua visa vya mateso na mauaji ya kikatili yaliyofanyika ndani ya Ikulu kwa mkono wa rais. Wanaojua wanajua jinsi baadhi ya vyumba vya Ikulu vilivyogeuzwa kambi ya kutesea watu kama ilivyokuwa Ikulu ya Idi Amin wa Uganda. Tumesikia taarifa za vikao vya mauaji ya wapinzani vikipangiwa Ikulu na kumhusisha rais mwenyewe moja kwa moja.
Yapo na masimulizi ya aibu ya vitendo vya ufuska vikifanyika kwenye sofa za Ikulu mchana kweupe. Tumesikia vipigo vikifanyika ndani ya familia iliyo Ikulu, wakati mwingine mbele ya watumishi wa Ikulu.
Kuna na aibu za waganga wa kienyeji kupewa ofisi na miundombinu, na kuwa sehemu ya Ikulu na misafara ya rais. Hizi ni baadhi ya aibu ambazo baadhi ya wasaidizi wa rais wamelazimika kuzivumilia kwa tabu kwa miaka mitano mfululizo, huku wakimsindikiza pia makanisani Jumapili.
Tumeshuhudia vikao vya chama vikifanyika ndani ya Ikulu chini ya Magufuli. Binafsi sina kumbukumbu za vikao vya aina hiyo hata wakati wa chama kimoja chini ya Mwalimu Nyerere. Haviruhusiwi; labda itokee tu viwe na agenda nyeti za kiusalama.
Chini ya Magufuli, urais kama taasisi ulitikiswa na ulidhalilishwa sana. Ni Magufuli huyu huyu aliyelazimisha idara ya usalama imwajiri binti yake aitwaye Jesca, na akapewa jukumu katika kitengo maalumu kurekodi simu za watu.
Simu za marais wastaafu na viongozi waandamizi zilirekodiwa, mazungumzo yao yakasambazwa mitandaoni. Huu ni uhuni usiopaswa kuhusishwa na taasisi ya urais. Huu ni udhalilishaji wa taasisi ya urais.
Taasisi ambayo Mwalimu Nyerere aliijenga na kuipa “utakatifu” ilichafuliwa ndani ya muda mfupi na mtu ambaye watu wasiojali misingi, waliojipendekeza kwake, walidiriki kumlinganisha na Baba wa Taifa.
Ni kweli kwamba Mwalimu Nyerere, kama binadamu wengine, alikuwa na makosa yake. Alitenda mengi tu, na baadaye aliyakiri kabla hajafa. Pamoja na hayo, dhamiri yake na utendaji wake si vitu vya kulinganisha na hiki tulichokiona kwa Magufuli katika miaka mitano tu. Kwa waliomjua Mwalimu Nyerere, ni sahihi kwako kusema kuwa hata Magufuli mwenyewe hakumjua Baba wa Taifa.
Tatu, Mwalimu Nyerere alichukia rushwa. Hakuwa na mzaha katika suala hili. Hakuna mtu leo anayeweza kujitokeza hadharani kudai kuwa aliwahi hata kufikiri kwamba Mwalimu Nyerere angeweza kupokea rushwa au kukutana na wakala anayempokelea rushwa.
Lakini katika miaka mitano ya Magufuli tumeshuhudia mawakala wa rushwa mchana kweupe, tena wengine wakipewa vyeo vikubwa bila kustahili kabisa ili wavitumie kwa kazi maalumu, wakawekewa hata ulinzi kutoka vikosi vya ulinzi wa rais.
Ni kwa vile alijenga mazingira ya vitisho na hofu kwa raia, mambo haya hayajaibuliwa, lakini kuna ushahidi mweupe hata wa rushwa zilizopokelewa siku chache kabla hajafa. Siku moja, mambo haya yatawekwa hadharani kwa faida na mafunzo kwa vizazi vijavyo.
Katika miaka mitano ya Magufuli, wapo watu waliojinadi kuchangisha fedha ili kumpelekea aweze kuwakubalia kuwapa kandarasi au biashara fulani. Kila mkoa alikuwa na kundi la wahandisi na makandarasi wake ambao walichanga hela kumpelekea ama moja kwa moja au kupitia kwa mawakala wake.
Zipo taarifa za uhakika kuwa baada ya kifo chake, baadhi ya akaunti zake na za mawakala wake akina Bashiru Ali, Dotto James na wengine kadhaa zilifungwa haraka haraka katika benki moja jijini Dar es Salaam.
Kama si busara za Rais Samia Suluhu na CAG Kichele, taifa lingeshuhudia aibu kubwa kuhusu rais na mawakala wake waliomzunguka na kuhusishwa na rushwa zake.
Hata tabia ya Magufuli kujaza maboksi yenye fedha taslimu na kutembea nayo kwenye msafara wake na kuzigawa alivyopenda ni ishara ya ufisadi ambao kwa namna yoyote unaonyesha kukosekana kwa utaratibu na umakini. Ni mtindo unaomfunua Magufuli kushikishwa hela chafu.
Tusisahau malalamiko ya CAG aliyeondolewa kinyume cha utaratibu Musa Assad kuhusu ununuzi wa ndege kwa fedha taslimu. Ni ushahidi wa kimazingira wa rais kuhusika katika rushwa na utakatishaji wa fedha.
Katika maeneo mengi ya Kanda ya Ziwa hasa Chato, Geita na Kagera, kuna miradi binafsi ya Magufuli iliyokuwa inasimamiwa na mawakala wa rushwa.
Kama kuna kitu Rais Samia anaweza kulifanyia taifa hili ni kujitenga na ufisadi wa Magufuli kwa uwazi. Mambo haya yaachwe yasemwe, yawekwe hadharani ili huko tuendako taifa lisije kupata rais mwingine anayefanana na Magufuli.
Bado natafakari sababu za serikali kuadhimisha kifo cha Mwalimu Nyerere badala ya kuenzi kuzaliwa kwake na maisha yake; na kwanini mwaka huu wameamua kuzima Mwenge huko alikolazwa Magufuli.
Kuna jambo wanajaribu kulizima kabisa? Kwa hili, walau nina uhakika – si Mwalimu Nyerere. Hazimiki. Kwa watu waadilifu, Mwalimu Nyerere bado yu hai.
Nasisitiza tena kuwa kwa vyovyote vile, ni makosa ya kimantiki na kimaadili kumfananisha Mwalimu Nyerere na viongozi hawa wa kizazi hiki.