TAKUKURU, JKT Mzinga lawamani kwa “kumdhulumu” Askofu Rweyongeza

VYOMBO vya dola vimemnyanyasa Askofu Almachius Rweyongeza wa Jimbo Katoliki la Kayanga, mkoani Kagera, kwa siku tatu mfululizo sasa kutokana na deni ambalo anadaiwa na Kampuni ya Ujenzi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mzinga, kiasi cha shilingi milioni 135.

SAUTI KUBWA inafahamu kuwa Jumamosi tarehe 13 Februari, kikosi maalumu cha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kilimweka askofu huyo chini ya ulinzi mkali na kumsafirisha hadi Bukoba Mjini kwa mahojiano, akiwa na mapadri wake wawili – Herman Kalimwenjuma na Hans Humer – chini ya mtutu wa bunduki.

Baada ya mahojiano, na baada ya kubembelezwa na askofu na viongozi kadhaa wa kanisa, maofisa wa TAKUKURU walimrudisha Askofu Rweyongeza kwenye makazi yake Kayanga kimya kimya na kwa sharti kwamba wanamruhusu aongoze misa za Jumapili ili kutoleta msukosuko kwa waamini lakini baada ya hapo ahakikishe anatafuta pesa za kulipa deni hilo, vinginevyo hawatoki kwenye eneo lake, naye haruhusiwi kutoka. Wamekuwa pale tangu Jumamosi usiku wakisubiri kulipwa pesa zao.

Hadi tunaenda mitamboni, leo Jumatatu usiku, mapadri wake wawili bado wapo rumande Bukoba mjini, huku jitihada za kuwatoa zikiendelea.

Leo Jumatatu tarehe 16, baada ya taarifa hizi kuenea mitandaoni tangu jana, na katika jitihada za kanisa na serikali kuokoa sura zao, Waziri Innocent Bashungwa, ambaye ni mbunge wa Karagwe, alimtembelea Askofu Rweyongeza, wakapiga picha sebuleni na mbele ya jengo, halafu waziri akaposti picha hizo katika akaunti ya Instagram.

Hakutaja kabisa sakata linalomkabili Askofu lakini ilieleweka kuwa tukio hilo lilikuwa sehemu ya propaganda za “kufunika” sakata hili.

Awali ilisemekana kwamba Askofu anadaiwa shilingi milioni 73 ambazo JKT Mzinga walizifanyia kazi akagoma kuwalipa, lakini baadaye imebainika kuwa kiasi wanachomdai ni shilingi milioni 135.

Chanzo za tatizo

Rweyongeza ni askofu mwanzilishi wa Jimbo la Kayanga. Wakati linazinduliwa, alimkuta Pd. Hans Humer kutoka Austria akiwa amesimamia ujenzi wa Kanisa Kuu na nyumba ya zamani ya Askofu.

Baada ya muda mfupi, alianza kugombana na watu aliodai si waaminifu kwake. Akamfukuza aliyekuwa Katibu wake Padri Benezeth Birusya (ambaye baadaye aliamua kuacha upadri), na akamfukuza makamu wake (vicar general) Padri Rwechungura.

Baadaye, makamu aliyefuata, Padri Fortunatus Bijura, alijiuzuru katika mazingira ambayo baadhi ya wasaidizi walidai yaliashiria “ukiukwaji wa nadhiri za kiaskofu.” Askofu akakaa miaka miwili bila vicar general wala katibu.

Hali hii imesababisha udhaifu wa kiuongozi na migogoro ya kiutawala katika jimbo hilo, huku kukiwa na makundi ya mapadri, watawa na waamini wanaozozana na askofu chinichini (na wengine kwa uwazi). Migogoro hii imerahisisha kashfa za askofu kuvuja kirahisi.

Askofu avunja mkataba wa JKT Mzinga

Taarifa tulizonazo zinadai kuwa mgogoro wa sasa unatokana na Askofu Rweyongeza kuvunja mkataba kibabe na kampuni ya ujenzi  ya JKT Mzinga.

Aliipa kampuni hiyo kandarasi ya kujenga jengo la shule ya awali na baadaye ikasaini mkataba kujenga jengo jipya la uaskofu lenye orofa tatu. Kampuni ilichora michoro yote na kuandaa gharama kisha ikapima udongo. Kabla haijaanza kujenga, Askofu aliifukuza kibabe na kuajiri wakandarasi wengine.

“Kampuni iliyojenga ni ya mfukoni, na inamilikiwa na kijana aitwaye Process Mwemezi, aishiye jirani na askofu, na ndiye anasimamia ujenzi wa kiwanda cha maziwa cha bwana mkubwa,” chanzo kutoka Kanisani kimesema.

Padri mwingine amesema: “JKT Mzinga pia ilijenga zahanati ya Kijiji cha Kibombo lakini haikuisha kwa sababu Askofu aliingilia mchakato, akamnyang’anya Padri Herman milioni 200. Padri Herman alikuwa amekusanya fedha hizo yeye mwenyewe kutoka kwa rafiki zake nje ya nchi.

“Askofu anatumia ukabila katika masuala ya fedha. Hata mkubwa wa JKT Mzinga aliyekuwa amewaleta kwake, alikuwa rafiki yake, lakini amestaafu. Askofu yumo kwenye vikao na mapadri wapambe kutafuta fedha, na katika hatua za awali waliamua wauze ardhi na Kituo cha Afya Kibombo.”

Kampuni hiyo imekuwa inamdai ailipe gharama za kazi ya awali lakini askofu akapuuzia. Baadhi ya mapadri wake wanadai kwamba askofu alichukua fedha kwenda kulipa lakini alizitumia kwa mambo mengine.

Yapo madai pia kuwa zilichukuliwa  fedha nyingine za Bima ya Afya kutoka St. Mary’s Hospital Isingiro (hospitali ya Kanisa) ambazo alizitumia kwa mambo mengine kinyume cha taratibu. Wanadai askofu alishauriwa asifanye hivyo lakini alikaidi. Wengine wanasema alitumia ubabe wa kiaskofu kupuuza madai ya JKT Mzinga.

Kutokana na mgawanyiko ulioko jimboni, baadhi ya “wapinzani” wa askofu walitumia udhaifu wake wakatoa taarifa kwa JKT Mzinga na TAKUKURU mkoani Kagera.

Maofisa wa JKT Mzinga na TAKUKURU walifika Karagwe Jumamosi na kumuita kwa mahojiano pamoja na mapadri Hans na Herman. Yeye alijaribu kukaidi, akawekwa ndani kwa saa chache kabla hajapelekwa Bukoba kwa mahojiano zaidi.

Askofu alirejeshwa kwake Jumamosi usiku, Jumapili akaongoza misa asubuhi akiwa chini ya ulinzi wa siri. Maofisa wa kikosi maalumu cha TAKUKURU walikuwemo kanisani, na walimruhusu aongoze ibada ili kuepusha taharuki kwa waamini kwa sababu walishauriwa wamalize jambo hili kimya kimya.

Jumapili baada ya misa, Askofu Rweyongeza aliitisha kikao kirefu hadi usiku kutafuta ufumbuzi wa jambo hili. Kikosi maalum kilibaki makao ya Askofu kusubiri malipo yao.

Jitihada za kulipa deni kimya kimya zaendelea

Jumapili na Jumatatu zimetumika kutafuta fedha kwa njia mbalimbali. Baadhi ya vyanzo vyetu vya habari vimesema kuwa mmoja wa watu walioahidi kumsaidia askofu katika sakata hili ni Mkuu wa Wilaya ya Karagwe ambaye amekuwa anachangisha baadhi ya wafanyabiashara wa Karagwe ili wamnusuru askofu.

Hata hivyo, baadhi yao wameiambia SAUTI KUBWA kuwa wamegoma kuchanga kwa madai kuwa hawana uhakika iwapo pesa watakazompa mkuu wa wilaya zitafikishwa kwa askofu.

Katika jitihada binafsi na kwa kutumia vyanzo vya mapato vya jimbo, askofu amewataka baadhi ya mapadri wanaosimamia miradi kadhaa jimboni wachange pesa (wengi wao kwa kulazimishwa) kwa ajili ya kumaliza sakata hili. Mmoja wa mapadri anasema amenyang’anywa kiasi cha shilingi milioni 68.

Baada ya kuzikusanya, askofu ametuma watu wake Bukoba mjini wafanye malipo ya awali ili mapadri wake wawili – Hans na Herman – waachiwe huru. Kabla hawajafika Bukoba, Bashungwa alipopata taarifa hizo, akamshauri askofu awazuie watu hao kulipa pesa hizo ili kwanza yeye (waziri) awasiliane na Rais John Magufuli, ili aingilie kati.

Hadi tunakwenda mitamboni, wajumbe wa askofu walikuwa hawajalipa fedha hizo, na mapadri walikuwa bado wapo rumande, huku uongozi wa jimbo ukisubiri simu kutoka kwa Waziri Bashungwa ili kupata uamuzi wa Rais Magufuli.

Awali, kabla ya madai haya ya JKT Mzinga kujitokeza hadharani, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliandika barua (nakala yake tunayo) kwa Jimbo la Kayanga kuhusu madai ya kodi zipatazo milioni 600. Barua hiyo ni ya tarehe 5 Februari 2021.  

Kodi hizo ni malimbikizo ya kodi ya moja ya  hospitali za Jimbo hilo. Zipo taarifa kuwa Askofu huyo anadaiwa zaidi ya shilingi bilioni mbili za kodi ya ardhi.

Askofu akanusha taarifa

Baada ya taarifa hizi kuvuja mitandaoni, waamini na mapadri kadhaa, marafiki na ndugu wa Askofu Rweyongeza wamekuwa wanafuatilia kinachoendelea, huku wengine wakimtumia ujumbe wa kumpa pole na kumtia moyo, na wengine wakiuliza ili wapewe ukweli juu ya kinachoendelea.

SAUTI KUBWA imeelezwa kuwa kutokana na jinsi taarifa hizo zilivyoenea, na kwa kuwa zilisambazwa na watu ambao serikali mkoani Kagera inawaona kama “wabaya” wake, iliamua kuingilia kati kufanya mambo mawili.

Kwanza, ilishauri askofu aachiwe huru ili apewe muda wa kutafuta fedha na kuzilipa ili mapadri wake nao waachiwe na suala liishe kimya kimya. Pili, serikali ilimpatia sharti yeye akanushe taarifa za kutiwa msukosuko na kuwekwa chini ya ulinzi.

Kwa sababu hiyo, leo Jumatatu Askofu Rweyongeza alisambaza ujumbe wa maandishi usemao:

“Tumsifu Yesu Kristu. Poleni sana kwa taharuki iliyosababishwa na habari hiyo ya uzushi na uchochezi usio na maana. Mimi niko salama salimini nikiendelea na utume kama kawaida. Asante sana kwa kujali. Tuombeane utakatifu. Bikira Maria wa amani, utuombee.”

Mwandishi wa habari hizi alipowasiliana naye kuhusu sakata hili, akampa pole na kumuuliza maswali, Askofu Rweyongeza hakujibu maswali aliyoulizwa, bali aliandika maneno yafuatayo:

Asante kwa pole. Habari hizo ni za uzushi tu na uchochezi. Mimi niko huru na salama salimini.”

Hata hivyo, mapadri wake na baadhi ya maaskofu wenzake wamethibitisha sakata hilo. Wengine waliozungumzia suala hilo kwa uchungu ni ndugu, rafiki na jamaa wa mapadri wawili waliowekwa rumande tangu Jumamosi.

Mmoja wa ndugu hao amesema: “Askofu anatuma ujumbe kutwambia kuwa yuko salama. Je, ana furaha gani ya kuwa huru wakati mapadri wetu Hans na Herman wapo rumande? Kwani akisema ukweli kuwa ametiwa msukosuko kwa kutolipa madeni atapoteza kitu gani?”

Mwingine amesema: “Hata wakicheza sarakasi, suala hili halifichiki tena. Madeni yapo, JKT Mzinga wapo, TAKUKURU wapo, na hatua hizi zimechukuliwa. Hata baadaye wakubwa wakiingilia kati, haiondoi ukweli kuwa baba askofu na watu wake wamekamatwa na kutiwa msukosuko. Wawe wakweli.”

Chanzo chetu kutoka JKT Mzinga kimesema: “Tunafahamu kuwa askofu ni shabiki wa rais wetu na amekuwa anamuunga mkono katika jitihada zake zote, lakini deni letu si la kisiasa. Hata rais alitupatia ruksa majuzi kuwa tuchukue hatua kali kama hizi kwa wadeni sugu hata kama ni mawaziri. Nakwambia, hata wanasiasa wakiingilia kati, atazilipa tu.”

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wenzake wa dini wanasema hata kama ni kweli askofu anadaiwa, si sahihi kuchukuliwa hatua za kumdhalilisha na kumlipisha nje ya utaratibu rasmi wa kisheria, jambo ambalo linachochea wizi na ufisadi kwa kutumia vyombo vya dola.

Kiongozi mmoja mwandamizi wa Kanisa Katoliki (ambaye aliomba asitajwe jina) alihoji: “Sawa Askofu anadaiwa. Lakini madai yana sheria zake. Zitumike kumdai, badala ya kumdhalilisha yeye na mapadri wake na kanisa zima. Hii ni dhuluma. Kwani sheria za nchi hazina nafasi katika utawala huu?”

SAUTI KUBWA inatambua kuwa askofu na watu wake walitamani sakata hili liishe kimya kimya ili lisilete taharuki kwa waamini, lakini baadhi ya waamini hao ni sehemu ya sakata lenyewe. Baadhi yao wamo kanisani, wengine Mzinga JKT, na wengine TAKUKURU. Wanajua kinachoendelea, na wanasema.

Mmoja wao amesema: “Kwa sehemu kubwa, suala hili amelikuza Baba Askofu mwenyewe kwa kutokuwa mkweli na kusimama na watu wale wale wanaomdhulumu.”

Like