KAULI ya Rais Samia Suluhu Hassan kwamba ameamuriu Taasisi ya Kuzuia na Kupabana na Rushwa (Takukuru) ifute kesi 147 ilizobambikia wananchi, imethibitisha kuwepo kwa “mchezo mchafu” unaendelea kwenye taasisi za usalama nchini dhidi ya raia.
“Takukuru wamefuta kesi 147 ambazo walibambikizia watu,” amesema Rais Samia jana Jumanne Mei 18, 2021 wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha ushonaji, Bohari Kuu ya Jeshi la Polisi, Kurasini jijini Dar es Salaam. Kiwanda hicho kimejengwa kwa Sh. milioni 666.4.
SAUTI KUBWA imezungumza na wananchi kadhaa wa kada mbalimbali jijini Dar es Salaam na maeneo mengine, wakieleza kwamba kauli ya Rais Samia inakiri kuwepo kwa vitendo vya kubambikia kesi na tuhuma za uongo kwa wananchi, huku ikielewa kuwa kilio hicho kimekuwa kikipazwa na wengi, lakini wakiipuzwa.
Rais Samia alieleza kuwa kilio cha kubambika kesi na tuhuma mbalimbali kwa wananchi, hakiko Takukuru pekee, bali taasisi na idara zingine za usalama wa nchi.
“Nawataka hata Polisi kupunguza kesi za kubambikiza watu” alisisitiza Rais Samia.
Wakili na mtetezi wa haki za binadamu, Jebra Kambole anaeleza kauli ya Rais Samia inathibitisha kuwepo kwa vitendo hivyo nchini na kwamba ni wakati muafaka sasa akiwa kiongozi mkuu wa Tanzania, kuhakikisha anakomesha hali hiyo.
Jebra anasisitiza kwamba ni vyema Rais Samia akaacha kusema Polisi na Takukuru wapunguze matukio ya kubambikiza kesi, bali ahakikishe anakomesha kabisa.
“Watu wengi wamefurahi kusikia Mama Samia (Rais) akitaka vyombo vya usalama kupunguza kuonea wananchi wake kwa kupunguza matukio ya kubambikia watu kesi, lakini mimi naona akomeshe kabisa,” alisisitiza wakili huyo na kuongeza, “watu wengi sana wameonewa kwa mtindo huo.”
Rukia Mfinanga, mwanasheria anasema anaamini idadi kubwa ya watu wenye kesi wanateswa kwa makosa wasiyofanya; kwamba walibambikiwa na taasisi za usalama, ikiwamo Jeshi la Polisi, Takukuru na idara zingine.
“Ukisikiliza watuhumiwa wengi wa makosa makubwa, wengi wamebambikiziwa na hii ni njia inayotumika sana kwa baadhi ya watendaji wa taasisi za usalama kutaka rushwa, mtu anapogoma kutoa, basi wanambambikiza kesi,” anasema Rukia.
Mbunge wa zamani wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa alisema akiwa mbunge alipiga kelele sana kuhusu suala hili, lakini hakuna aliyesikiliza wala kuchukua hatua.
“Nimefurahi kusikia mheshimiwa Rais Samia analisema hili, lakini kikubwa zaidi ni kuhakikisha anamaliza tatizo hili, ni dhambi mbaya sana kubambikia mtu kesi,” aliongeza Msigwa ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.
SAUTI KUBWA inazo taarifa za kushamiri kwa mtindo wa kubambikia watu kesi katika vituo vidogo vya Polisi ambako “vijana” wamekuwa wakiteseka kwa kuwekwa mahabusu kwa makosa ya kubambikwa ili waweze kutoa rushwa.
Makosa mengi katika vituo hivyo wanayobambikiwa wananchi ni pamoja na kukutwa na bangi au dawa za kulevya pamoja na mauaji, ikiwa baadhi ya askari wanataka rushwa kubwa.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime amesema tuhuma kuwepo baadhi ya askari wa jeshi hilo wakibambikizia watu kesi, zipo na kwamba wamekuwa wakipokea malalamiko hayo na kuyafanyia kazi.
Anasema wapo baadhi ya askari waliofukuzwa kazi kutokana na kubainika kuhusika na vitendo hivyo vinavyokandamiza haki za wananchi.
“Tumekuwa tukichukua hatua na jeshi haliruhusu wananchi kuonewa kwa njia yyoyote ile ikiwamo kubambikiza kesi, sheria na taratibu zetu zinatutaka kufanya kazi kwa weledi, kwa kulinda na siyo kuonea wala kuangamiza,” alisisitiza Misime.