Maswali matano ya Dk. Mahanga: Kwanini Serikali ya Magufuli inahujumu utalii?

SEKTA ya utalii ndiyo ya pili inayoingizia Tanzania fedha nyingi za kigeni baada ya sekta ya madini. Kwa sasa sekta hii inaingizia nchi zaidi ya dola za kimarekani bilioni 2 sawa na Shs. trilioni 4.5 kwa mwaka.

Na kwa mujibu wa Benki ya Dunia kama Tanzania ingewekeza vizuri zaidi kwenye sekta hii, kufikia mwaka 2025 sekta hii itakuwa inaingizia Tanzania dola za kimarekani bilioni 16 sawa na zaidi ya shilingi trilioni 35 kwa mwaka.

Na katika Sera ya kuendeleza sekta ya Utalii, Serikali ilitunga Kanuni ya Mfuko wa Maendeleo ya Utalii (Tourism Development Levy Regulations) za mwaka 2013. Mfuko huu unatakiwa utumike kwa shughuli na mipango mbalimbali ya kukuza utalii nchini ili hatimaye sekta hii ikue zaidi kama Benki ya Dunia na wataalam wengine wanavyobashiri.  Na kwa mujibu wa Kanuni Na. 9(1) ya Mfuko huo, TRA wanatakiwa kuhamisha fedha zote zinazopokelewa kama tozo ya Utalii kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Utalii.

Hata hivyo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa miaka miwili ya 2015/16 na 2016/17 anasema katika taarifa zake za Ukaguzi kwamba TRA haikupeleka tozo yoyote kwenye mfuko huo ingawa ilikusanya jumla ya shs. 14,605,613,432 kwa miaka hiyo miwili.

Katika ukaguzi wa hesabu za mwaka 2015/16 CAG alionyesha kwamba TRA ilikusanya shs 6,357,529,854 kutokana na tozo la utalii lakini fedha yote hiyo haikupelekwa kwenye mfuko wa utalii ili zifanye kazi za kukuza utalii nchini kama zilivyoainishwa kwenye Kanuni za kukuza utalii. CAG akaitaka TRA kuhamisha fedha hizo kwenda kwenye mfuko huo. Hata hivyo TRA haikufanya hivyo, na badala yake mwaka uliofuata wa 2016/17 TRA tena ilishindwa kupeleka hela yoyote kwenye mfuko huo ingawa ilikusanya Shs. 8,248,083,588 kama tozo ya utalii. CAG anasema _”kushindwa kupeleka makusanyo ya tozo ya utalii kwa mujibu wa Kanuni ni kuzuia_ *(kuhujumu)* _mipango na shughuli za maendeleo ya utalii nchini..)_

Maswali matano ya kuuliza:

  • Fedha hizi bilioni 14.6 kwa miaka miwili zilizokusanywa na TRA lakini hazikupelekwa kwenye mfuko wa utalii zimetumikaje na Serikali?
  • Kwa kushindwa kupeleka fedha hizo kwenye mfuko wa utalii ili zitumike kukuza utalii, TRA na Hazina hawaoni kwamba wanahujumu sekta muhimu ya utalii ili isifikie lengo la kuleta shs. trilioni 35 kila mwaka kama fedha za kigeni kufikia mwaka 2025 na kupaisha uchumi wa Tanzania?
  • Kwanini TRA na Hazina wanakaidi ushauri na maelekezo ya CAG kila mwaka ya kupeleka tozo hii kwenye mfuko wa utalii?
  • Serikali haioni kwamba inavunja sheria kupitia Kanuni Na. 10 (a-e) ya Mfuko wa Maendeleo ya Utalii ya mwaka 2013?
  • Hivi wananchi tukisema kwamba fedha hizo bilioni 14.6 kwa miaka miwili zimetumika kwenye mambo yasiyokuwa kwenye Bajeti au zimefisadiwa tutakuwa tumekosea? 

Dk. Milton Mahanga, mtaalamu kwenye masuala ya fedha, ununuzi na uendeshaji wa nyumba mijini. Amekuwa mhadhiri kwenye fani za uhasibu, ununuzi na ugavi, mbunge kwa miaka 15, na naibu waziri kwa miaka 10 katika wizara kadhaa za Tanzania. Ni mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Ilala, na  mjumbe wa Baraza Kuu la Chadema.

Like
2

Leave a Comment

Your email address will not be published.