Tanzania yaporomoka hatua 10 uhuru wa vyombo vya habari

RIPOTI ya mwaka 2018 inayotolewa na taasisi ya Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka (RSF), kuhusu uhuru wa vyombo vya habari katika mwaka uliopita, inaonyesha kwamba ndani ya mwaka mmoja Tanzania imeporomoka  kwa hatua 10 kutoka ilipokuwa mwaka jana.

Katika ripoti ya 2017 Tanzania ilishika nafasi ya 83 kati ya nchi 180 zilizofanyiwa utafiti. Mwaka huu imeshika nafasi ya 93.

Miongoni mwa sababu zilizoshusha nchi hiyo katika katika mwaka 2017, kwa mujibu wa utafiti huo wa RSF, ni vitisho vya serikali dhidi ya vyombo vya habari kufungia magazeti, kufungua mashitaka dhidi ya waandishi, wahariri na wamiliki wa vyombo vya habari,  kutisha na kuteka waandishi wa habari.

Baadhi ya matukio yaliyoshusha heshima ya Tanzania ni pamoja na Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kuvamia kituo cha Clouds FM, serikali kushitaki Maxence Mello, mmiliki wa mtando wa Jamii Forums, na “watu wasiojulikana” kuteka na kupoteza Azory Gwanda, mwandishi wa gazeti la Mwananchi.

Miongoni mwa sheria mbaya ambazo zimekuwa zinatumiwa na serikali kuminya uhuru wa habari ni pamoja na Sheria ya Takwimu, Sheria ya Mitandao, na Sheria ya Huduma za Habari, ambazo serikali ya awamu ya tano imezitumia kuzuia vyombo vya habari kuandika habari zinazoibua kashfa za serikali, na kutisha au kushitaki waandishi wa habari au kufungia vyombo vya habari.

Taarifa zaidi kuhusu ripoti hiyo unapatikana katika tovuti ya RSF, yenye makao makuu nchini Ufaransa – https://rsf.org/en/tanzania

Like
2

Leave a Comment

Your email address will not be published.