Sabaya ahukumiwa miaka 30 jela kwa ujambazi

LENGAI Ole Sabaya, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, ametiwa hatiani kwa unyang’anyi wa kutumia silaha na amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.

Katika hukumu hiyo iliyotolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Odira Amworo, kwenye mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, waliokutwa hatia ni Sabaya na wenzake wawili – Sylvester Nyegu, Daniel Bura – ambao pia watatumikia kifungo cha miaka 30 jela.

Hukumu hiyo ilitolewa Ijumaa Oktoba 15, 2021 saa 11:47 jioni kwa hukumu iliyosomwa tangu saa 5:56 asubuhi.

Hakimu alisema kuwa kwa vile Sabaya alikuwa mkuu wa wilaya (ambaye huteuliwa na rais) kitendo alichofanya kinadhalilisha taasisi ya urais.

“Kwa mujibu wa sheria, hakuna ubishi kwamba mikono yangu imefungwa, naweza kuwafunga miaka 100, lakini siruhusiwi kuwafunga chini ya miaka 30… Mbali ya kwamba wakili wa serikali ameomba wachapwe viboko, na walistahili wachapwe, maanake nao walikuwa wanawatoa wenzao wenge…,” alisema hakimu.

Mashitaka dhidi ya Sabaya na wenzake yalitokana na tukio la ujambazi ambalo SAUTI KUBWA ililiripoti tarehe 23 Februari 2021.

Mara baada ya hukumu, mawakili wa Sabaya na wenzake walisema wanatarajia kukata rufaa kwa kuwa hawajaridhishwa na hukumu.

Iwapo hukumu hiyo itatekelezwa ilivyo bila kuathiriwa na uamuzi mwingine wowote wa kisheria, kama rufaa ya wafungwa wenyewe au msamaha wa rais, Sabaya na wenzake watakaa jela hadi mwaka 2041, maana kwa mujibu wa ukokotoaji wa idadi ya miaka, wafungwa watatumikia theluthi mbili ya kifungo chao, yaani miaka 20.

Like