TANZANIA INAKABILIWA NA MFUMUKO WA BEI: TUJADILI TAFSIRI HAFIFU NA ATHARI ZAKE

MAPEMA wiki hii, Benki ya Dunia imetoa matarajio yake ya hali ya uchumi wa dunia mwaka 2022. Taarifa yake inaonesha kuwa, Kasi ya ukuaji uchumi wa dunia itapungua hadi 4.1% mwaka 2022 ukilinganisha na 5.5% mwaka 2021. Matarajio baada ya mwaka huu ni kuwa ukuaji huo utashuka zaidi hadi kufikia 3.2% mwaka 2023, japo uwezekano wa mabadiliko pia ni mkubwa, kwani uchumi wa dunia umeanza kuimarika dhidi ya athari za Uviko 19.

Kwa upande mwingine, taarifa ya Shirika la Fedha Duniani(IMF) inaonesha kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi Kusini mwa Jangwa la Sahara itafikia 3.8% mwaka 2022.

Hata hivyo, Benki ya Dunia inasisitiza kuwa kuongezeka kwa tofauti kubwa ya vipato duniani ni jambo hatari kiuchumi. Taarifa yake inataja kuwa; tofauti kubwa ya vipato imejizingira kwenye mifumo ya uchumi na kuongeza kuwa nchi maskini ziko kwenye hatari zaidi kwenye hali hii hasa zinapojaribu kudhibiti mfumuko wa bei.

Rais wa Benki ya Dunia, David Malpas anazilaumu nchi zilizoendelea katika kuchagiza tofauti ya vipato katika kipindi hiki zinapokabiliana na ongezeko la mfumuko wa bei. Wakati nchi nyingi zilizoendelea kama Marekani zikitarajia ongezeko la viwango vya riba kudhibiti kuongezeka kwa gharama za bidhaa, David Malpas anatahadharisha kuwa; gharama kubwa za mikopo zinaweza kuathiri chumi dhaifu. Tatizo kubwa la kuongeza viwango vya riba ni kuwa; watu wanaohitaji pesa kwa ajili ya shughuli za haraka za kuanzisha biashara mpya, biashara za akina mama watazipata kwa gharama kubwa ama wengine wakakosa kabisa kutokana na masharti ya ukopaji.

Lakini lililo wazi ni kuwa; tatizo la mfumuko wa bei liko Rio de Jeneiro mpaka Dodoma, Beijing, Washington na London. Katikati ya mtanziko huu kila taifa lina mbinu za uchumi kulinda, raia wake dhidi ya bei ya huduma na bidhaa. Kwenye kitovu cha haya, ni raia wanaostawi kwa kutumia njia za kiuchumi zinazofanya kazi kwa ajili ya wengi. Na hapa ndipo penye utofauti.

Hapa nchini, gharama za bidhaa zinaongezeka, mitaani. Mwanafunzi wangu mmoja aliniuliza; Kwa nini mamlaka zinajizatiti sana kudhibiti mfumuko wa bei kwenye takwimu wakati kuna ongezeko kubwa la gharama za bidhaa na huduma kila kukicha? Mwanafunzi huyu alikuwa ameona taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) mapema wiki hii ikionesha kuwa kiwango cha mfumuko wa bei ulikuwa 4.2% mwezi Desemba, 2021 ukilinganishwa na 4.1% mwezi Novemba. Hiki kikiwa kiwango cha juu kabisa kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita. Aidha, taarifa hiyo ikionesha kuwa bado kiwango hicho kiko ndani ya mpango kati wa serikali wa chini ya 5% na malengo ya sera ya fedha (monetary policy).

Walaji hupata wanachostahili?

Hapa kuna jambo la kufikirisha. Taasisi kama IMF(Shirika la Fedha Duniani), Benki Kuu ya Tanzania, Wizara ya Fedha na NBS wanasema kuwa mfumuko wa bei umedhibitiwa chini ya 5%. Kiwango cha wastani kinachopigiwa chapuo ni kile cha mwaka 2018 cha 3.4%. Ukilinganisha na nchi ilipokuwa mwanzoni mwa miaka ya tisini(1990’s) wakati mfumuko wa bei rasmi ukiwa kwenye tarakimu mbili, na hivi karibuni kati ya mwaka 2006 na mwaka 2013, kiwango cha sasa kinaonekana angalau kuridhisha.

Hata hivyo, ukiweka kiwango hiki cha mkakati wa muda mfupi cha serikali kwa muda mrefu- kila kitu kinabadilika. Ukweli ni kuwa, kimya kimya tunaweza kuamini mfumuko wa bei ni himilivu na tunapata thamani halisi ya pesa yetu. Nafikiri hata wajuzi wetu wengi ndani ya IMF, BOT, NBS au Wizara ya Fedha nao wanaingizwa kwenye boksi hili.

Tunatakiwa kuanza kutazama suala la mfumuko wa bei kwa njia hii; Kiwango cha mfumuko wa bei cha 3.4% sio tu ni kidogo, kinawaumiza walaji chini kwa chini bila wao kutambua.

Kuanzia mwaka 2011 hadi leo, wastani wa mfuko wa bei ni 7.6% hii maana yake ni ongezeko la bei za bidhaa na huduma kwa 76% kwa muongo mmoja uliopita. Hii ni sababu ya kwa nini Watanzania wanahisi kuwa gharama zao za maisha zimeongezeka.

Aidha, sababu nyingine inafikirisha zaidi. Badala ya makampuni kuongeza bei za bidhaa kwa ajili ya kihimili ongezeko la mfumuko wa bei kwa muda mrefu; kampuni hizi zimebuni mbinu ya kuwapa wateja wake kiwango kidogo cha bidhaa kwa bei ile ile au kubwa zaidi. Mfano hai ni ule wa vinywaji baridi.

Wewe unakunywa soda?

Ujazo wa soda ambao umepunguzwa kutoka chupa ya mililita 500 mpaka mililita 350 ili kucheza na saikolojia ya wanywaji.

Mfumuko wa bei wa kimya kimya

Wiki iliyopita, nikiwa kwenye mjadala wa WANAZUONI kwenye Club House ambao ulikuwa unahusu deni la taifa; niligusia kidogo hii silent inflation. Rafiki yangu mmoja mchumi alionesha kushangaa lakini walau akakiri kuwa hafahamu kitu kama hicho. Nikiwa kwenye mjadala mwingine, mtu mwingine aliyejiita mchumi akanishambulia kuwa nilisema “silent inflation” na kuwa sifahamu ninachosema. Safari hii, tofauti na rafiki yangu aliyekiri kutokufahamu huyu alijivisha ujinga kuwa hakipo. Wachumi wetu; “silent inflation” ipo na hii ni maana yake.

Hii “silent inflation” mantiki yake ni kuwahadaa wanywaji wa soda kuwa bei haijabadilika sana. Kwa mfano, pesa ambayo inanunua soda ya mililita 350 leo, ingweza kununua nusu lita( mililta 500) miaka kumi iliyopita. Hata kwenye vifurushi vya Simu za mkononi, nako Kuna silent inflation ambako kiwango cha dakika na data zinapungua wakati bei inabaki palepale.

Unapojumuisha hatua za kupunguza gharama, utagundua kuwa, kiuhalisia, kiwango cha mfumuko wa bei ni kikubwa kuliko wanachosema NBS. Hiki ndicho wachumi hukiita silent inflation. Huwa kitu hiki kinasababisha watu kuitazama hali ya wakati uliopo na kusahau athari za muda mrefu. Kwa kutumia mfumuko huu wa kimya kimya ni rahisi kuficha ukweli.

Muhimu kufahamu ni kuwa, hii “silent inflation” haiko tu kwenye nchi maskini kama Tanzania. Profesa wa Uchumi wa Mienendo ya Binadamu(Bahavioral Economics) na mshindi wa tuzo ya Nobel ya Uchumi mwaka 2013 kutoka chuo kikuu cha Yale(Marekani), Robert Shiller aliandika makala mwaka 2018 iliyoifungua dunia.

Kabla ya makala yake, wengi waliishi kufikiri kuwa mfumuko wa bei kwenye nchi zilizoendelea kama Marekani, Sweden, Korea Kusini au Japan siyo kitu cha maana kwenye uchumi mpana. Hivi sasa , kwenye nchi hizi malengo ya mfumuko wa bei kwa serikali ni 2%

Hapa Tanzani, malengo ya Benki Kuu ni 5% kwa muda wa kati. Lakini hii hali ni ya hatari kwa uchumi wa watu na kwa kweli mara kadhaa nimeandika kuwa Benki Kuu inahitaji kubadili majukumu yake au muelekeo wa sera ya fedha, hasa mfumuko wa bei.

Majukumu ya Benki Kuu

Kwa muda sasa, magavana wa BOT wameifanya benki hii kuwa mdhibiti wa mfumuko wa bei( inflation controller), kwa kutumia sera ya fedha na bajeti. Maana kila wakija kwenye umma wa Watanzania wanasema kuwa kuwa mfumuko wa bei chini ya malengo ya 5% huleta matokeo mengine bora ya kiuchumi. Lakini hoja hii inakinzana na ukweli wa kitafiti na hasa juu ya hali ya mambo hapa Tanzani. Hali ya sasa inathibitisha haya.

Jumatatu ya wiki hii, nilihudhuria mjadala kazini kwangu kuhusu sera hitajika ili kukuza uchumi unaozalisha ajira. Huwa naongea sana kwenye mijadala lakini siku hiyo nilijaribu kukaa kimya ili kujifunza zaidi.

Maoni mengi yalikuwa juu ya kurejesha ukuaji wa uchumi. Maoni hayo, sio kuwa hayakuwa sahihi lakini hayaakisi ukweli wa mambo hapa nchini. Kwa kawaida, ukuaji wa uchumi huaminika kuwa unatengeneza ajira na kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira, lakini kwa mtazamo wangu, hapa nchini mambo ni tofauti.

Tafiti zinaonesha kuwa ukuaji wa uchumi hapa Tanzania umeshindwa kutengeneza ajira. Kilichonishangaza kwenye ule mjadala ni wakubwa zangu kitaaluma kupendekeza mambo yaleyale ambayo tumefanya nyakati zote. Lakini sikugutuka kwani ndicho serikali inachokisema. Kwa hiyo sisi wengine tunasema! Khaa!

Vichocheo na vizingiti vya ukuaji uchumi

Ushahidi wa kitafiti unaonesha kuwa nchi zilitengeneza uchumi unaozalisha ajira kuanzia Marekani mpaka Ujerumani, Japan, Italy, Korea Kusini mpaka Sweden; benki kuu zao zilielekeza mikopo kwenye kuendeleza viwanda na wafanyabiashara wadogo hasa kipindi kile cha ukuaji wa viwanda.

Kama nilivyowahi kuandika, benki kuu ipeleke au ishawishi mikopo kuelekea kwenye sekta ya viwanda na hasa kwenye kuchochea tija kwenye kilimo kwa kutoa ruzuku kwenye teknolojia mpya, kuzuia upotevu wa mazao baada ya mavuno, umwagiliaji, kuongeza thamani badala ya haya madirisha ya kilimo kwenye benki zetu ambayo hayawezi kufanya zaidi ya hapo kutokana na ufinyu wa fedha.

Muelekeo wetu wa kiuchumi uwe wa kuwekeza kwenye rasilimali watu( elimu na ujuzi), kurekebisha sera yetu ya mkakati wa viwanda, kuratibu uchumi na kushughulika na nidhamu kwenye matumizi ya umma.

Nafahamu kuwa kuna mikakati “kufungua uchumi” kuanzia kwenye kuongeza thamani kwenye kilimo, utalii na kwenye sekta ya ngozi. Maswali yangu ni haya;

Vigezo vipi vimetumika kwenye uchaguzi wa vipaumbele vyetu?

Vigezo hivi vina ushahidi kiasi gani wa kitafiti?

Kama ushahidi upo, ni kwa jinsi gani sekta hizi zitafunguka na kuendelezwa zikiwa zinaongeza uzalishaji na ajira?

Nani anafanya nini serkalini, kwenye sekta binasfi, taasisi za kiraia, wananchi na “wabia wa maendeleo”?

Haya ni masuala mijadala yetu ya kiuchumi ndani na nje ya serikali inabidi kuyajibu. Siyo kuyajibu kwa kuwa huwa tunayajibu, tutajibu kwa kuyajibu kweli.

Lakini kwanza hatua za dharura zinatakiwa kilinda wananchi dhidi ya huu mfumuko wa bei wa kimya kimya.

Like
3