Mwakinyo atamani kuwa namba wani

BAADA ya sifa ya Tanzania katika michuano ya kimataifa katika riadha kufifia, kupoteza mvuto kwenye mpira wa miguu, sasa nchi hiyo ya Afrika Mashariki inasomeka vyema katika medani za masumbwi.

Anayepaisha jina la Tanzania katika masumbwi (mchezo wa ngumi) ni Hassan Mwakinyo, kijana kutoka Jiji la Tanga ambaye sasa anatamani kuzichapa na bingwa namba tano duniani – kwa uzito wa juu mwepesi (super welter), Erickson Lubin kutoka Marekani.

Mwakinyo anashikilia rekodi ya kuwa bondia namba 11 duniani, huku akiongoza Afrika, baada ya kupanda ngazi haraka alipomchakaza mwanamasumbwi kutoka Namibia, Julius Indingo mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar e Salaam. Bondia huyo wa Tanzania alishindwa kwa TKO katika raundi ya nne.

Kabla ya ambano lake na Indigo, Mwakinyo alikuwa bondia namba 16 kwa ubora duniani.

Akizungumza na SAUTI KUBWA jana, Mwankinyo amesema anatamani sasa kupigana na bondia kutoka Marekani, ambaye atahakikisha anamchakaza ili kufikia namba mbili kwa ubora duniani ili apate nafasi ya kupigana na bondia anayeshikilia namba moja duniani – kwa uzito wake, Jermell Charlo.

Mwakinyo amesema anatamani kuwa bondia namba moja duniani baada ya miaka miwili au zaidi kidogo ili kudhihirisha dunia kuwa Tanzania na Afrika kuna vipaji na watu wenye uwezo katika michezo na maeneo mengine.

“Akili yangu sasa ni safari kwenda kupigana Marekani, au mahali pengine ambako kuna mabondia wanaoweza kukabiliana nami, naamini nitafika mbali kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu,” amesema Mwakinyo.

Mwakinyo alishangaza dunia miaka mitatu iliyopita -2018 baada ya kumchapa katika raundi ya pili – kwa TKO, bingwa wa Uingereza na bondia aliyekuwa akishikilia namba moja kwa uzito mwepesi wa kati (light middle) Ulaya, Sam Eggington, huko Marekani.

Baada ya ushindi huo, Mwakinyo alipanda hadi nafasi ya 16 duniani akitoka nafasi ya 158. Katika pambano lake na Sam, hakupewa nafasi ya kushinda na wengi walimdharau. Vituo vikubwa vya televisheni duniani, ikiwamo Sky, BBC, CNN vilimtaja kuwa “bondia wa ajabu” kutoka Tanzania.

Mchambuzi mahiri wa masumbwi nchini, John Kayenza amesema Mwakinyo anaweza kuwa miongoni mwa mabondia wazuri walowahi kutokea Tanzania katika miaka ya hivi karibuni.

Tanzania iliwahi kuwa na rekodi nzuri ya masumbwi kupitia kwa ukoo wa Matumla, hasa Rashid ‘Snake Boy’ ambaye aliweza kuwakilisha vyema nchi katika michuano ya Jumuia ya Madola ya 1994 na 1998. Hata hivyo, Rashid aliamua kupumzika na kubaki kuwa mwalimu wa ndondi.

Like
1