Tamu chungu ya usajili wa Messi PSG

BAADA ya Lionel Messi kujiunga na PSG, athari, msukumo na ushawishi alionao katika ulimwengu wa soka barani Ulaya vimejidhihirisha kuwa mkubwa sana kuwahi kutokea kwani tangu nguli huyo alipojiunga na timu yake mpya ya Paris St-Germain, Jumanne wiki hii, kwa wachache imekuwa neema lakini kwa wengine wengi, imekuwa kama jinamizi.

PARIS ST-GERMAIN:

Kwa PSG, hii ni neema kubwa kuwahi kutokea klabuni hapo tangu ulipofanyika uwekezaji mkubwa na Qatar Sports Investment wakiongozwa na rais wa klabu hiyo Nasser El-Khelaifi walipowasili rasmi mwaka 2011.

Ni wazi PSG wanatarajia kupata faida kubwa sana kupitia njia tofauti tofauti, Jana asubuhi, kabla ya duka mahsusi la timu hiyo kufunguliwa, kulishuhudiwa idadi kubwa sana ya masahabiki waliopanga foleni ndefu mno, wakingoja duka lifunguliwe ili wanunue jezi zenye jina la Messi. Imetabiriwa kuwa kwa dunia nzima, mauzo yanatarajiwa kufikia uniti 200,000 mpaka 300,000 ndani ya siku chache tu.

Si mauzo ya jezi pekee bali pia udhamini kwa timu hiyo unatarajiwa kukua kwa kasi.
Gazeti la Ufaransa maarufu kama L’Equipe, limeripoti ongezeko la wafuasi wapya 850,000 kwenye ukurasa wa Instagram (ongezeko la asilimia 4), kwa Facebook wameongezeka wafuasi 200,000 wa timu hiyo kwa usiku mmoja tu baada ya Messi kujiunga nao.

Ni dhahiri kuwa sio kwa maajabu ya uwanjani aliyonayo Messi, bali ni kivutio cha watalii pia na hivyo watu wamekuwa wakimiminika kutoka sehemu mbalimbali duniani kwenda kumuona Messi kwenye mchezo dhidi ya Strasbourg wiki hii. Mpaka sasa, tiketi za mchezo huo zinauzwa kwa Euro 1,500.

Kwa usajili wa Messi, unategemewa kuwanufaisha PSG kwenye uwanja lakini pia kibiashara na kiuchumi kwa ujumla.

Kwa nchi ya Rwanda, kutokana na udhamini wao kwa PSG, uwepo wa Messi kama balozi wao, unatarajiwa kuwanufaisha sana kiutalii na baada tu ya kusajiliwa Messi alionekana akiwa amevaa fulana iliyoandikwa Visit Rwanda. Tanzania bado tumelala!

KYLIAN MBAPPE KUMKIMBIA MESSI?

Ujio wa Messi PSG, si neema kwa wote klabuni hapo kwani tayari kinda nyota, Kylian Mbappe 21, inasemekana kuwa anataka kuondoka klabuni hapo ili kuepuka kufunikwa na kivuli cha Messi.

Mpaka hii leo, inasemekana hakuna maelewano mazuri kati ya viongozi wa Real Madrid na PSG kwani PSG wanawashutumu Madrid kumlaghai Mbappe na ndio sababu amegoma kusaini kandarasi mpya mpaka sasa.

Mbappe ameweka bayana kuwa hayuko tayari kusaini kandarasi mpya hivyo kama hauzwi sasa, ataondoka bure msimu ujao.

BARCELONA

Kwa Barcelona, hiki ni kipindi kigumu sana kwenye historia ya imu hiyo kwani mpaka sasa imeripotiwa kwamba kuondoka kwa Messi klabuni hapo, kumewafanya thamani ya timu imeshuka kwa Euro milioni 137, wamepoteza Euro milioni 77 zitokanazo na ushuru na mauzo ya jezi yameshuka kwa asilimia 80.

Licha ya Messi kuondoka klabuni hapo, Barcelona watapaswa kumlipa Messi kitita cha Euro milioni 39 kama bonsai ingawa hakusaini mkataba mpya. 

PAUL POGBA

Kiungo nyota wa Manchester United Paul Pogba, 28, ameripotiwa kukataa kusaini kandarasi mpya na timu yake hiyo kwa matumaini ya kujiunga na PSG ambao walikuwa wameandaa dau la  Euro milioni 40 ili kumnasa kiungo huyo.

Baada ya ujio wa Messi PSG, usajili wa Pogba kwenda PSG msimu huu, hautawezekana na hivyo gazeti la Metro la nchini Uingereza limeripoti kuwa Pogba ataondoka Manchester kama mchezaji huru msimu ujao.

Majadiliano juu ya kandarasi mpya kati ya Pogba na Manchester United yamekuwa yankisuasua sana kwani Pogba aliripotiwa kukataa ofa ya kuongeza mkataba ya mwisho kutoka klabuni hapo. 

Like
3