MCHEZO mchafu wa kuikosesha mapato Serikali ya Tanzania umeibuka katika mnada wa bidhaa unaondeshwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa njia ya mtandao (online auction).
Mbali na kukosa mapato, serikali pia hulazimika kuingia hasara kubwa kwa kuteketeza bidhaa ambazo zinaisha muda wake kwa “michezo hiyo michafu” katika mnada huo kwa njia ya mtandao.
Uchunguzi uliofanywa na SAUTI KUBWA umebaini kwamba baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakitumia vibaya utaratibu huo wa kuuza bidhaa, hivyo kuikosesha mapato serikali na wakati huohuo, wakikwamisha wanunuzi makini kununua.
Kwamba endapo kuna bidhaa inakadiriwa kuwa na bei ya Sh. 3,000,000 na akatokea mnunuzi wa juu kwa kiasi cha Sh. 7,000,000, kundi moja ndani ya mnada huo, huamua kuweka fedha zaidi, hadi Sh. 32,000,000 kwa bidhaa hiyo, lakini hushidwa kulipa na “kupotea.”
Kushidwa kulipa baada ya nyundo ‘kugogwa,’ hulazimisha TRA kurudia mnada kwa gharama zingine; muda, rasilimali watu na hata fedha za kukamilisha mnada mwingine.
Kinachofanyika ni kuwepo kwa udukuzi wa kuingilia mfumo wa mnada wa TRA na kupata siri ya bei elekezi ya serikali kwa wafanyabiashara hao na wao huamua kuvuruga mnada kwa kuweka kadirio la juu ambalo hawawezi kulipa, ili kuharibu mnada.
“Hawa wafanyabiashara wahuni wanaoikosesha serikali mapato na kuzuia wenzao kununua bidhaa ni wahuni tu, huenda wanadukua au kutumia njia zingine kupata taarifa za mfumo, ni wahujumu uchumi hawa,” alig’haka mnunuzi mmoja Issa Yahya aliyeulizwa na kuthibitisha kuwepo kwa mchezo huo mchafu.
Uchunguzi zaidi umebaini kwamba wengi wanaoweka kiwango cha juu hawana uwezo wa kununua, isipokuwa kuvuruga, kwa sababu wanzojua wao. Hawa huweka kiwango cha fedha kikubwa na mara nyingi hubeba tarakimu zinazofanana; 999,999; 444,444; 111,111 na nyingine.
Imebainika kwamba hasara ya Sh. 97,043,999.58 (milioni 97) ambazo zingelipwa kodi serikalini zilikosekana kwa siku tatu tu baada ya kukwama kuuzwa kwa bidhaa mbalimbali kutokana na mnada huo wa mtandaoni.
Hasara hiyo ya siku tatu tu ilionekana katika mnada wa Agosti 5, 16 na 30 ikiwa imetokana na wafanyabiashara waaminifu kuweka fedha kiasi cha Sh. 539,133,331 ili kupata bidhaa mnadani, lakini wenzao baada ya kuona wanaweza kufanikiwa, waliweka kiwango cha juu zaidi cha Sh. 702,133,330 ambapo kama wangenunua, wangelipa kodi ya Sh. 126,383,999.40 (milioni 126). Hata hivyo hawakulipa. Kodi ya serikai ni asilimia 18.
Uchunguzi zaidi umebainika kuwa Agosti 2, 2021 katika mnada namba TZDL-2021-150-0004 mnunuzi wa juu aliweka Sh. 18,000,000 kununua katoni 219 za paneli za umeme wa jua (solar panel) zilizokuwa ndani ya kontena namba MRSU0090037, lakini kabla ya nyundo kugongwa, akajitokeza mfanyabiashara mwingine aliyeweka Sh. 78,000,000,000, ambaye hata hivyo “aliingia mitini” bila kulipa kiasi alichoiaminisha TRA kwamba angenunua mzigo huo.
Baada ya siku mbili kupita, bidhaa hiyohiyo, ilirudisha kwenye mnada namba TZL-2021-154-0116, mnunuzi wa juu aliweka Sh. 8,788,889 kununua katoni hizo 219 za paneli za umeme wa jua zilizokuwa ndani ya kontena lilelile (namba MRSU0090037), lakini kabla ya nyundo kugongwa, akajitokeza mnunuzi mwingine aliweka Sh. 51,299,999, ili kununua, lakini ‘alitokomea.’
Agosti 16, 2021 katika mnada namba TZDL-2021-156-0005 kuliuzwa seti moja ya genereta ya kuzalisha umeme yenye uwezo wa KV 65, mnunuzi makini alifika kulipa Sh. 10,000,008, lakini kabla ya nyundo kugogwa, alitokeza mnunuzi mwingine na kuweka Sh. 37,999,999, lakini hakuweza kulipa.
Kutokana na kushindwa kulipwa, ilibidi kufanyika mnada mwingine namba TZDL-159-0014 kwa bidhaa hiyohiyo baada ya siku 12 ambapo mnunuzi makini aliweka Sh. 4,620,000 lakini kabla ya nyundo kugongwa, alijitokeza mnunuzi mwingine ambaye aliweka Sh. 21,121,111, ambaye hata hivyo, hakujitokeza kulipa.
Imegundulika kuwa wafanyabiashara hawa wanaovuruga taratibu za mfumo wa mnada huo, wanaweza kufahamika kirahisi, ingawa wamekuwa wakiendelea na mchezo huo bila kuchukuliwa hatua kali.
Endapo TRA itambaini mfanyabiashara huyo na kuchukua hatua za kisheria, adhabu anayoweza kupewa ni kufungia namba ya utambulisho ya mfanyabiashara (TIN) kwa mfanyabiashara husika- kwa muda wa miezi sita.
Utaratibu uliopo kwa wafanyabiashara wanaojiunga na mchakato wa mnada huo wa mtandao, ni kujisajili kwa kutumia namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN) na majina ya mhusika.
Mmoja wa wakurugenzi wa TRA, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kueleza kwamba mamlaka imekuwa ikishughulikia na kuchukua hatua dhidi ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu.
“Michezo ya kuhujumu mnada wa mtandaoni na kuikosesha mapato serikali, tumekuwa tukiibaini na kuchukua hatua ikiwamo kuwafungia wahusika, lakini tunachukua hatua kali zaidi kwa kuwapeleka mahakamani,” amesema, huku akikataa kuandikwa jina gazetini.
Uchunguzi zaidi umebaini kwamba wafanyabiashara wanaohujumu serikali wamekuwa wakitumia TIN za watu wengine, hasa wamiliki wa pikipiki, maarufu bodaboda kwa kuwapa kiasi cha fedha na kuweka namba na utambulisho wa majini ilikuvuruga mnada.
Inapotokea kwamba TIN imefungiwa, wafanyabashara hao wasiokuwa waaminifu wamekuwa wakiwarubuni wafanyabiashara wengine wadogo na kununua TIN zao.
TIN hizo hununuliwa kwa wenye bodaboda au wafanyabiashara wengine wadogo kwa Sh.50,000 na ikitokea kwamba utambulisho huo wa mlipakodi umefungiwa, huenda kuomba upya TRA. Hivi sasa TRA imeboresha huduma zake kiasi kwamba TIN hutolewa bure na kwa muda mfupi kwa wenye uhitaji – tena kwa njia ya mtandao.
“Mimi TIN hainisaidii sana, anapokuja mtu wa mnada anaihitaji namna na ananipa changu nasepa, akiipoteza, ananilipa tena naenda kuomba nyingine, kwanini nife njaa bhana? Anahoji Ngule Sanga, dereva wa bodaboda, anayeendesha shughuli zake jirani na kituo cha daladala cha Stesheni.
Mbali na hasara hiyo kwa serikali kukosa mapato na wafanyabiashara, TRA pia huingia hasara kubwa kwa kuteketeza bidhaa ambazo zimeisha muda wake. Imebainika kuwa mamlaka hiyo ya mapato imekuwa ikitoa kandarasi ya kuchoma bidhaa zilizoisha muda wake, na kwamba gharama ya kuchoma tani moja hufikia hadi Sh.1,500,000.
Serikali kupitia TRA mwaka jana- 2020 ilisitisha kufanyika kwa minada ya hadhara kwa ajili ya kuuza bidhaa mbalimbali kwa kutumia madalali. Bidhaa zinazouzwa ni zile zilizoshindwa kuchukuliwa na waagizaji baada ya kukwama kulipa kodi au changamoto zingine.
Utaratibu huo mpya wa minada hiyo hufanyika kwa kutumia njia ya mtandao wa kielektroniki kwa kupitia tovuti ya TRA ambayo ni www.tra.go.tz ambapo huendeshwa kwa muda maalumu na kuonekana kwenye mfumo wa taarifa na baadaye mshindi kutangazwa baada ya nyundo ‘kugongwa.’
Awali minada kwa njia za madalali ilikuwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanyika mara moja kwa wiki, hivyo kwa kiasi kikubwa bidhaa kushindwa kuuzika kwa wakati na kusababisha serikali kutopata kodi kwa wakati, ingawa wafanyabashara “wahuni” wanaojitokeza kwenye mtandao, hawakuwepo.