TANAPA YAJIPANGA KIMKAKATI

KAMPUNI ya Uwekezaji iliyo chini ya Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa (TANAPA) ijulikanayo kama Tanapa Investment Ltd imejipanga kutoa ushindani na kampuni za nje kuwania tenda mbalimbali za ujenzi serikalini na hata nje ya nchi.

Kampuni hiyo kwa sasa inaimarisha uwezo wake wa ndani kwa kununua mitambo mbalimbali yenye hadhi ya Kandarasi Daraja la kwanza (Class One) yenye sifa ya kupata tenda za hadhi ya juu kama kampuni nyingine kubwa za nje.

Akizungumza na SK Media jana, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Mhandisi Mshauri, na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo, Dkt Richard John Matolo alisema kipaumbele chao kwa sasa ni kuhakikisha wananunua vifaa vyenye uwezo mkubwa wa kufanyakazi zote kubwa za ujenzi wa aina mbalimbali.

Alisema ingawa Tanapa Investment Ltd ilianzishwa kwa lengo la kushughulikia kandarasi za ndani ya Tanapa na taasisi nyingine za serikali kwenye uhifadhi, lakini hawana budi kwenda nje ya hapo kwakuwa uwezo walio nao pamoja na leseni yao vinawaruhusu kufanya hivyo.

“Kampuni yetu ina hadhi ya Kandarasi Daraja la kwanza, wataalam wenye viwango vya juu katika masuala ya ujenzi, ushauri wa kitaalam tunao, tunachotilia mkazo kwa sasa ni kununua vitendea kazi, tunahitaji mitambo mikubwa ya kutosha ili tuweze kushindana na makandarasi wakubwa kutoka nje kwenye tenda mbalimbali za serikali.

“Kwa kutumia kampuni yetu ya ndani, tunao uhakika wa kufanya na kukamilisha miradi kwa wakati, na faida kubwa ambazo zilikuwa zinakwenda kwa kandarasi wa nje, sasa zitabaki ndani na hilo ndilo lengo la serikali.”alisema Dkt Matolo na kuongeza kuwa

“Kimsingi bado hatujapata mtaji stahiki, tukiondoa fedha za uendeshaji, kulipa kodi, leseni na kadhalika, fedha nyingine za kampuni zinatoka kwenye kazi mbalimbali za mashirika mengine ya uhifadhi lakini tunataka twende mbali zaidi.”alisisitiza.

Aidha akijibu swali kuhusu kiasi cha fedha Shilingi bilioni 26 walizokuwa wameziomba kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 23/24, Dkt Matolo alitoa ufafanuzi kuwa ingawa ni kweli walikuwa wameomba fedha hizo, lakini mpaka mwaka wa fedha wa bajeti uliomalizika Juni 30 mwaka huu,  hakuna kiasi chochote cha fedha kilichotolewa na hazina ya serikali.

Alisema wanatajia bajeti waliyowasilisha kwa serikali kwa mwaka huu wa fedha 24/25 ambayo ni Shilingi Bilioni 17 zitatoka kwa wakati ili kampuni hiyo anayoiongoza iweze kukamilisha malengo waliyojiwekea.

Tanapa Investment Ltd ilianzishwa mwaka 2019 kwa ushauri wa Serikali baada ya kubaini changamoto mbalimbali kutoka kwa makandarasi wa nje ikiwamo kutokukamilisha miradi yao kwa wakati.

Aidha miradi mingine ilitengenezwa chini ya kiwango na hivyo kuilazimisha Serikali kukatisha mikataba na hivyo kusababishia hasara kubwa pamoja na upotevu wa raslimali muda.

Like
1